HISTORIA YA KOMBE LA DUNIA TANGU 1930, WAANDAAJI & WASHINDI


KUANZISHWA KWA MICHUANO YA KOMBE LA DUNIA

Mafanikio ya michuano ya mpira wa miguu ya Olimpiki ndiyo yalikua mwanzo wa  FIFA kutamani kuwa na michuano yake ya Kombe la Dunia kwa mchezo wa mpira wa miguu. Ikumbukwe kwamba kipindi hicho mpira wa miguu wa wanaume pekee ndiyo ulikuwepo. Maswali yalitumwa kwa wahisani wa FIFA ili kuona kama wanakubaliana na uanzishwaji wa michuano hiyo na kwa masharti yapi? Kamati maalumu ilichunguza maswali hayo chini ya uongozi wa  Rais wa FIFA wa kipindi hicho Jules Rimet akishirikiana na Katibu wa Shirikisho la Soka nchini Ufaransa kwa wakati ule Henri Delaunay.
Rais wa FIFA Jules Rimet aliyeanzisha na kusimamia Kombe la Dunia la kwanza.
Kufuatia uwepo wa muswada wa Kamati Tendaji ya FIFA, lilifanyika kongamano la FIFA Mei 28, 1928 jijini Amsterdam nchini Uholanzi likiazimia kuwepo kwa michuano ya mabingwa wa soka duniani ambayo ilipangwa na shirikisho hilo la mpira duniani na sasa nchi waandaji wa michuano hiyo zilitakiwa kuchaguliwa. Hungaria, Italia, Uholanzi, Hispania na Uswidi (Sweden) ziliwasilisha maombi  ya kuandaa michuano hiyo kwa mara ya kwanza. Kwa kipindi hicho Urugwai ilikua ni nchi iliyokua ikipigiwa upatu kuandaa michuano hiyo si tu kwa sababu nchi hiyo ilishinda medali ya dhahabu ya Olimpiki mwaka 1924 na 1928 bali pia nchi hiyo ilikuwa ikijiandaa kusherehekea maazimisho ya miaka 100 ya uhuru wa nchi hiyo mwaka 1930. Hili pia lilikua ni kivutio kikubwa sana kwa nchi ya Urugwai pamoja na kule kushinda medali ya dhahabu katika michuano ya soka ya Olimpiki.

Mbali na hapo Urugwai ilikua tayari kugharamia gharama zote za usafiri pamoja na makazi na malazi kwa timu zote ambazo zingeshiriki michuano hiyo kwa makubaliano kwamba faida yoyote ambayo ingepatikana basi nchi hiyo ingegawana  na FIFA hata kwa kuchukua kiasi kidogo tu. Makubaliano haya yaliazimiwa na hivyo kongamano hilo la FIFA lililofanyika jijini Barcelona, Uhispania mwaka 1929 kuipa kibali Urugwai kuwa nchi ya kwanza kuandaa michuano hiyo ya kombe la dunia. Hii ilifanya nchi nyingine zilizowasilisha maombi hayo kujitoa katika kinyang'anyiro hicho cha kuwania uandaaji wa michuano hiyo.

Kwa kipindi hiki bara la Ulaya lilikuwa katika mdororo mkubwa wa uchumi ambao ni mkubwa zaidi kuwahi kutokea duniani na hivyo hii ilipekea idadi ndogo ya ushiriki wa nchi za Ulaya. Pia, katika kipindi hiki usafiri wa ndege ulikuwa bado haujapanuka sana kwa hivyo ilizigharimu nchi za Ulaya kusafiri umbali mrefu kwa meli mpaka kufika huko Urugwai ambayo ni nchi katika bara la Amerika ya Kusini. Nchi washiriki wa michuano hii walitakiwa kutangaza wachezaji wao miezi miwili kabla ya michuano hii ili kurahisisha safari kuelekea Urugwai.

