Showing posts with label Kitaifa. Show all posts
Showing posts with label Kitaifa. Show all posts

KAMPUNI YA ACACIA KUPUNGUZA SHUGHULI NA WAFANYAKAZI NCHINI

Kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia imesema itapunguza wafanyakazi na shughuli zake za migodini ikiwa ni sehemu ya athari ya uzuiaji wa usafirishwaji wa makinikia uliowekwa na serikali ya Tanzania mwezi Machi mwaka huu.

Kampuni hiyo inasema wakati baadhi ya shughuli ndani ya mashimo yake ya dhahabu zitasimama, ndani ya wiki nne, uchenjuaji wa makininia pia nao utasimama.

"Kwa masikitiko, mpango huu utapelekea kupunguzwa kwa ajira kati ya wafanyakazi 1,200 waliopo hivi sasa na wanakandarasi 800" kampuni hiyo imesema kwenye taarifa.

Hata hivyo Acacia hawajasema ni wafanyakazi wangapi hasa watakaopunguzwa kazini.

Kampuni hiyo ambayo imeorodheshwa katika soko la hisa la London nchini Uingereza inasema kusimamishwa kwa usafirishwaji wa makinikia kumekuwa kukiikosesha takribani $15 milioni (Dola milioni kumi na tano) kwa mwezi.

Acacia wanasema hali hiyo imesababisha uendeshaji wa siku hadi siku wa moja ya migodi yake mikubwa Bulyanhulu kuathiriwa kwa kiasi kikubwa.

Acacia imekuwa katika mgogoro na serikali ya Tanzania kwa takribani miezi sita sasa tangu serikali ya Tanzania izuie usafirishwaji wa makinikia ya kampuni hiyo nje ya nchi.

Lakini serikali ya Tanzania pia imekuwa ikiishutumu kampuni ya Acacia kwa kukwepa kulipa kodi inayostahili, tuhuma ambazo kampuni hiyo imezikanusha.

Mazungumzo yanayolenga kutatua mgogoro huu bado yanaendelea.

"Kampuni ina matumaini kwamba majadiliano yanayoendelea kati ya Barrick na serikali ya Tanzania yatatatua kuzuiwa kwa usafirishaji wa makinikia na kurudisha mazingira ya uendeshaji wa mgodi wa Bulyanhulu katika hali nzuri" inasema taarifa ya Acacia.

Mapema mwaka huu Rais John Magufuli aliamuru uchunguzi wa kina katika sekta ya madini nchini Tanzania huku akiamini kwamba Tanzania hainufaiki vya kutosha kutokana na sekta ya madini.


Chanzo: BBC

MMILIKI WA NGURDOTO HOTEL AFARIKI DUNIA


Mfanyabiashara maarufu nchini, Maleu Mrema amefariki dunia jana akiwa kwenye matibabu nchini Afrika Kusini.

Akizungumza na Mwananchi ndugu wa marehemu,Vincent Laswai alithibitisha msiba huo akiwa nyumbani kwa marehemu eneo la Uzunguni jijini Arusha.

Akihojiwa na gazeti la Mwananchi Laswai amesema kwamba alipokea taarifa za kifo cha marehemu jana saa 12 jioni na uongozi wa familia utatoa taarifa za kifo cha mfanyabiashara huyo leo.

Laswai, amesema kwamba ni mapema kuzungumzia chanzo cha kifo kwa sababu bado hawajapata taarifa kutoka katika hospitali aliyokuwa akitibiwa nchini humo.

Hivi karibuni marehemu Mrema alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kiafya ambapo Juni mwaka huu alipelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu.



Chanzo: Mwananchi

WABUNGE: "BILA KILIMO KWANZA HAKUNA SERIKALI YA VIWANDA"

 
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamesema bila kuwekeza katika kilimo, azima ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda haitatimia.

Kadhalika, wameipongeza Serikali kwa kuondoa tozo 108 zilizokuwa kero kwa wakulima na kuitaka Serikali kuhakikisha tozo zilizoondolewa zinawanufaisha zaidi wakulima na Watanzania, badala ya kuwanufaisha wafanyabiashara pekee. Waliyasema hayo jana kwa nyakati tofauti bungeni Dodoma wakati wakichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa Fedha 2017/18.

Mbunge wa Viti Maalum, Mariam Ditopile (CCM), alisema kama Tanzania inataka kuwa ya viwanda, haina budi kuwekeza katika utafiti kwa ajili ya sekta ya kilimo ili kubaini namna bora zaidi za kutumia rasilimali na fursa zilizopo ili kuimarisha kilimo na hivyo kusaidia kufikia haraka azima ya kujenga Tanzania ya viwanda. Alisema tayari fursa za kuinua kilimo na kukifanya uti wa mgongo nchini zimeanza kuonekana kwani kwa sasa Tanzania ndiyo inayouza vyakula na bidhaa za biashara katika nchi mbalimbali duniani zikiwemo nchi za Sudan, Kenya na Uganda wanaonunua mazao ya chakula kama mahindi.

“Nchi kama India inanunua kwetu korosho, choroko na tumbaku. Kwa sasa mipango ni kuipeleka nchi kwenye viwanda ni wakati muafaka wa kuwekeza kwenye kilimo kwa kufanya utafiti za kisayansi za namna bora ya kuendeleza kilimo chetu kwa sababu kilimo ndio ajira, chakula na fedha,” alisisitiza. Alisema Tanzania inasifika kwa kufanya utafiti, lakini pamoja na kuwa na uwezo huo bado haujatumika vizuri kuendeleza mambo ya msingi yakiwamo maeneo ya kilimo, mifugo na uvuvi.

“Kwa mfano sisi ndio wenye eneo kubwa katika Ziwa Victoria, lakini takwimu za kidunia zinaonesha Uganda yenye sehemu ndogo katika ziwa hilo ndiyo inayoshika nafasi ya juu; ya sita duniani kwa uvuvi huku sisi Tanzania tukishika nafasi ya nane,” alisema. Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM) aliitaka serikali iwekeze kwenye utafiti wa kilimo ili kuyabaini maeneo ya kijiografia na kisayansi yanayoweza kuikuza kwa kasi sekta hiyo ya kilimo inayokwenda sambamba na sekta ya viwanda.

“Kwa mfano Morogoro ina udongo wenye rutuba na mito inayotiririsha maji kwa mwaka mzima, utafiti ukifanyika wa namna bora ya kutumia rasilimali hizo, ni wazi kuwa Morogoro pekee inaweza kulisha Tanzania nzima,” alisema. Pamoja na hayo mbunge huyo alisema si kweli utitiri wa kodi zilizofutwa na serikali umewalenga zaidi wafanyabiashara na wenye kampuni na si wakulima kwa kuwa wafanyabiashara na kampuni hizo kutokana na kufutwa kwa tozo hizo kuanzia sasa watanunua mazao na bidhaa hiyo kwa bei inayostahili.

Kwa upande wake Mbunge wa Hanang, Mary Nagu (CCM), alisema serikali haina budi kuzingatia kuwa kilimo ndicho kinachochangia ajira kwa Watanzania takribani asilimia 65, kinachozalisha chakula kwa Watanzania kwa asilimia 100 na kuingiza asilimia 28 katika pato la taifa. “Hii ni sekta muhimu sana, ni vema Serikali ione umuhimu wa kuifanyia mageuzi sekta ya kilimo na kuongeza bajeti ya wizara ya kilimo kwani hali ilivyo sasa badala ya kilimo kukua, kinashuka kwa kasi,”alisema.

Alisema takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2011 kilimo kilikuwa kwa wastani wa asilimia 3.5 lakini miaka sita baadaye yaani mwaka2016 kilimo hicho kilishuka na ukuaji wake kufikia asilimia 1.7 hali inayozidisha umasikini kwa Watanzania,” alisema Dk Nagu. Alisema pamoja na ukuaji wa kilimo pia bajeti ya Wizara ya Kilimo imekuwa ilishuka badala ya kupanda kila mwaka kwani mwaka 2011 bajeti ya Wizara hiyo ilikuwa asilimia 7.8 ya bajeti nzima ya Serikali, lakini katika bajeti ya mwaka 2016, bajeti ya Wizara hiyo ilishuka na kufikia asilimia 4.9.

Nagu aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika Serikali ya Awamu ya Nne, kupongeza hatua ya Serikali kuondoa utitiri wa kodi zenye kero kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, aliitaka Serikali ihakikishe kuwa hatua hiyo inawanufaisha zaidi wakulima, wafugaji na wavuvi na si kwa wafanyabiashara.

Kwa upande wake mbunge wa Malindi, Ally Saleh (CUF) aliishauri serikali iwekeze zaidi kwenye fikra za kuleta mabadiliko ya kilimo, mifugo na uvuvi kutokana na ukweli kuwa Tanzania imebarikiwa rasilimali kama vile maziwa, mito, bahari na mikoa yenye rutuba ambayo endapo itatumiwa vema itakuza sekta hizo.
“Sasa hivi tuna tatizo gani, badala ya kilimo kwenda mbele kinashuka. Leo hii haiwezekani sisi tunaongoza kwa kuwa na ng’ombe wengi kuliko Kenya, lakini wao wanatuzidi kwa kuzalisha maziwa. Tunahitaji fikra mpya,” alisema. Alisema Tanzania kuna hekta takribani milioni 13.5 zinazolimika na hekta milioni 1.5 za mikoko, pia ni nchi ya tatu Afrika lakini pia nchi ya 11 duniani kwa kuwa na wingi wa mifugo, lakini bado rasilimali hizo haijatumiwa vizuri.

Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema), aliishauri Serikali iwekeze zaidi katika kilimo kupitia mbolea ya uhakika, dawa za mimea, masoko na miundombinu bora kwa kuwa huo ndio usalama wa watanzania katika chakula.


