PINDA: NITAFURAHI NIKIONDOLEWA

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda uwaziri mkuu ni mzigo anaobeba kama Msalaba na ikiwa ataondolewa, atafurahi kwa kuwa atapumzika. Alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Kassim Mohamed (CUF), katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo.“Rais akiniambia nimeshindwa majukumu nitaondoka, huku nikiwa na kicheko, hata ninyi wabunge mna nafasi ya kuniondoa, mnaweza kufanya hivyo mkiona inafaa kwani nitafurahi na kupumzika,” alisema.Rukia katika swali lake, alimtaka Pinda kutoa ufafanuzi kuhusu kauli za wabunge wa CCM kuwa yeye ndiye mzigo. Alisema licha ya jitihada anazofanya kutekeleza wajibu wake kwa kusimamia wizara 20, anashangaa kuhukumiwa kwa upungufu unaotokea katika wizara moja au mbili.Alifafanua, kuwa anasimamia wizara kama 20 na zote zinafanya kazi vizuri, lakini kama kuna wizara moja au mbili hazijafanya vizuri sana, hiyo haitoshi kudai atimuliwe kazi.Alisema uzuri wa nafasi ya uwaziri mkuu, mtu haombi, bali anateuliwa na Rais kwa majaaliwa ya Mwenyezi Mungu, hivyo isipompendeza, ni kazi rahisi kwa Rais ambaye atamwambia kuwa ameshindwa jukumu lake na kumwondoa.“Bunge pia mnaweza kumwondoa Waziri Mkuu kwa uwezo wenu, hivyo dada Rukia kama unafikiri hilo na wabunge wote wakaona sawa, nipo tayari, tena nitafurahi kweli kweli angalau nimeutua Msalaba huu, mana’ke hii kazi ni ngumu,” alisema.Katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua kauli ya Waziri Mkuu iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuwa kuna baadhi ya mawaziri ni mizigo alipokuwa katika ziara yake mkoani Mbeya.Akijibu swali hilo, Pinda alisema hata yeye alisikia kauli hiyo kwenye vyombo vya habari akasema ni vema kumsubiri Kinana arudi kutoka katika ziara na kumsikiliza alichosema alikuwa na nia gani, ndipo wataona namna ya kwenda mbele zaidi.Hata hivyo, aliyesema bungeni kuwa Pinda ni mzigo kwa Serikali alikuwa Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) akisema ndiye ambaye anastahili aondolewe kwenye nafasi yake hiyo.Pia Waziri Mkuu alimwahidi Mbunge wa Mkanyageni, Habib Juma Mnyaa (CUF), kufuatilia kwa nini suala la kupeleka fedha za chenji ya rada hazijafikishwa Zanzibar. Alisema suala hilo lilishazungumzwa ndani ya Serikali wakakubaliana na likaisha.Aliongeza kuwa suala hilo ni la kisekta na litatolewa ufafanuzi zaidi na waziri husika. Katika swali lake la awali, Mnyaa alimwuliza Waziri Mkuu ni kwa nini hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya kauli iliyotolewa bungeni ya kushughulikia suala la chenji ya rada kupelekwa Tanzania Bara pekee.

Comments

Popular Posts

MKUTAO WA G7 KUANGAZIA USALAMA NA MAZINGIRA

CHEKI PICHA HIZI ALIZOWEKA NICKI MINAJ INSTAGRAM

ZIFAHAMU NCHI ZINAZOZUNGUMZA KISWAHILI BARANI AFRIKA

WAFAHAMU WAIGIZAJI 10 WA KIUME WENYE MVUTO KOREA 2017

HISTORIA YA KOMBE LA DUNIA TANGU 1930, WAANDAAJI & WASHINDI

WAFAHAMU WAIGIZAJI 10 WA KIKE WA KOREA AMBAO NI WAREMBO KWA MWAKA 2017

BIBI WA MIAKA 85 AKAMATWA KWA KUIBA HERENI

MAMBO YA MUHIMU KUFAHAMU NA KUZINGATIA KABLA YA KUCHAGUA KOZI (TAALUMA) CHUO KIKUU

WAFAHAMU MATAJIRI 10 WA TANZANIA MWAKA 2018