BBC YALAUMIWA KUVUNJA VIPINDI KWA AJILI YA MSIBA WA MANDELA
Wakati Dunia ikifuatilia kwa karibu safari ya mwisho ya Mandela hapa duniani, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limeripotiwa kuingia lawamani kutokana na uamuzi wake wa kupangua vipindi vingi na kuweka matangazo ya moja kwa moja ya mazishi ya kiongozi huyo wa zamani wa Afrika Kusini ambaye kabla ya kuingia Ikulu, alisota gerezani kwa miaka 27 kutokana na harakati zake zilizowakera makaburu.
Gazeti la Daily Mail la Uingereza limeripoti kuwa, watazamaji na wasikilizaji 1,834 wa redio na televisheni za BBC, wamelalamikia matangazo mfululizo ya mazishi ya Mandela. Mmoja wa wabunge wa chama cha Conservative, Conor Burns amekaririwa akisema hakukuwa na ulazima wa BBC kutumia muda mwingi na pia kupoteza fedha za walipa kodi kutuma wanahabari wanane kwenda Johannesburg, Afrika Kusini kwa ajili ya vipindi vya mahojiano katika shughuli ya kumuaga Mzee Mandela.“Tunafahamu heshima ya Mzee Mandela, alikuwa mmoja wa viongozi wa kipekee katika karne ya 20 na 21. Ametufundisha mengine juu ya amani na kuheshimu wengine, lakini BBC wamekurupuka na kutumia fedha nyingi badala ya kuwaeleza walipa kodi umuhimu wa safari hiyo na hata kukata vipindi zaidi ya 100 kwa wiki moja sasa,” anasema Burns.
Chanzo: BBC
Comments
Post a Comment