Chanzo: Habari Leo

RAIS MAGUFULI AMETUMA SALAMU ZA POLE KWA WAFIWA WA AJALI ARUSHA

Tokeo la picha la magufuli
Hii hapa chini ni taarifa kama ilivyoandikwa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu:
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko mkubwa taarifa ya vifo vya wanafunzi 32 wa darasa la saba, walimu 2 na dereva wa gari la shule ya msingi iitwayo Lucky Vicent ya Arusha vilivyotokea leo saa 3 asubuhi baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali katika eneo la Rhotia Marera, Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.
Wanafunzi na walimu hao walikuwa wakitoka shuleni kwao kwenda shule ya msingi iitwayo Tumaini kwa ajili ya kufanya mtihani wa ujirani mwema na walipofika katika eneo la Rhotia Marera basi walilopanda liliacha njia na kisha kutumbukia korongoni ambako limesababisha vifo hivyo na majeruhi watatu.
Kufuatia ajali hiyo, Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo na kueleza kuwa ajali hiyo imezima ndoto za watoto waliokuwa wakijiandaa kulitumikia Taifa na imesababisha uchungu, huzuni na masikitiko makubwa kwa familia za marehemu na taifa kwa ujumla.
"Ndugu Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo naomba unifikishie pole nyingi kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wote wa wanafunzi, walimu na dereva waliopoteza maisha, hiki ni kipindi kigumu kwetu sote, na uwaambie naungana nao katika majonzi na maombi.
"Muhimu kwa sasa tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali pema, majeruhi wapone haraka na wote walioguswa na msiba huu wawe na moyo wa subira, ustahimilivu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu" Amesema Rais Magufuli.

SERIKALI IMEPELEKA TSH. BILIONI 177 KWENYE HALMASHAURI ZA WILAYA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imepeleka katika halmashauri nchini Sh bilioni 177 Oktoba mwaka huu kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Aidha, amempongeza Rais John Magufuli, kwa kufikisha siku 365 za kuwapo madarakani na mafanikio makubwa ya utawala wake tangu alipopewa na Watanzania ridhaa ya kuwa Rais wa Tano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.

Licha ya pongezi zake, amewaomba Watanzania waendelee kumuunga mkono Rais Magufuli ili afanikishe zaidi dhamira yake njema ya kuwatumikia wananchi. Majaliwa aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma ambapo alizungumzia mambo mbalimbali katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu.

Akizungumzia suala la fedha kupelekwa katika halmashauri, alisema serikali imechukua muda kupeleka fedha mara baada ya bajeti kupitishwa na Bunge kwa kuwa ilitaka kufanya mambo muhimu ya kujiridhisha.

Aliyaja maeneo muhimu ambayo serikali ilitaka kuyafanyia kazi kabla ya kupeleka fedha kuwa ni kujiridhisha kuwepo kwa takwimu muhimu za mapato na matumizi na kupeleka watumishi watakaosimamia shughuli za ukusanyaji wa mapato na matumizi katika halmashauri zote nchini.

Alisema pia serikali ilitaka kuratibu na kutathmini miradi yote iliyokuwa imeanza na haikuwa imeendelezwa kabla ya kuanza miradi mipya ili kutambua thamani zake.

“Baada ya kuwa tumejiridhisha, sasa tumeanza kupeleka fedha kwenye halmashauri zote nchini na kwa mujibu wa kumbukumbu zangu kutoka Hazina wakati napewa taarifa ofisini kwangu, kufikia Oktoba tumeshapeleka zaidi ya Sh bilioni 177,” alisema Majaliwa.

Alisema fedha hizo ni za miradi ya maendeleo kwenye halmashauri zetu nchini na alisema kudhihirisha hilo, aliwaambia wabunge ni shahidi wameanza kuona katika wiki tatu kwenye magazeti kumekuwa na matangazo ya zabuni. Alisema hali hiyo inadhihirisha kuwa miradi iliyokuwepo na inayoendelea imeshaanza kutengewa fedha na kuanza kutekelezwa.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Abdallah (CCM), alimuuliza Majaliwa katika maswali ya papo kwa hapo, kwamba serikali ina mpango gani wa kupeleka fedha katika halmashauri kutekeleza miradi.

Mbunge huyo alisema miradi mingi imesimama na akitolea mfano wa mkoa wa Tabora anakotoka, akisema halmashauri zote saba hazijapata fedha hizo na kwa nini katika robo ya mwaka wa utekelezaji wa bajeti fedha hazijapelekwa.

“Kabla ya kujibu Mheshimiwa Naibu Spika uridhie niwakumbushe Watanzania kuwa Rais John Magufuli amefikisha siku 365 kwa mafanikio makubwa, tumuombee aendelee vizuri, kila mmoja kwa dhehebu lake amuombee nchi ipate mafanikio makubwa,” alisema Majaliwa kabla ya kujibu swali hilo.

Baada ya kumpongeza Rais Magufuli ambaye aliapishwa Novemba 5 mwaka jana kuwa Rais wa Tanzania baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huo, alijibu swali la Abdallah alisema ni kweli baada ya bajeti serikali inapaswa kupeleka fedha katika halmashauri.

Alisema baada ya tathmini tayari fedha zimeanza kupelekwa katika halmashauri hizo. Akijibu swali la Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) kuhusu mgawanyo wa fedha za Mfuko wa Bunge kuchelewa kufika na kueleza kuwa ni dalili za serikali kufilisika.

Waziri Mkuu alisema serikali haijafilisika na katika kipindi cha mwaka bado kuna miezi saba ya kuzipeleka fedha hizo zinazopelekwa mara moja kwa mwaka.

Aidha, akijibu swali la nyongeza la Waitara kwamba Segerea inapata fedha nyingi (Sh milioni 33) ingawa ina watu wachache wakati Ukonga inapata Sh milioni 16 pekee, Majaliwa alisema atalishughulikia kwa kuwa jimbo lenye watu wengi linapaswa kupewa fedha nyingi.



Chanzo: Habari Leo

RAIS MAGUFULI AAHIDI KUENDELEA KUTOA MIKOPO 2016/2017 KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU NA KUTOA RAI SUALA HILO KUSHUGHULIKIWA

Tokeo la picha la magufuli udsm leo oktoba 21

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo kwa nafsi yake ametoa matumaini kwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali nchini kuhusu hatima yao ya mkopo wa Elimu ya Juu alipokuwa akihudhuria sherehe ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Rais Magufuli amebainisha haya, namnukuu;

"Tunapopitia katika challenge hii muivumilie serikali kutengeneza utaratibu ulio mzuri, ninafahamu, katika bajeti ya mwaka 2015/2016, fedha iliyotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi kwa sababu Mh. Waziri umezungumza hapa zilikuwa bilioni 340 ambazo  zilikjuwa zinatosha karibu wanafunzi tisini elfu (90,000)  baada ya serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani  ili kutimiza yale tuliyokuwa tumeahidi tuliongeza fedha hizo za mkopo hadi kfikia bilioni 473 bajeti ilikuwa ya bilioni 340 tukaongeza zikafika bilioni 473 kutokana na makusanyo na tukaweza kutoa mikopo kwa wanafunzi 124,358 mwaka huu ameeleza ni zaidi ya bilioni 483 zimepitishwa katika bajeti  kwa hiyo wanafunzi wengi zaidi watapata mkopo ninafahamu kwa mfano wanafunzi wanaoendelea ambao wako karibu 93,000 wote wamekuwa accommodated kwenye mkopo pamoja na wanafunzi wapya ambao nafikiri ni zaidi ya 25,000 lakini ni lazima kweli nikiri hapakuwepo na coordination palitakiwa kwanza vyuo vyote vya elinu ya juu viwe na tarehe moja ya kufungua kwa sababu wapo wengine walifungua mwezi mzima uliopita wako wengine wamefungua jana wako wengine watafungua keshokutwa ukishafungua haraka haraka wanafunzi wakakaa pale kwa mwezi mmoja halafu unawambia kufanya registration lazima walipe wakati Bodi ya Mikopo haijatoa orodha ya majina ya vijana ambao watakaokopeshwa ni contradiction.

Palikuwa pawepo na communication kati ya Bodi ya Mikopo sijui ni TCUsijui ni nani, Wizara ya Elimu na Wizara ya Fedha kwamba katika orodha ya wanafunzi watakaopata mikopo ni hawa hapa majina yao ni haya hapa mnapeleka majina hayo na orodha, amount ya fedha zinazotakiwa Wizara ya Fedha, Wizara ya Fedha nao wanaprocess zao fedha hizi tunazitoa baadaye zikishapelekwa kwenye benki kwenye hizo akaunti za wanafunzi, mngeweza mkafungua vyuo hapakuwa na sababu ya kufungua mwezi mzima kabla wanafunzi wanakaa pale hajui kama atapata mkopo au hatapata mkopo halafu unamwambia hakuna registration  kwa sababu hujapata mkopo inaleta usumbufu wa ajabu, na hilo.

Nitoe wito kwa Wizara ya Elimu na hili nasema kwa dhati lengo la serikali si kuleta usumbufu kwa wanfunzi  lakini ni ukweli pia kwamba haitatoa mikopo kwa wanafunzi ambao wenye uwezo unamkuta mtoto wa Profesa Rwekaza na wewe upate mkopo mtoto wa Ndalichako naye apate mkopo mtoto wa Katibu Mkuu Kijazi naye apate mkopo haiwezekani mkopo huu umelenga kwa ajili ya kutoa watoto masikini lakini nafahamu na ninasikia hata katika Bodi ya Mikopo kule kuna upendeleo upendeleo wa aina fulani katika kutoa mkopo hata ambao hawastahili wanapewa mikopo na ambao hawastahili wananyimwa mkopo sasa hili Waziri na Bodi zinazohusika mulisimamie sitaki siku moja nije huko kwenye Bodi ya mikopo nichukue orodha ya wanafunzi wote niangalie shule walizosoma na particulars walizozijaza halafu nije nipewe majina ya watu ambao hawakustahili kupewa mkopo wanafunzi 25 wa mwaka huu siwezi kushindwa kusoma kwa siku 1 ntapekua page by page 25,000 ukigawa kwa masaa 12 ambayo naweza nikajifungia kila jina naweza nikalisoma kwa sekunde ngapi ninajua naweza, sasa tusifikie huko.

