JELA MIAKA 30 KWA UNYANG'ANYI WA KUTUMIA SILAHA
Wakazi wawili wa vijiji vya Nyabisaga Kata ya Pemba wilayani Tarime mkoani Mara, Mhoni Chacha Ng’wena (25) na Isack Magawi Meng’anyi (30), wamehukumiwa kwenda jela miaka 30 kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya unyang’anyi wa kutumia silaha. Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama ya Wilaya ya Tarime.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tarime, Adrian Kilimi alisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka, ukiongozwa na Inspekta Usu, George Lutonja kwamba washitakiwa walitenda kosa la unyang’anyi wa silaha.Alisema Mahakama imeridhika na ushahidi, ulioambatana na vielelezo vya mlalamikaji, vilivyokamatwa kwa watuhumiwa hao, vikiwemo baiskeli, simu ya mkononi, viatu na tochi.
Awali, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Inspekta Usu Lutonja alidai kuwa washitakiwa hao pamoja Januari 3, mwaka huu saa 12 alfajiri, wakiwa na silaha za jadi za mapanga na marungu walivamia na kuingia ndani ya nyumba ya Selestin Omahe, mkazi wa Sirari na kumshambulia na familia yake na kupora vitu vya ndani, vikiwemo baiskeli aina ya Phoenix, simu ya mkononi, viatu na tochi, vyote vyenye thamani ya Sh 284,000.Alidai baada ya tukio hilo, mlalamikaji Omahe alipiga yowe, kuomba msaada na majirani, ambao walitokea pamoja na polisi, waliokuwa doria eneo hilo. Hata hivyo, hawakufanikiwa kukamata washitakiwa hao wakiwa na mali za mlalamikaji.
Baada ya kukamatwa, washitakiwa walifikishwa kwenye vyombo vya sheria, ambapo upande wa mashitaka ulileta mashahidi wanne na vielelezo, vilivyokamatwa kwa washitakiwa wakati wa tukio hilo. Washitakiwa hao waliomba wasamehewe. Mwendesha Mashitaka aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa washitakiwa. Hakimu Kilimi alisema anawahukumu kwenda jela miaka 30 kila mmoja ili iwe fundisho kwa watu wenye tamaa ya kupora mali za watu.
Chanzo: Habari Leo
Comments
Post a Comment