MWILI WA NELSON MANDELA KUZIKWA LEO KIJIJINI KWAKE QUNU
NDEGE ya kijeshi aina ya C-130 Hercules iliyobeba mwili wa Rais wa Kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini, ilitua Uwanja wa Ndege wa Mthatha jana majira ya saa 6.37.Ikisindikizwa na ndege nyingine mbili za kijeshi, iliruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kijeshi wa Waterkloof, Pretoria saa 4:58, tayari kwa safari ya mwisho ya kuuhifadhi mwili wa Mandela kwa maziko kijijini kwake Qunu katika Jimbo la Eastern Cape.Mwili wa mwanamapinduzi huyo kipenzi cha dunia, unatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya familia ya Mandela, shughuli inayotarajiwa kuanza saa 3 asubuhi.Shujaa huyo wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, alifariki dunia Alhamisi ya Desemba 5, 2013 saa 2:50 usiku nyumbani kwake, Mtaa wa Laa Namba 12, Houghton jijini Johannesburg akiwa amezungukwa na wanafamilia wote, wakiwemo mkewe Graca Machel na mtalaka wake, Winnie Medikizela –Mandela na mtoto wake mkubwa, Makaziwe Mandela.Tayari Serikali imetangaza leo kuwa siku ya mapumziko, ili kuwawezesha wananchi kufuatilia maziko ya kiongozi huyo ambaye tangu kufa kwake siku kumi zilizopita, amekuwa gumzo kubwa kutokana na heshima aliyojiwekea kote duniani.Kama ilivyokuwa katika miji ya Soweto na Pretoria ulikoagwa mwili wa shujaa huyo aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 95, Mji wa Mthatha nao ulifurika umati wa wananchi ambao bila kutarajia, walijikuta wakitengeneza mstari mrefu kutoka katikati ya mji hadi uwanja wa ndege kuulaki mwili wa shujaa wao.Na baada ya kutua, mwili huo ulizunguka katika mitaa ya Mthatha na baadaye kusafirishwa kwa msafara mkubwa wa magari na pikipiki za kijeshi hadi Qunu, umbali wa kilomita 31 kutoka Mthatha, huku anga lote la barabara iliyotumika kusafirisha mwili huo ikilindwa kwa helikopta za kijeshi.Akizungumza kutoka Qunu mapema, mmoja wa watu walioteuliwa na familia kusimamia maandalizi ya mazishi, Phathekile Holomisa kabla na kupaa kwa ndege na wakati wote wa safari angani, wazee wa familia walizungumza na mwili wa marehemu mithili ya mtu anayesikia, wakiutaarifu juu ya safari nzima kuelekea Qunu.“Wanazungumza na Mandela kama mtu aliye hai,” alisema Holomisa na kuongeza;” Hii ni kwa sababu tunaamini kiroho bado yu hai.” Mwili wa Mandela uliwasili kijijini Qunu saa 9:26 alasiri, huku mji wote ukiwa na umati mkubwa wa wananchi waliojitokeza kumlaki shujaa wao. Mara baada ya ujio wa mwili huo, helikopta nne za kijeshi zilionekana zikizunguka anga la Qunu.Tutu kutomzika `swahiba’ wakeLicha ya kuwa rafiki wa siku nyingi wa Mzee Mandela, taarifa za kushangaza zinasema kuwa, Askofu mashuhuri mstaafu wa Kanisa la Anglikana Afrika Kusini, Desmond Tutu ambaye pia ni Mshindi wa Nishani ya Amani ya Nobel, hatashiriki katika shughuli ya kuupumzisha kaburini mwili wa Mandela leo kijijini Qunu.“Hakuna taarifa zaidi zitakazotolewa kuhusiana na Askofu Tutu kutomzika Mandela,” anasema Mpho Tutu, binti wa Askofu Tutu ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Desmond Tutu na mkewe Leah. “Askofu hakualikwa, hivyo hatakwenda,” alikaririwa na kusisitiza kutozama katika kuelezea suala hilo.Taarifa za baadaye kutoka Ikulu ya Afrika Kusini zinasema, Askofu Tutu amealikwa kwenda Qunu. “Askofu Tutu si mtu wa kawaida, ana nguvu na ushawishi ndani na nje. Ni mtu muhimu nchini mwetu, yupo katika orodha yetu,” anasema Mac Maharaj wa Ikulu ya Afrika Kusini.Hata hivyo, vyombo vya habari vimedokeza kuwa, huenda hakualikwa kutokana na misimamo yake `migumu’ dhidi ya serikali ya sasa inayoongozwa na Jacob Zuma.Vyombo hivyo vimeongeza kuwa, Tutu hakuwamo katika orodha ya wasemaji siku ya mazishi ya kitaifa ya Mzee Mandela kwenye Uwanja wa Soka wa FNB, Soweto Jumanne wiki hii.Hata hivyo, katika dakika za mwisho aliombwa kutoa `neno’ baada ya umati wa waombolezaji kumzomea Rais Zuma. Askofu Tutu aliweza kupoza hasira za wananchi hao wa Afrika Kusini, baada ya kuzungumza kwa ukali akisema; “Tuioneshe dunia tumekuja hapa kumuaga shujaa wetu.Lazima tuoneshe kuwa sisi ni watu wenye nidhamu, tutulie na ikiwezekana kwa ukimya wenu nisikie sauti ya pini ikidondoka.”Alimmwagia sifa Mandela kuwa alikuwa mtu wa maajabu na alionesha maajabu akiwa hai kutokana na matendo yake yanayopaswa kuigwa na hata baada ya kuaga dunia, kwani licha ya kuiliza dunia nzima, amefanikiwa pia kuwakutanisha viongozi mahasimu wa kisiasa duniani katika uwanja mmoja wakimuaga.Miongoni mwa viongozi mahasimu waliokutana ni Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe aliyekutana na Rais Barack Obama na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron.Obama na Cameron waliweka vikwazo vya kiuchumi kwa Zimbabwe wakipinga matokeo ya uchaguzi uliompa Mugabe ushindi wa asilimia 61 dhidi ya wapinzani wake, wakidai kuwa kiongozi huyo alichakachua kura.Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Natanyahu ambaye awali aliripotiwa kutokwenda, alifika na kukaa katika uwanja mmoja na Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, licha ya kuwa na ugomvi wa muda mrefu na unaoendelea baina yao.Pia Rais Obama, alikutana na hasimu wa nchi yake wa siku nyingi, Rais Raul Castrol wa Cuba, ambao uhusiano wao umekuwa ukidorora tangu Mapinduzi ya Cuba ya mwaka 1959.Kutokana na uhusiano mbovu kati ya nchi hizo, mpaka leo Marekani haina uhusiano wa kibalozi na Cuba, huku nchi hiyo ikiweka katika sheria zake vizuizi kwa kampuni za Marekani kufanya biashara na Cuba.Nchini Marekani, wachambuzi wa kisiasa walishangazwa na uamuzi wa familia za kisiasa za Obama, George W. Bush na Bill Clinton, kupanda ndege moja kwenda Afrika Kusini kumuaga Mandela.
Comments
Post a Comment