Ninashukuru Waziri baada ya kuona hii changamoto ukawa umelileta hili suala haraka haraka na tukatoa instruction Wizara ya Fedha watoe bilioni 80 za mwanzo haraka haraka na nimeambiwa zimeshatolewa, sasa niwaombe wanafunzi msiwe na haraka haraka kwa sababu katika changamoto hizi ambazo zinapita ndani ya serikali wanafunzi hewa, mikopo hewa, mishahara hewa hatutaki hela yetu ipotee ovyo pameshatokea changamoto na najua haitatokea tena vyuo vikuu vitakuwa vinafunguliwa siku ambapo wana uhakika na fedha zitakuwa zimeshapelekwa kwenye wanafunzi.

Lakini pia pamekuwa na utitiri mwingi mno wa vyuo vikuu unakuta shule ilikuwa inaitwa sekondari leo ukisoma kwenye orodha nayo inaitwa Chuo Kikuu na saa nyingine inafikia wanafunzi unaanza kuwagombania, Chuo Kikuu kwa mfano cha Dodoma kina capacity ya kuweka wanafunzi mpaka 45,000 waliopo ni 30,000 lakini unakuta kinafunguliwa chuo kingine Bagamoyo kina wanafunzi 20 mabweni hayapo maabara hayapo natoa mfano tu labda nimesema Bagamoyo kingine kinafunguliwa Chato.

Sasa ninachotaka kutoa wito kwa Bodi, TCU, Wizara hebu mpitie vizuri hivi vyuo mnatoa vibali mnatoa vibali mno vya kuanzisha chuo kikuu kila mahali wakati vyuo vilivyopo havijajaa watu na mnawachanganya saa nyingine hawa watoto kwa sababu mnakuwa mnawagombania, na vyuo vikuu vingine havina walimu unakuta mwalimu leo yuko  Dar es Salaam kesho yuko Mbeya keshokutwa yuko Iringa keshokutwa Moshi ataconcentrate namna gani kufundisha kwa hiyo matatizo haya mengine yameletelezwa na nyinyi mnnaopendwa kuitwa maVice Chancellors wenye vyuo vilivyopo sijasema wewe (akimaanisha Prof. Rwekaza, VC wa UDSM) kwa hiyo nikuombe Waziri simamia hili, kwanu kuna ubaya gani tukiwa hata na vyuo vikuu vinne tu kila chuo kina watu milioni moja moja watu wako palepale wanalipwa mshahara mzuri na wanaconcentrate vizuri."


KWA MSAADA KUTOKA KWA MWANAFUNZI ALIYEFATILIA SPEECH HII CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM NA KUSAMBAZA KWA WATANZANIA.

WALIOKUFA KATIKA TETEMEKO WAFIKIA 16

Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kuaga miili ya waliokufa katika tetemeko la ardhi mkoani Kagera.


Maafa zaidi yameripotiwa katika janga la tetemeko la ardhi, lililotokea juzi mkoani Kagera, ambapo imeripotiwa idadi ya vifo kuongezeka na kufikia watu 16, huku wengine 253 wakijeruhiwa na kusababisha simanzi na masikitiko kwa familia nyingi. Katika tukio hilo, pia nyumba 840 za makazi zimeanguka, nyumba 1,264 zimepata nyufa kubwa na majengo 44 ya taasisi mbalimbali zikiwemo shule yameanguka.

Tukio hilo limemfanya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kulazimika kufanya ziara ya ghafla ya kuwatembelea waathirika wa tetemeko hilo, ambalo limedaiwa kusababisha tafrani pia katika nchi jirani za ukanda wa Afrika Mashariki za Kenya na Rwanda.

Katika hatua nyingine, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela kilichopo eneo la Tengeru, mkoani Arusha kimeeleza mpango wa kuanza kufunga vifaa vitakavyotoa ishara ya matukio ya matetemeko ya ardhi kabla majanga hayo kutokea.

Katika mradi huo maalumu chini ya Kitengo cha Utafiti wa Miamba na Volcano, chuo hicho kitashirikiana na taasisi mbalimbali za elimu ya juu zilizopo Ulaya na Marekani, hasa Chuo Kikuu cha Glasgow kilichopo Scotland, kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Burton Mwamila. Ziara ya Waziri Mkuu

Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu jana katika Uwanja wa Kaitaba ulioko mjini Bukoba ambapo umeandaliwa maalumu kwa ajili ya kuaga miili ya watu waliopoteza maisha katika tukio hilo la kusikitisha, Mkuu wa Mkoa, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu alisema tukio hilo ni la kwanza kutokea mkoani humo na kwamba limeleta madhara makubwa kwa wananchi na kuacha majonzi makubwa.

Kijuu alisema mpaka taarifa inaandaliwa watu 16 waliripotiwa kupoteza maisha na kusababisha majeruhi 253, huku 170 wakiwa wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo na 83 wakitibiwa na kuruhusiwa.

Alisema pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 840 za makazi kuanguka, nyumba 1,264 kupata nyufa kubwa na majengo 44 ya taasisi mbalimbali zikiwemo shule kuanguka.

Alisema tetemeko hilo lenye ukubwa wa alama 5.7 uliopimwa kwa kipimo cha Ritcher cha kisayansi cha kupima matetemeko, limeleta madhara makubwa ambapo Serikali ya Mkoa inaendelea kutathmini kwa kina athari zaidi zilizosababishwa na tetemeko hilo na pia uharibifu uliojitokeza kisha kupeleka katika Ofisi ya Waziri Mkuu waone jinsi ya kusaidia.

Alisema hatua zilizochukuliwa na mkoa mpaka sasa ni kuwaokoa na kuwapeleka watu hospitali kwa ajili ya matibabu na kuwapatia makazi ya muda baadhi ya wananchi wenye nyumba zilizoathirika, wakati mipango mingine ikiandaliwa.

Taarifa hiyo ya Mkuu wa Mkoa, ilimfanya Waziri Mkuu kueleza masikitiko yake na serikali kutokana na janga hilo na kutoa salamu za pole kwa wananchi waliopatwa na madhara na kuwatembelea wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa na pia maeneo yote yaliyoathirika.

"Leo si siku nzuri kwetu, nimekuja kumwakilisha Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye anawapa pole sana wana Kagera wote na Watanzania kwa ujumla. Pia Makamu wa Rais anawapa pole kwa msiba huu mkubwa, lengo la safari yangu ni kuja kuwapa pole, tukio hili ni kubwa na halijawahi kutokea Tanzania, tumekuwa tukisikia kutoka mataifa ya nje lakini leo limetupata nchini kwetu," alisema Majaliwa.

Aliwasihi na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu, kuonesha umoja na ushirikiano, lakini pia kujitokeza kuwafariji wenzao wakati wote wa majonzi, huku akisema Watanzania kwa miaka mingi wamekuwa wakishuhudia mitikisiko midogo, lakini juzi tumeshuhudia mtikisiko mkubwa kabisa ambao umeleta madhara makubwa kwetu.

"Mpaka sasa hatuna uhakika mtikisiko huu utakuwa endelevu kwa kiasi gani, nataka niwahakikishie Watanzania wote, Serikali tunafanya mawasiliano na taasisi zenye uwezo wa kubaini mtikisiko huu ili tuweze kujua jambo hili litakuwa endelevu kwa kiasi gani na kuona dalili na ukubwa wake utakuwaje ili tujipange katika kutoa elimu lakini pia tahadhari pindi jambo kama hili linapoweza kutokea au tunapoona viashiria au dalili za jambo hili," alisema Waziri Mkuu.

Alisema kuwa Mkuu wa Mkoa katika taarifa yake alimweleza kwamba tathmini inaendelea na kwamba ameiagiza Kamati ya Maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kufika mkoani Kagera mara moja na kuzunguka mkoa mzima kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa kwa lengo la kufanya tathmini ya jumla.

Alisema baada ya tathmini hiyo, utaratibu utafuatwa kwani serikali haiwezi kuwatupa mkono wananchi hao, pia alitumia fursa hiyo kuwaambia wafiwa kuwa Watanzania nchini kote wako pamoja nao katika janga hilo.

Akielezea mkasa huo, majeruhi Happines Apolinary ambaye ni mkazi wa kata ya Buyekera aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera kwa kuumia kichwani na mgongoni, alisema alishtuka kusikia mtikisiko mkubwa wakati akiwa ndani ya nyumba yake na ghafla aliangukiwa na kuta na kumsababishia majeraha. Pamoja na kueleza kuumia vibaya kutokana na tukio hilo, Happines aliwashukuru wafanyakazi wa Hospitali ya Mkoa wa Kagera kwa huduma nzuri waliyompatia tangu juzi alipofikishwa hospitalini hapo.

Majeruhi mwingine, Paulina Spilian aliyelazwa hospitalini hapo akiwa amejeruhiwa miguu alisema akiwa ndani ya nyumba yake ghafla alisikia mtikisiko mkubwa ulioambatana na kishindo cha kuanguka kwa kuta za nyumba na akiwa katika harakati za kutaka kukimbia nje aliangukiwa na ukuta miguuni.

Majeruhi huyo aliiomba Serikali kuwasaidia kwa kuwajengea nyumba na pia kuwapa elimu kuhusiana na matukio kama hayo ili waweze kujiokoa baada ya kuona dalili au viashiria tofauti na ilivyotokea juzi.

Advela Respicius ambaye ni mama wa marehemu, Verdiana Respicius aliyekufa baada ya kufunikwa na kifusi cha nyumba, akizungumza kwa niaba ya familia za wafiwa wa tukio hilo, alitoa shukrani kwa serikali kwa kutoa majeneza, sanda na usafiri wa kuwapeleka marehemu hao mpaka vijijini kwa ajili ya maziko.

