Kikwete kumuaga Mandela leo

RAIS Jakaya Kikwete leo ataungana na viongozi wenzake kutoa heshima za mwisho na kuuaga rasmi mwili wa kiongozi mashuhuri wa Afrika Kusini na duniani, Nelson Mandela. Mwili wa Mandela unatarajiwa kuwekwa kwenye majengo ya Urais wa Afrika Kusini ya Union Buildings mjini Pretoria, ambayo sasa yataitwa Majengo ya Kumbukumbu ya Mandela.Jana Rais Kikwete aliungana na viongozi wa mataifa mbali mbali duniani na maelfu ya wananchi wa Afrika Kusini, kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Mandela.Maelfu kwa maelfu ya wananchi walihimili mvua kubwa iliyokuwa inanyesha kwa nguvu kwenye Uwanja wa Michezo wa FNB mjini Johannesburg, kumwaga Mzee Mandela ambaye alikuwa ishara kuu ya upinzani wa siasa za ubaguzi wa rangi za makaburu wa Afrika Mashariki.Baada ya kutoka jela, Februari 1990, Mandela alichaguliwa kuwa Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini mwaka 1994.Hata hivyo, Mandela alitumikia kipindi kimoja tu cha miaka mitano na kukataa kutumikia kipindi cha pili. Viongozi 91 kutoka sehemu mbalimbali duniani walihudhuria kumbukumbu hiyo iliyokuwa na kila aina ya mchanganyiko wa hisia, wengine wakiwa na majonzi na wengine wakicheza na kuimba kwa muda wote wa shughuli hiyo iliyochukua saa tano.Mbali na Rais Kikwete ambaye amefuatana na mkewe Mama Salma, marais wengine mashuhuri duniani waliohudhuria kumbukumbu hiyo ni Barack Obama wa Marekani, Francois Hollande wa Ufaransa, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroun na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon.Kumbukumbu hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi wa zamani wa Marekani wakiwemo marais watatu wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter, Bill Clinton na George Bush na mawaziri wakuu wawili wa zamani wa Uingereza, Tony Blair na Gordon Brown.

0 comments:

Post a Comment