Vifaa vya kutabiri kufungwa Wakati hofu ikiwa bado imetawala kutokana na tukio hilo hasa kutokana na wananchi wa Kagera kueleza kutofahamu lolote kabla ya kutokea kwa tetemeko kutokana na kutopewa taarifa zozote na mamlaka za serikali, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela kilichopo eneo la Tengeru, mkoani Arusha kimesema kinatarajia kuanza kufunga vifaa vitakavyotoa ishara ya matukio ya matetemeko ya ardhi kabla majanga hayo kutokea.

Katika mradi huo maalumu chini ya Kitengo cha Utafiti wa Miamba na Volcano, chuo hicho kitashirikiana na taasisi mbalimbali za elimu ya juu zilizopo Ulaya na Marekani, lakini hasa Chuo Kikuu cha Glasgow kilichopo Scotland, kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Burton Mwamila.

Katika mradi huo wa kwanza nchini unaolenga kutoa utabiri wa matukio ya matetemeko na ulipukaji wa volcano nchini, vifaa maalumu vitakavyokuwa vinapima uwezekano wa kutokea majanga hayo, vitafungwa katika maeneo nyeti kama milima, vilima na sehemu ambazo huwa na volcano hai.

Mtaalamu wa miamba ambaye pia ni Mkuu wa Taasisi ya 'Eco Science' inayoshughulika na utafiti wa miamba pamoja na milipuko ya volcano, Dk Ben Beeckmans amefafanua kuwa 'Mlima wa Mungu' (Oldonyo Lengai) uliopo eneo la Ngaresero, wilayani Ngorongoro ndio chanzo kikubwa cha matetemeko ya ardhi katika eneo lote la Afrika Mashariki. Mlima huo wenye volkano hai pia umekuwa ukilipuka mara kwa mara na tukio la mwisho lilirekodiwa mwaka 2007.

Vifaa hivyo vya kutabiri matetemeko ya ardhi vitafungwa kuzunguka eneo la mlima huo, Ziwa Natron, Mlima Meru na hata Mlima Kilimanjaro pamoja na maeneo mengine nchini.

Lakini hatua hiyo si kwamba imetokana na matukio ya tetemeko yaliyoyakumba maeneo mengi ya nchi juzi bali ni mpango uliobuniwa na wataalamu mapema mwaka huu na kwamba kilichobaki ni utekelezaji tu.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Karimu Meshaki alisema atatoa taarifa rasmi kuhusu maendeleo ya mpango huo wiki hii.

Hivi karibuni Serikali ilijenga maabara kubwa kabisa ya utafiti wa kisayansi katika Chuo cha Nelson Mandela, Arusha ambayo ilizinduliwa miezi miwili iliyopita.

Serikali ya India pia ilitoa mchango wake kwa kukipatia chuo hicho kompyuta kubwa na yenye uwezo mkubwa zaidi nchini ijulikanayo kama 'Param Kilimanjaro,' ambayo pamoja na shughuli nyingine pia inatarajiwa kutumika katika tafiti za miamba, gesi asilia na pia kwenye huu mradi mpya wa kufuatilia matukio ya tetemeko la ardhi na milipuko ya volkano.



Chanzo: Habarileo

TETEMEKO LA ARDHI LIMEPITA MIKOA YA MWANZA NA KAGERA NA KUFANYA UHARIBIFU

Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 5.7 limetikisa mkoa wa Mwanza likitokea mkoa wa Kagera umbali wa kilomita 44 karibu na ukingo wa magharibi wa Ziwa Victoria huku likijirudia kwa ukubwa zaidi ya ule wa awali. Tetemeko hilo lilipita umbali wa kilomita 10 kwenda chini limefanya uharibifu mkoani Kagera kama picha zinavyoonesha hapa chini. Pia kumeripotiwa vifo vya watu.












PICHA KWA HISANI YA JAMII FORUMS.

CHADEMA 'YAIBIPU' POLISI






Ni wazi sasa kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeamua kujipima nguvu na Jeshi la Polisi baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kutangaza kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima kuanzia Septemba mosi, mwaka huu.

Kamati Kuu hiyo katika maazimio yake yaliyosomwa kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, ilisisitiza kuwa azma yake hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kupinga agizo la jeshi hilo la kuzuia kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Sababu nyingine zilizoisukuma Kamati Kuu kufikia azma hiyo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe ni pamoja na kupinga zuio la urushwaji wa moja kwa moja wa mijadala ya Bunge, kupinga wabunge wa upinzani kudhibitiwa bungeni, kuingiliwa kwa mhimili wa mahakama, upuuzwaji wa utawala wa sheria na haki ya kupata habari.

Katika hatua nyingine, Kamati Kuu ya Chadema imezindua operesheni Ukuta yenye lengo la kupambana na kile ilichokiita kuwa ni udikteta nchini, huku ikitangaza kushirikiana na wale tu watakaoona umuhimu wa kuwepo kwa haki na demokrasia nchini.

Mbowe aliyeambatana na viongozi mbalimbali wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, aliagiza maagizo hayo kupewa umuhimu na ngazi zote za chama hicho kuanzia vijiji, kata, majimbo, wilaya, mikoa, kanda, mabaraza hadi taifa.

Alisema Jeshi la Polisi nchini limeamua kuvidhibiti vyama vya siasa ili visiweze kufanya mikutano ya kisiasa, wakati serikali inaongozwa na viongozi ambao ni wanasiasa na ambao wamekuwa wakifanya kazi zao za kisiasa kupitia nafasi zao za kiserikali.

Mwenyekiti huyo wa Chadema Taifa alisema katika maandalizi ya mikutano hiyo, chama hicho kitafuata taratibu, kanuni na sheria zinazostahili ili waweze kupata ruhusa huku akisisitiza kwamba si nia ya chama hicho kuanzisha vurugu, bali kutumia haki ya msingi ya kukosoa akisema ndiyo njia sahihi ya kufuatwa katika ukuzaji wa haki na demokrasia nchini.

Alisema Kamati Kuu imeagiza ngazi zote za chama kuanzia ngazi ya msingi, kata, majimbo, wilaya, mikoa, kanda, mabaraza na Taifa kukaa vikao vyake vya kikatiba haraka na ajenda za vikao hivyo iwe ni kujadili maandalizi ya mikutano hiyo ya hadhara, kujadili hali ya siasa na pia hali ya uchumi nchini.

Alisema Kamati Kuu imewataka wanasheria wa chama hicho wakiongozwa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kukaa na kuyatazama mambo yote ambayo yametokea na kuchukua hatua za kisheria kwa lengo la kuyatafutia suluhisho la kisheria.

“Inaonekana kwamba wao ndio wana haki lakini sio sisi. Viongozi wetu wakubali kukosolewa na waamini kuwa taifa ni letu sote, hali ya sasa imesababisha Taifa kuwa lenye uoga wa kupindukia,” alisema na kuongeza kuwa Septemba mosi ni siku ya kukata misingi ya uonevu wa demokrasia.

Kuhusu ni nini kitazungumzwa na viongozi wa chama hicho katika mikutano hiyo ya hadhara Mbowe alisema kwa kifupi; “Lazima tufanye mikutano ya hadhara. Tutaelezana namna ya kukatiza mto pindi tutakapoufikia.

” Kuhusu operesheni Ukuta, Mbowe alisema jana ni siku ya kwanza ya utekelezaji wa operesheni hiyo yenye maana ya ‘Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania’ huku akisisitiza kuwa inatokana na chama hicho kutokuwa tayari kuruhusu nchi kuongozwa nje ya misingi ya demokrasia.

Alisema kupitia operesheni hiyo chama hicho kitashirikiana na wale wote ambao wanaona umuhimu wa kuzingatiwa kwa misingi ya haki na demokrasia, na kuongeza kuwa hiyo haina maana kwamba chama hicho hakiungi mkono hatua za serikali katika kupambana na matendo maovu nchini.

Kauli yapingana na agizo la Polisi

Msimamo huo wa Chadema ni wazi kwamba sasa utakifanya chama hicho kukabiliana na Jeshi la Polisi ambalo limezuia kufanyika kwa mikutano ya hadhara kwa vyama vyote vya kisiasa nchini.

Agizo hilo la Jeshi la Polisi lilitolewa na Kamishina wa Polisi Operesheni na Mafunzo kutoka Makao Makuu ya jeshi hilo, Nsato Mssanzya. “Katika siku za hivi karibuni, Jeshi la Polisi nchini, limepokea taarifa kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa wakitaka kufanya mikutano na maandamano.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi kupitia vyanzo vyake mbalimbali vya habari limebaini kuwa mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi.

“Aidha vyama vingine vya siasa vimeonesha dhamira ya kupinga kile ambacho kitasemwa na wapinzani wao. Vyanzo hivyo vya habari vimebainisha kwamba upo uwezekano mkubwa wa kutokea vurugu baina ya makundi mawili ya kisiasa.

“Kwa hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini linapiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara kuanzia Juni 7, mwaka huu hadi hapo hali ya usalama itakapotengemaa. Jeshi la Polisi linawataka wanasiasa kuacha mara moja kuwashinikiza wananchi kutotii sheria za nchi. “Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua kali za kisheria mtu yeyote au chama chochote cha siasa kitakachokaidi agizo hili.

Aidha Jeshi la Polisi linawataka wananchi kuwa makini na wanasiasa wenye lengo la kutaka kuvuruga amani ya nchi hii na badala yake linawasihi waendelee kushirikiana katika kujenga umoja wa nchi hii,” alisema Kamishna Mssanzya katika agizo hilo la Jeshi la Polisi.

Katika tukio jingine, Mwandishi Wetu John Mhala kutoka Arusha anaripoti kwamba wabunge wawili na wenyeviti wawili wa Chadema wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa kufanya mkutano wa hadhara katika Wilaya ya Karatu bila ya kibali.

Waliokamatwa na polisi ni pamoja na Mbunge wa Karatu, Willey Kaboroo (58) na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha kupitia chama hicho, Cecilia Pareso (35).

Wengine waliokamatwa na kuhojiwa na polisi Arusha kwa zaidi ya saa tatu ni pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Jubilet Mnyenye (55) na Makamu wake Lazoro Kajuta ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ganako.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Yusuph Ilembo alisema kuwa viongozi hao walifanya mkutano wa hadhara Julai 23, mwaka huu, bila kufuata tararibu kama inavyotakiwa.

Kamanda Ilembo alisema wabunge hao na wenyeviti hao wa halmashauri waliamua kukiuka taratibu za kufanya mkutano wa hadhara hivyo polisi iliamua kuwaita na kuwahoji sababu za kushindwa kufuata tararibu.

Alisema wamefunguliwa jalada la uchunguzi na wote wamehojiwa na kuachiwa kwa dhamana yao wenyewe na upelelezi wa shauri hilo unaendelea.

Hata hivyo, wabunge hao na wenyeviti baada ya kuhojiwa walisema kuwa wamesikitishwa na hatua ya kuitwa polisi na kuhojiwa kwa kufanya mikutano ya hadhara wakati Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu alikuwa anajua kila kitu.



Chanzo: Habari Leo

BARAZA LA MITIHANI LIMETANGAZA MATOKEO YA KIDATO CHA SITA 2016

Matokeo ya Kidato cha Sita 2016 yametoka, unaweza kuyaona kwa kubofya HAPA

UJENZI WA BOMBA LA MAFUTA TANZANIA NA UGANDA SASA NI RASMI

BOMBA la mafuta ghafi kutoka Hoima katika Ziwa Albert nchini Uganda, sasa ni rasmi kwamba litapita katika ardhi ya Tanzania kwenda Bandari ya Tanga, ambako ndiko meli kubwa za mafuta, zitakapotia nanga kubeba mafuta hayo kwenda sehemu mbalimbali duniani. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, imeeleza kuwa Serikali ya Uganda imetangaza rasmi uamuzi wake wa kutumia bandari hiyo. Kwa hatua hiyo, bomba hilo linalotakiwa kuwa limekamilika ifikapo 2018, litaingilia Mkoa wa Kagera kutoka nchini Uganda na kupita katika mikoa ya Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma hadi Bandari ya Tanga. Rais Museveni Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, ndiye aliyetangaza uamuzi huo wakati wa mkutano wa 13 wa Ushoroba wa Kaskazini uliomalizika jijini Kampala jana. “Ujumbe wa Tanzania uliokamilisha mazungumzo hayo na kushuhudia utangazwaji wa hatua hiyo, uliongozwa na Dk Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,” imeeleza taarifa hiyo. Mbali na kiongozi huyo, taarifa hiyo imeeleza kuwa jopo la wataalamu lililoshiriki katika mazungumzo hayo, liliongozwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambalo litaendelea kubakia Kampala kukamilisha mpango huo wa bomba la mafuta ghafi, ambalo litanufaisha pia nchi zingine za Afrika Mashariki na Kati. Mchakato ulivyokuwa Awali, serikali za Uganda na Kenya, ziliwahi kufikiria kupitisha bomba hilo katika ardhi ya Kenya, kwa nia ya kutumia bandari itakayojengwa ya Lamu nchini humo. Hata hivyo, wakati hatua za kina hazijachukuliwa, Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli na Rais Museveni walikutana mwanzoni mwa mwezi uliopita na baada ya mazungumzo yao, wakatoa agizo kuwa mchakato wa ujenzi wa bomba hilo, ufanyike kwa kasi. Baada ya kikao cha marais hao kutoa agizo hilo, kilifuata kikao cha Rais Magufuli na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total, tawi la Afrika Mashariki, Javier Rielo, ambapo kiongozi huyo wa kampuni alimhakikishia Rais Magufuli kuwa kampuni yao itaanza ujenzi wa bomba hilo haraka iwezekanavyo, kwa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zipo. Katika mazungumzo hayo, Rielo alimueleza Rais Magufuli kuwa kampuni yake inatarajia kutumia Dola za Marekani bilioni 4 ambazo tayari zimeshaandaliwa. Bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,410 na litasafirisha mafuta ghafi mapipa 200,000 kwa siku kutoka Ziwa Albert nchini Uganda, hadi Bandari ya Tanga na ujenzi wake unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000. Makubaliano ya awali Katika utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli na Rais Museveni, Machi 17 mwaka huu, serikali za Tanzania na Uganda pamoja na kampuni ya Total E&P Uganda na Shirika la Maendeleo ya Petroli la Tanzania (TPDC), walitia saini mpango wa pamoja wa utekelezaji wa mradi huo. Mpango huo ulitiwa saini na Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Muhongo; Waziri wa Maendeleo ya Nishati na Madini wa Uganda, Irene Muloni; Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio na Meneja Mkuu wa Total E&P Uganda, Adewale Fayemi. Kwa nini Tanzania Baada ya utekelezaji wa agizo hilo kufikia hatua ya mkataba kuliibuka mjadala kuhusu uhakika wa bomba hilo kupita Tanzania baada ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kukutana na Rais Museveni, kujaribu kuangalia uwezekano wa bomba hilo kupitia Kenya kwenda Lamu. Pamoja na jitihada hizo, Bandari ya Tanga, ilibakia kuwa eneo pekee lenye mazingira bora, nafuu na yenye ufanisi kwa utekelezaji wa mradi huo. Uzoefu Mbali na Bandari ya Tanga kuwa ya kimkakati zaidi katika utekelezaji wa mradi huo, taarifa za ndani za wataalamu wa mafuta, zilionesha kuwa pia Tanzania ndiyo yenye uzoefu wa muda mrefu na wa hivi karibuni wa ujenzi, uendeshaji, ulinzi na uelimishaji jamii katika miradi ya bomba la mafuta. Uzoefu wa muda huo mrefu unatajwa kuwa ni wa ujenzi, uendeshaji na uhudumiaji wa Bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (Tazamaaaaaa tangu mwaka 1968, likitoka Dar es Salaam mpaka Ndola Zambia. Bomba hilo lenye kipenyo cha nchi 8 mpaka 12 na urefu wa kilometa 1,710; kati ya hizo kilometa 860 zipo kwenye ardhi ya Tanzania na limekuwa likipitisha mafuta tani milioni 1.1 kwa mwaka. Tanzania pia ina sifa ya uzoefu wa ujenzi, uendeshaji na uhudumiaji wa bomba la gesi kutoka Songo Songo mpaka Dar es Salaam, lenye kipenyo cha nchi 12 na urefu wa kilometa 25 kutoka kisiwa cha Songo Songo mpaka Somangafungu. Pia kuna bomba lingine la urefu wa kilometa 207 na kipenyo cha nchi 16, kutoka Somangafungu mpaka Ubungo Dar es Salaam, mbali na bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara mpaka Kinyerezi Dar es Salaam lenye zaidi ya kilometa 490. Lipo pia bomba la gesi linalotoka Mnazi Bay kwenda Mtwara, urefu wa kilometa 27 na kipenyo cha nchi 8, ambalo limeanza kutumika tangu 2006. Uzoefu wa kazi Katika ujenzi na uendeshaji wa mabomba hayo kwa miaka mingi, Tanzania imejijengea uzoefu wa kazi ya kupata ardhi kwa ajili ya kupitisha miundombinu ya bomba, tofauti na ugumu uliopo kwa nchi shindani ya Kenya na kusimamia masuala ya kimazingira. Tanzania pia imefanikiwa katika kusimamia wakandarasi wa kimataifa na matarajio ya umma wakati wa ujenzi na uendeshaji wa miradi hiyo na hata katika ulinzi wa miundombinu hiyo ambao umekuwa ukishirikisha jamii. Utayari Bandari ya Tanga Sifa nyingine iliyochangia Tanzania kukubalika zaidi katika mradi huo kwa kiwango cha kusaini mkataba wa utekelezaji tofauti na Kenya, ni utayari na mazingira wezeshi ya asili ya Bandari ya Tanga. Wakati Kenya wakijadili namna bomba hilo litakavyotumia bandari ambayo haijajengwa ya Lamu, kwa ajili ya kuuza mafuta, Bandari ya Tanga yenyewe iko tayari kwa kazi. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bandari ya Tanga imeshakamilisha Tathimini ya Athari za Kimazingira (EIA) na Upembuzi Yakinifu, wakati njia ya Tanga ya bomba hilo imekwishaainishwa na haitapitia katika hifadhi za taifa wala mapori ya akiba. Bandari ya Tanga inayo fursa ya kutumika zaidi na mradi huo, kwa kuwa haina msongamano wa shughuli za bandari na tayari Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Bandari (TPA), kwa mujibu wa taarifa hiyo, imeshatenga fedha za upanuzi utakaohitajika na eneo. Bandari hiyo pia imeunganishwa kwa reli na barabara za lami, zinazokwenda nchi za jirani na hivyo iko tayari kuanza kutumika kwa ajili ya kuingizia mizigo kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo. Bandari ya Tanga pia ndiyo yenye kingo za asili zinazoruhusu shughuli za upakiaji mafuta kufanyika mwaka mzima bila kusimama, tofauti na bandari zingine ambazo kipindi cha mawimbi makali ya bahari, huwa na wastani wa siku 40 ambazo husababisha shughuli za upakiaji au upakuaji mizigo kusimama. Pia bandari hiyo inatumika na hivyo kuwa tayari kwa matumizi ya haraka kama ilivyo dhamira ya Rais Magufuli na Rais Museveni, na hata ujenzi wa boya la kupakia mafuta unatarajiwa kuchukua mwaka mmoja tu hivyo kukamilika Juni 2017, kabla ya muda uliowekwa na mwekezaji wa kuanza kuuza mafuta wa 2018. Gesi mikoa saba Mbali na fursa hizo za pekee, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk Mataragio, mradi huo unafungua fursa kwa usambazaji wa gesi asilia katika mikoa ya Kaskazini yaani Dodoma, Singida, Shinyanga, Tabora, Geita, Mwanza na Kagera na vile vile nchi za jirani ambazo zitahitaji gesi ya Tanzania. Pamoja na hayo, kutakua na ujenzi wa barabara mpya kiasi cha Kilometa 200 na uboreshaji wa barabara zilizopo kiasi cha Kilometa 150 na madaraja. Aidha utekelezaji wa mradi huo pia utachochea shughuli za utafiti wa mafuta Tanzania, kwani bomba hilo linapita maeneo ambayo yana uwezekana mkubwa wa kuwa na mafuta, hivyo uwapo wa miundombinu unavutia zaidi uwekezaji katika shughuli za utafiti wa mafuta na gesi. Fursa nyingine inayotajwa ni ya matumizi ya reli ambapo takribani mabomba 123,000 yatasafirishwa katika kipindi cha ujenzi huo. Chwnzo: Habari Leo

ZITTO KABWE: RAIS AMELIINGIZIA TAIFA HASARA YA TSH. BILIONI 36

Mbunge wa Kigoma mjini kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amefunguka na kusema kuwa Rais John Pombe Magufuli ameliingizia taifa hasara ya bilioni 36 mpaka sasa toka alipoingia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

 Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa Facebook aliandika kuwa kitendo cha Rais Magufuli kushindwa kuchukua hatua juu ya malipo ya IPTL ambayo yanalipwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kila mwezi yamepelekea sasa hivi kufikia jumla ya bilioni 36. 

 "Tshs bilioni 8 kila mwezi TANESCO bado wanalipa IPTL. Rais haijampendeza kumaliza ufisadi huu. IPTL nadhani ni Jipu la Mgongoni (kwa kutumia maneno ya Hidaya wa Richard Mabala ). Rais, kwa kutochukua kwake hatua, ameshaliingizia taifa hasara ya tshs 36 bilioni toka aingie madarakani" aliandika Zitto Kabwe. 

Wakati Rais John Magufuli anatimiza siku 100 toka kutangazwa kama Rais Zitto Kabwe alitoa tathimini yake na kugusia sakata la Escrow pamoja na kampuni ya IPTL na kusema kuwa pesa ambazo wamelipwa IPTL/PAP kwa siku 100 tu zingeweza kununua CT Scan kwa hospitali zote za mikoa nchini.

 "Mkataba wa IPTL bado unaendelea kunyonya Nchi na Serikali inatazama tshs 8 bilioni zinalipwa Kwa matapeli wa IPTL na PAP kila mwezi. Katika siku 100 tangu Rais Magufuli aingie madarakani, jumla ya tshs 30 bilioni zimeshalipwa Kwa IPTL/PAP ambazo zingeweza kununua CT scan Kwa hospitali zote za mikoa nchini. Fedha hii ni zaidi ya mkopo ambao Serikali imechukua kutoka Benki ya Dunia ili kujenga ' fly over ' ya Ubungo jijini Dar Es Salaam" Alisema Zitto Kabwe.



 Chanzo: East Africa Television

RAIS KIKWETE AELEKEZA NGUVU KATIKA ELIMU YA KIDATO CHA 5 & 6

Rais Jakaya Kikwete akipokea tuzo maalum kutoka kwa Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi, Dk.Shukuru Kawambwa kwa kutambua mchango wake katika kuendeleza na kuboresha elimu nchini wakati wa maadhimisho ya kilele cha wiki ya elimu yaliyofanyika katika uwanja wa michezo wa Jamhuri mjini Dodoma jana. Picha na Ikulu

Rais Jakaya Kikwete jana alitumia kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Elimu kuaga wadau wa sekta hiyo, akisema sasa nguvu zielekezwe katika kujenga majengo kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu ya sekondari.

Rais Kikwete, ambaye alikiri kuwapo udhaifu katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, alisema mafanikio pia ni makubwa kiasi kwamba sasa hakuna wanafunzi wanaokosa nafasi ya kwenda sekondari baada ya kufaulu na hivyo nguvu sasa inatakiwa kuwekwa katika kuongeza miundombinu ya kidato cha tano na sita.

Kikwete alitoa kauli hiyo jana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa alipohutubia maelfu ya wakazi wa Dodoma, wakiwamo wanafunzi wa shule za sekondari na msingi katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Elimu.

Rais alisema katika kipindi cha uongozi wake, amekuwa akitamani kutekeleza yale aliyoyaahidi bila ya kuacha jambo na akaongeza kuwa kuna haja ya kuongeza majengo kwa kidato cha tano na sita pamoja na kukamilisha majengo ya maabara.

Rais Jakaya Kikwete aliwataka wadau wa elimu na sekta binafsi kujenga shule za kidato cha tano na sita ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya elimu ambalo amelifikisha katika hatua nzuri katika kipindi chake cha miaka 10.

Kikwete, ambaye uongozi wake ulianzisha mkakati wa kujenga shule za sekondari za kata, alisema kwa sasa zipo za kutosha kumuwezesha kila mwanafunzi anayemaliza darasa la saba kupata nafasi ya kwenda sekondari kulingana na ubora na kiwango cha ufaulu wake.

“Ukiona mtoto amefeli, basi amefeli kweli na siyo kama zamani tulipokuwa tunasema hakuchaguliwa kwani nafasi zilikuwa chache. Hivi sasa anayefaulu kulingana na vigezo anapata nafasi hayo ni mafanikio makubwa katika elimu,” alisema Rais Kikwete.

Alifafanua kuwa hata bajeti ya elimu kwa miaka yake 10 aliyokuwa madarakani imekuwa ikiongezeka kila mwaka huku mwaka ya mwaka 2014/15 ikiwa kubwa kuliko miaka miaka iliyopita.

Alitoa mfano wa bajeti ya mwaka 2005/2006 wakati anaingia madarakani zilitengwa Sh669.5 bilioni wakati mwaka 2014/2015 zimetengwa Sh3.1 trilioni ili kuhakikisha kunakuwapo na elimu bora inayopatikana katika nyanja zote.

Alifafanua kuwa hata bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu imeongezeka kutoka Sh56.1 bilioni hadi Sh345 bilioni. Kwa sababu hiyo idadi ya wanafunzi wanaofaidika imeongezeka kutoka 16,345 mwaka 2005 hadi 98,000 mwaka 2014.  Huku shule za msingi zikiongezeka kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi 16,343 mwaka 2014.

Pamoja na kusifia mambo mengi ambayo alisema yamefanywa na utawala wake, Rais alikiri kuwa bado kunahitaji kazi ya ziada katika kufanikiwa kielimu kama ilivyo kwa nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tumefanikiwa katika mambo mengi kwenye elimu ingawa bado tunakabiliwa na changamoto. Kazi iliyopo mbele yetu ni kuhakikisha elimu inakuwa bora zaidi na kwa wote,” alisema JK.

“Tumefanya mambo mengi kwa pamoja. Nawaageni bai bai kwani sherehe zijazo mtakuwa na Rais Mwingine, mkitupa nafasi tena haya.”

Alisema mpango wa Tekeleza Matokeo Makubwa Sasa (BRN) aliutoa nchini Malaysia ambako alikuta kuna utaratibu wa kufuatilia masuala ya utekelezaji wa ahadi za Serikali.

“Wenzetu kule waliamua kuwafanyia mitihani walimu wao ili kujua kama kweli walikuwa na uelewa wa kile walichokuwa wanafundisha, walimu wengi walifeli hivyo wakagundua wanachokifundisha nao hawakijui,” alisema.

Kutokana na hilo, alisema kuwa Tanzania nao waliamua kuwapa mtihani walimu kwa baadhi ya masomo na kwamba nao walifeli.

Katika mkutano wa jana, Rais aliwatunuku vyeti na zawadi mbalimbali zikiwamo fedha wanafunzi na shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya kumaliza darasa la saba na kidato cha nne 2014.

Nao Wizara ya Elimu waliamua kumtunuku Rais tuzo mbili ikiwemo ya uongozi bora na Weredi na Tuzo ya BRN, huku Mama Salma Kikwete akitunukiwa tuzo ya kumtunza Rais hadi kufikia kiwango cha kutekeleza majukumu yake ipasavyo ambapo alipewa ng’ombe wawili wa maziwa.



Chanzo: Mwananchi Communication Ltd

PINDA: CCM ITAELEZA HAYA KWENYE KAMPENI ZA UCHAGUZI MKUU

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, jana alihitimisha mjadala wa makadirio ya Bajeti ya Ofisi yake ya Sh trilioni 5.7 ambayo ilipitishwa na Bunge, huku akifafanua hoja zitakazotumiwa na CCM kuomba kura za wananchi katika Uchaguzi Mkuu ujao.


Pinda alisema hakuna haja ya kuandikia mate wakati wino upo na kufafanua kuwa katika Uchaguzi Mkuu, CCM itatakiwa kueleza mafanikio ya Serikali katika nishati ya umeme vijijini, miundombinu ya barabara, elimu, maji na afya.


Alitaka waliokuwa wakijiuliza nani atashinda katika uchaguzi huo, wapitie kidogo historia kuanzia mwaka 1995 mpaka katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uliofanyika Desemba mwaka jana, ili waelewe nani alipata kipigo.


Elimu


Akifafanua kwa ufupi mafanikio yaliyopatikana katika elimu, Pinda alisema watakapoulizwa katika sekta hiyo nini kimefanyika, wataweka wazi kuwa ingawa bado kuna changamoto lakini yapo pia mafanikio makubwa.


“Wacha tubebe lawama katika changamoto, lakini tutaeleza kuwa katika vyuo vya ufundi mwaka 1995 na 1996, udahili katika vyuo vya ufundi ulikuwa 7,700 tu, mwaka 2005 wanafunzi 78,000 lakini takwimu za 2013, waliodahiliwa walikuwa wanafunzi 145,000,” alisema.


Katika vyuo vikuu, alisema mwaka 2005 walikuta vyuo vikuu vikiwa 23 lakini takwimu za 2013, zinaonesha kuwa vyuo vikuu vimefikia 50 na ongezeko hilo lisingewezekana kama si kuwepo kwa sera nzuri na usimamizi mzuri wa Serikali.


Kuhusu idadi ya wanafunzi waliodahiliwa katika vyuo hivyo, Pinda alisema mwaka 2005 walikuta wanafunzi 40,000 katika vyuo vikuu lakini mwaka 2015 wanaiacha nchi ikiwa na wanafunzi 200,000 waliopo katika vyuo vikuu mbalimbali.


Kuhusu ubora wa elimu aliosema kuwa una changamoto, lakini alikumbusha kuwa utafiti uliofanyika wa vyuo vikuu 100 bora Afrika, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),kiliibuka namba nne kwa ubora Afrika na kufuatiwa na Chuo Kikuu cha Capetown Afrika Kusini.


Katika elimu ya msingi, alisema alipokwenda Marekani alipatwa na mshangao kukabidhiwa Tuzo ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa katika Uandikishaji wa Wanafunzi wa Elimu ya Msingi.


Afya


Katika sekta ya afya, Pinda alisema umri wa kuishi wa Mtanzania umeongezeka huku vifo vya watoto chini ya miaka mitano vikipungua. “Tanzania ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika, zilizofanya vizuri katika kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano,” alisema.


Miundombinu ya barabara


Kuhusu miundombinu ya barabara, Pinda alihoji ni nani anayeweza kusimama kwa wananchi na kusema Serikali haijafanya chochote katika sekta hiyo.


“Hivi kuna anayeweza kusema kuwa katika barabara hatujafanya kitu na akasimama kwa wananchi kuomba kura? Njooni kule Rukwa nenda Kigoma useme hakuna kitu, nawahakikishia hamtapata kura,” alisema.


Aliwasema wabunge wa Kigoma ambao tangu Uhuru wamekuwa wakilalamika kuwa mkoa huo umetengwa na kushangazwa kwa hatua yao ya kutosema chochote kuhusu ujenzi mkubwa wa barabara kwenda katika mkoa huo na daraja kubwa la Kikwete.


Mbali na Daraja la Kikwete, Pinda alisema madaraja zaidi ya 20 yaliyokuwa kikwazo katika miundombinu ya barabara yamejengwa huku vivuko vingi katika mito, maziwa na bahari vikinunuliwa.


Maji, umeme


Kwa upande wa huduma ya maji, Pinda alisema kuna kazi kubwa imefanyika katika miaka miwili iliyopita na kutoa mfano wa Mradi wa Maji Karatu.


“Inasikitisha hata rafiki yangu wa Karatu akija hapa hasemi mradi huu ni mzuri. Wamejenga shule nzuri lakini hawasemi, lakini mimi nilipofika pale niliwasifia shule nzuri kwa kuwa najua wanatekeleza Ilani ya CCM,” alisema Pinda.


Kuhusu umeme vijijini, Pinda alisema ingawa hawajamaliza vijiji vyote lakini kazi imefanyika na kwa kuwa anaamini kuwa Serikali ijayo ni ya CCM, kazi hiyo itaendelezwa na Serikali ijayo.Kilimo
Katika kilimo, Pinda alisema changamoto kubwa iliyokuwa ikisumbua Taifa ilikuwa kukosekana kwa usalama wa chakula, jambo alilosema ilikuwa aibu kwa taifa kuomba chakula nje ya nchi.

Alisema Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, imejitahidi na leo Tanzania inatamba kuwa hata mikoa yenye njaa, italishwa kwa kutumiachakula kilichozalishwa ndani ya nchi.

AlisemaTanzania ni nchi ya nne barani Afrika kwa kuzalisha mahindi, duniani inashika nafasi ya 12 katika uzalishaji wa zao hilo huku akiongeza kuwa mwaka 2005 kulikuwa na matrekta 4, 000, sasa matrekta yaliyopo ni zaidi ya 10,000.

“Tusingewekeza katika uzalishaji wa mazao ya kilimo, tusingekuwa na jeuri ya kulisha mikoa yote yenye njaa. Kwa sasa tunaweza kulisha hata nje ya nchi na hivi karibuni, Sudan walikuja kuomba tuwasaidie. “Hata Kenya mwaka jana walikuja kuomba tuwasaidie tani 240,000 na tukawapa…nasema lazima tuone jeuri katika hilo,” alisema Pinda.

Uchumi


Pinda alisema yapo mambo mengi yanafanyika katika uchumi wa nchi na kutoa mfano wa utafiti wa wataalamu wa Benki ya Dunia (WB) wa mwaka 2012 kwa kushirikiana naTaasisi ya Business Insider kuhusu nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi.

Kwa kutumia vigezo vya ukuaji wa uchumi, Pinda alisema utafiti huo ulikuja na nchi 29 duniani ambazo zina uchumi unaokua kwa kasi na Tanzania ilishika namba 15.

Mbali na utafiti huo, mwingine ulifanywa na taasisi ya KPMJ ya Afrika Kusini kutafuta nchi kumi zenye uchumi unaokuwa barani Afrika na Tanzania ikashika nafasi ya sita.

Pia alitaja utafiti wa kikanda uliofanywa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) Aprili mwaka huu, ikabainishwa kuwa Tanzania inafanya vizuri. “Katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, sisi ndio tunaong’ara na hata hao watafiti wakija wanaona viashiria vilivyo bayana kabisa vya ukuaji wa uchumi,” alisema Pinda.

Alitoa mfano wa Mkoa wa Dodoma, kwamba alipokuwa anakuja na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere miaka ya 1980 na mkoa huo ulivyo sasa ni vitu viwili tofauti.

Ujenzi wa madarasa Pinda alisema anajua mafanikio hayo lazima yawaume Kambi ya Upinzani kwa kuwa wamenyang’anywa hoja za kuwaeleza wananchi katika uchaguzi mkuu.

Alisema hata kama inawauma hivyo, lakini ni vyema wanapojadili waheshimiane kuliko ilivyokuwa wakati wa kujadili makadirio ya Bajeti ya ofisi yake, ambapo baadhi ya wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani, walifikia hatua ya kuacha kuheshimiana na kuwaita mawaziri hawana akili.

“Ah! Inaonekana upande huo mna akili sana, lakini hivi Mbowe mkija kushika madaraka na sisi tukakaa huko tuache kuwaheshimu mtafurahi? Msiwatendee wenzenu lile msilopenda kutendewa,” alisema Pinda.

Alimtaka Mbowe na kundi lake la Umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA), katika mikutano yao ya kuchangisha fedha, wajaribu hata kujenga darasa moja ili wajue anachozungumzia cha kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo nini maana yake.



Chanzo: Habari Leo

KAMANDA WA WAASI ADF KUREJESHWA UGANDA

Waasi wa kikundi cha ADF.
SERIKALI ya Tanzania inatarajia kumpeleka Uganda Kamanda wa Kikosi cha Waasi cha ADF cha Uganda, Jamil Mukumu aliyekuwa akitafutwa muda mrefu hapa nchini na Shirika la Kimataifa la Polisi (Interpol).

Atapelekwa Uganda baada ya taratibu za kumfikisha mahakamani kukamilika.

“Baada ya kukamatwa mtu huyo tuliwauliza Umoja wa Mataifa kama watamchukua, lakini walikataa njia iliyobaki sasa ilibidi tumfikishe mahakamani na kisha mahakama kwa kufuata sheria ya kubadilishana wafungwa na mahabusu atapelekwa Uganda kwenye mashitaka yake,” alisema Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Alisema utaratibu huo wa kumpeleka Uganda unafanyika kisheria kwa sababu ndio njia pekee iliyobaki.

Membe alisema pamoja na tukio la wanajeshi wawili kuuawa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na wengine 15 kujeruhiwa, wanajeshi wa Tanzania wanafanya kazi nzuri.

Kundi la waasi la ADF limejikita mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) na limehusika kuua wanajeshi wa Tanzania.


Chanzo: Habari Leo

ALBINO AKATWA VIUNGO KATAVI

Katavi. Mwanamke mmoja mwenye ulemavu wa ngozi, Remi Luchoma (30), Mkazi Kijiji cha Mwamachoma, wilayani Mlele amekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana na kutokomea nacho.

Luchoma alikatwa mkono juzi saa sita usiku akiwa nyumbani kwa wazazi wake na sasa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda.

Kaimu mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dk Joseph Mkemwa alisema majeruhi huyo anaendelea vizuri na matatibu.

Akisimulia tukio hilo, Luchoma alisema akiwa amelala chumbani, alishtukia akivamiwa na watu wawili baada ya mlango kuvunjwa.

“Walipoingia ndani walinishika na mmoja alitoa panga na kunikata kiganja cha mkono wangu,” alisema Luchoma.

Ndugu wa karibu wa Luchoma, Maliselina Jackson alidai kuwa alisikia kelele za kuomba msaada kutoka kwa dada yake na alipoamka aliwaona watu wawili wakitoka chumbani.

“Niliwaona watu wawili wakitoka chumbani alikolala dada wakiwa na kiganja cha mkono, nilipiga kelele za kuomba msaada,” alisema Jackson.

Alisema dada yake alishindwa kufungua mlango kwa vile watu hao waliufunga kwa nje hadi walipofika majirani na kufanikiwa kumtoa.

“Baada ya majirani kufika, tulitoa taarifa kwenye Kituo cha Polisi Majimoto na muda siyo mrefu askari walifika na kuanza msako,” alisema.

Chanzo: Mwananchi

MVUA ZINAZOENDELEA DAR ES SALAAM KUPUNGUA MAKALI JUMAMOSI HII

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua za mfululizo zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam zitaendelea kunyesha na kwamba zinatarajia kupungua mwishoni mwa wiki hii.

Taarifa hiyo inaweza kuwa habari njema kwa wakazi wa Dar es Salaam na miji mingine iliyoathirika kwa kiasi kikubwa na mvua hizo zilizonyesha mfululizo na kusababisha vifo, uharibifu wa mali na miundombinu, huku hali ya usafiri, upatikanaji wa bidhaa hasa za vyakula ikiwa ngumu katika maeneo mengi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa  Huduma za Hali ya Hewa kwa Jamii wa TAM, Hellen Msemo alisema mvua hizi zinatarajia kupungua mwishoni mwa wiki hii; lakini sio kuisha kabisa na kwamba kwa sasa wananchi waendelee kufuatilia taarifa zinazotolewa.

“Mvua hizi zitaendelea kunyesha mpaka Ijumaa ya wiki hii na tunaweza kuona jua kidogo Jumamosi lakini sio mvua za kukatika kabisa zitaendelea kunyesha kidogo kidogo,” alisema Msemo.

Shule zajaa maji

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msasani ‘B’, Jane Reuben alisema mvua zinazoendelea kunyesha zimeathiri kwa kiasi kikubwa mahudhurio ya wanafunzi shuleni hapo huku wengine wakichelewa kufika darasani.

Gazeti hili lilishuhudia hali tete katika shule ya Msingi Msasani ‘A’ ambapo baadhi ya madarasa yamejaa maji na kushindwa kutumika na kuwalazimu wanafunzi kuchangia vyumba vya madarasa.

Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wengi wanaosoma katikati ya jiji wameshindwa kufika shuleni kwa kuhofia usumbufu wa usafiri kutokana na mvua ambayo imekuwa ikiendelea kunyesha.

Baadhi ya shule katika Kata ya Goba zimefungwa kwa muda kutokana na athari za mvua hizo. Foleni zawa kero Mvua hizo pia zimeendelea kuleta usumbufu mkubwa katika barabara nyingi za Dar es Salaam kutokana na kuharibika na kusababisha msongamano unaowafanya wakazi wa jiji hilo kupata wakati mgumu wa kuyafikia maeneo mbalimbali ama kikazi au shughuli binafsi.

HabariLeo ilishuhudia maeneo ya Posta Mpya katika barabara za Samora Avenue, Mkwepu, Ocean Road, Uhuru na zile zinazoelekea Magomeni na Mwenge zikiwa na msongamano wa magari.

Bidhaa bei juu Kwa upande wa bidhaa katika masoko, bei zimepaa na kusababisha kuongezeka kwa ukali wa maisha miongoni mwa wakazi wa Dar es Salaam.

Katika soko la Kariakoo, mfanyabiashara Baraka Lisulile anayeuza karoti alisema kabla ya mvua kilo moja ilikuwa inauzwa kwa Sh 2,000 lakini sasa imefikia Sh 3,000.

“Vile vile kabla ya mvua hizi kunyesha tenga la nyanya lilikuwa ni kati ya Sh 20,000 hadi Sh 35,000 lakini hivi sasa ni kuanzia Sh 48,000 hadi Sh 50,000,” alisema mfanyabiashara huyo.

Bidhaa za unga, mchele, maharage na aina nyingine za vyakula, nazo ziko juu. Nyumba zabomoka Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Musa Natty alisema mvua hizo zimefanya wananchi kukumbwa na uharibifu mkubwa ambao ni nyumba kufurika maji, kubomoka na barabara na madaraja kukatika.

Alisema katika manispaa hiyo maiti nne za wanaume na mwanamke moja zimepatikana na zimeripotiwa kata za Wazo Kunduchi na Mbezi beach.

Katika manispaa hiyo pia eneo la Africana nyumba zimejaa maji huku maeneo ya Nyaishozi kaya 151 zinahitaji msaada wa haraka ikiwemo mahema na chakula.

Alisema kata ya Tandale maeneo ya bondeni maji yameingia katika mitaa ya Pakacha, kwa Tumbo, Mahalitani, Sokoni, Mtogole na kwa Mkunduge.

Nyumba 14 ndizo zilizoathirika kwa kubomoka ambapo wakazi wake wamehifadhiwa na majirani.

Kata ya Kwembe watu 23 wamepata majeraha baada ya nyumba kuezuliwa paa, Shule ya Msingi King’azi ambayo inamilikiwa na Manispaa nayo imepata maafa ya kutitia na kutoa ufa kati ya lenta na paa.

Kata ya Mbweni familia 128 zimeathirika kwa kuzungukwa na maji na kukosa makazi na kuhifadhiwa na majirani na kata ya Magomeni mwili wa mtu mmoja umeopolewa akiwa amekufa, katika mtaa wa Suna watu 450 wamekosa makazi na mtaa wa Makuti A watu 250 hawana makazi na wanahifadhiwa na majirani.

Mtaa wa Idrisa watu 180 hawana makazi na nyumba nyingine 450 kuzingirwa na maji Kata ya Mabwepande daraja la mto Nyakasangwa mtaa wa Mbopo limekatika na kutitia hakuna mawasiliano kati ya pande mbili na barabara ya kwenda Mabwepande imekatika karibu na njia panda iendayo kwa waathirika wa Mji Mpya na nyumba 20 zimezingirwa na maji.

Kata ya Hananasif nyumba 400 ambazo ziko mabondeni zimezungukwa na maji na wakazi wa nyumba hizo wamehama makazi yao. Nyumba hizo ni zile zilizopo bondeni ambazo zilizobaki baada ya kubomolewa na wamiliki kupelekwa Mabwepande.

Kata ya Mabibo daraja la Tasaf linalounganisha Kata ya Mabibo na Makuburi limekatika kwa sababu ya wingi wa maji pamoja na nyumba tisa na vyoo.

Kata ya Manzese kumeripotiwa kifo cha mtu mmoja na kubomoka kwa nyumba moja. Daraja la linalounganisha kata ya Mbezi juu kwa Londa na Makongo kukatika.

Kata ya Wazo mtaa wa Mivumoni nyumba 13 zimeezuliwa na upepo mkali na Kata ya Kawe Mtaa wa Mzimuni nyumba 64 zimebomoka na nyingine kuzunguka na maji.

Kata ya Makumbusho mwili wa mtu mzima miaka 45 umeokotwa na waathirika 109 waliobomokewa na nyumba na zingine kujaa maji wamehifadhiwa shule ya msingi Kisiwani ambao wanahitaji msaada.

Kata ya Msasani Shule ya msingi msasani A imejaa maji katika madarasa 7 na nyumba za walimu na shule imefungwa kwa muda, Kata ya Sinza maji yamejaa yanaelekea katika makazi ya watu huku mtaa wa Barafu nyumba 3 zimebomoka na watu kukosa makazi huku nyumba 275 zimezungukwa na maji na kuhatarisha makazi.

Kata ya Mwananyamala katika mitaa ya Msisiri A na Msisiri B, Bwawani na mtaa wa Mwinyijuma jumla ya nyumba 150 zimezingirwa na maji na kuleta taabu kwa wakazi wake.

Kata ya Makuburi nyumba mbili zimebomoka na daraja la waenda kwa miguu linalounganisha Kata za Makuburi na Kimara kusombwa.

Kata ya Kimara familia saba zimehamia katika Kituo cha Polisi cha Kilungule A baada ya nyumba yao kujaa maji na kukatika, Kata ya Mizimuni nyumba tano zimevunjika kuta na kaya 15 zimehamia kwa majirani huku kaya 30 nyumba zake zimezingirwa na maji.

Kufuatia maafa hayo, Halmashauri imechukua jitihada mbalimbali ili kuokoa maisha ya watu na kuwawezesha kurudi katika makazi yao. Jitihada hizo ni pamoja ni kununua pampu za kunyonya maji ambayo yamezunguka makazi ya watu.Kazi hiyo ya kunyonya maji imeanza pamoja na kuzibua mitaro.




Chanzo: Habari Leo

HUENDA TANZANIA IKAKOSA MSAADA KUTOKA MAREKANI KWA SABABU YA RUSHWA

Serikali ya Tanzania iko hatarini kukosa dola za Marekani milioni mia saba sawa na trilioni 1.1 kwa fedha za Tanzania kwa ajili ya mradi wa pili wa mfuko wa changamoto za Milenia (MCC) kutokana na kushamiri kwa vitendo vya rushwa nchini humo.
Marekani imebainisha kuwa mkataba wa pili wa miradi inayofadhiliwa na shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC) utategemea hatua zitakazochukuliwa na serikali ya Tanzania dhidi ya wahusika wa kashfa hiyo.
Haya yanajiri wakati Rais Jakaya Kikwete akisubiriwa kutoa maamuzi ya mapendekezo yaliyofikiwa na Bunge kuhusiana na sakata la uchotwaji fedha zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka kaunti ya Tegeta Escrow wiki ijayo.
Katika tamko hilo kwa umma ambalo limewekwa kwenye tovuti ya MCC, bodi ilieleza kutambua umuhimu wa kusubiri na kuona utekelezaji kamilifu wa tamko lililotolewa na Ikulu ya Tanzania Desemba 9, mwaka huu kwamba itachukua hatua za haraka na kutoa maamuzi dhahiri na thabiti kuhusu maazimio ya Bunge juu la suala la IPTL.
Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ilieleza kuwa wakurugenzi wa MCC waliokutana katika mkutano wao uliofanyika Desemba 10, mwaka huu wamesikitishwa na hali ya rushwa nchini Tanzania.

Uamuzi huo wa Marekani ambayo inafadhili miradi mingi ya mabilioni ya fedha ni mtihani wa pili kwa Rais Kikwete baada ya ule wa maazimio ya Bunge yaliyotaka viongozi wakiwamo mawaziri waliotajwa katika kashfa hiyo kuwajibishwa.
Wanaotakiwa kuwajibishwa na Rais Kikwete ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa, Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Novemba mwaka huu, Serikali ya Marekani kwa kupitia MCC, ilikubali kutoa ruzuku ya hadi Dola za Kimarekani milioni 9.78 kwa ajili ya maandalizi ya miradi ya uwekezaji yenye matokeo makubwa katika sekta ya nishati nchini.
Tanzania ilikuwa mojawapo ya nchi kumi zilizojadiliwa na Bodi ya MCC iliyokutana kuangalia kama nchi hizo zimekidhi vigezo vya kuendelea na mchakato wa kuandaa mikataba mipya.
Wakati wa mkutano wa 16 na 17 wa Bunge, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alidokeza kusudio la Marekani kukataa kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya MCC, lakini Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alikanusha taarifa hizo.
Juhudi za BBC kumtafuta Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mark Childress,aweze kuzungumzia juu ya ripoti hiyo ziligonga mwamba kutokana na sababu za kiprotokali.


Chanzo: BBC