Mashirikisho mengi ya soka barani Ulaya yalivunja ahadi hii ya ushiriki katika michuano hii na ilitumia muda sana kwa Rais wa FIFA wa kipindi kile Rimet kuzishawishi nchi za Ufaransa, Ubelgiji, Romania na Yugoslavia kukubaliana naye katika safari ya kuelekea Buenos Aires, Ajentina kwa safari ya kuelekea Urugwai. Mara ya kwanza hakukuwepo na vigezo vya ushiriki kwa hatua ya makundi. FIFA ilizialika nchi zote ambazo zilikua wanachama wake kwa kipindi kile lakini ni nchi 13 tu zilizoshiriki michuano hiyo. Nchi hizo ni Urugwai, Ajentina, Brazil, Bolivia, Chile, Mexico, Paragwai, Peru, Marekani, Ubeligiji, Ufaransa, Romania na Yugoslavia. Timu zilikua katika makundi 4; kundi A likiwa na timu 4 na makundi B-D yakiwa na timu 3 kila moja. Timu hizi zilicheza mechi 18 na jumla ya magoli 70 yalifungwa, hii ni sawa na wastani wa magoli 3.89 kwa kila mechi. Mechi zote zilichezwa katika viwanja vitatu vyote vikiwa jijini Montevideo mji mkuu wa Uruguay. Guillermo Stábile (Ajentina) ndiye alikua mfungaji bora wa michuano hii. Alifunga jumla ya magoli 8.
Guillermo Stabile (Argentina) mfungaji bora wa Kombe la Dunia la kwanza 1930.
Michuano hii ya kombe la dunia kwa mara ya kwanza ilifunguliwa katika dimba jipya la Estadio Centenario katika jiji la Montevideo, hii ilikuwa Julai 13, 1930. Tukio hili likafungua mwanzo mpya wa soka duniani na kupelekea mafanikio makubwa katika soka  na kifedha pia. Kiukweli, wandaaji wa michuano hii hawakuridhishwa na ushiriki wa nchi 4 tu za Ulaya nilizozitaja hapo juu. Yaliyotokea huko katika michuano hiyo nchini Urugwai yalikuwa ya mafanikio makubwa sana na hii ikapelekea bingwa wa michuano hiyo ya dunia kutotwaaa taji hilo tena kwa miaka minne iliyofuata baadaye. Kwa hivyo Urugwai ndiye mshindi wa kwanza wa michuano hii ya kombe la dunia mwaka 1930 wakiwa nyumbani kwao.
Dimba la Estadio Centenario mwaka 1930 ambako mechi ya kwanza ya Kombe la Dunia ilichezwa
Baraza la Kongresi la FIFA lilipokutana tena baadaye mwaka huo 1930 jijini Budapest, Hungaria waliishukuru sana Uruguay kwa kukubali kuandaa michuano hiyo ya kwanza ya kombe la dunia katika mazingira magumu. Sambamba na shukrani hizo, baraza hilo la FIFA lilielezea masikitiko yake kwa ushiriki ambao haukuridhisha hasa hasa kwa nchi za Ulaya.

Umuhimu wa tukio jipya la michuano hiyo uliongezeka zaidi kufuatia kushindwa kwa kufanyika michuano ya Olimpiki mwaka 1932 ambayo ilipangwa kufanyika Los Angels, California nchini Marekani. Hii ikachochea zaidi ushiriki katika michuano ya FIFA ya kombe la dunia lililofuata.

FIFA iliichagua Italia ambayo ilikuwa ikiwania uandaaji na Sweden kuwa waandaaji wa pili wa michuano hiyo. Safari hii kulikuwa na mechi za kufuzu tofauti na ilivyokua katika michuano ya awali kufuzu katika hatua ya makundi tofauti na michuano ya awali ambayo kulikua timu ikifungwa basi inaondolewa katika michuano hiyo. Brazil na Argentina ziliondolewa katika mechi moja tu za awali katika michuano ya mara ya kwanza. Kwa mara nyingine tena kama ilivyokua kwa timu waandaaji Uruguay kutwaa ubingwa 1930, timu waandaaji Italia walishinda wakiifunga Czechoslovakia katika muda wa nyongeza. Safari hii michuano hii ya kombe la dunia ilitangazwa redioni kwa mara ya kwanza.

Miaka 4 iliyofuata, Rais wa FIFA, Rimet alishuhudia matarajio yake yakitimia pindi michuano hiyo ilipoandaliwa kwa mara ya tatu nchini Ufaransa ambapo ni nyumbani kwake. Kwa mara nyingine tena mambo hayakwenda sawa na matarajio baadaya kuona Austria ikijiondoa kwenye michuano hiyo na kufanya Sweden kukosa timu ya kucheza nayo raundi ya kwanza. Uruguay haikutaka tena kushiriki na pia Argentina ilijitoa katika michuano hiyo ya tatu na hii ndiyo ilikuwa sababu nchi za Cuba na Indonesia (wakati ule ikiitwa jimbo la Udachi ya Mashariki ya Hindi) zikielekea Ufaransa kushiriki michuano hiyo ya tatu. Italia ilichukua tena ubingwa kwa mara ya pili ikitetea ubingwa wake wa mwaka 1934 waliochukua wakiwa nyumbani.

Michuano mingine ya kombe la dunia ilitakiwa kufanyika mwaka 1942 lakini kutokana na mapigano ya Vita ya Pili ya Dunia ambayo ilidumu kuanzia 1939 hadi 1945, michuano hiyo haikuweza kufanyika hivyo Italia iliendelea kuwa kuwa bingwa mtetezi kwa kipindi chote hicho hadi mwaka 1950 ilipochezwa tena michuano hiyo.

Licha ya Vita hiyo ya Dunia, makao makuu ya FIFA yaliendelea kuwa jijini Zurich nchini Uswisi. Julai 1, 1946 baraza la Kongresi la FIFA lilikutana tena nchini Luxembourg ambapo jumla ya mashirikisho 34 ya soka yalikutana katika jubilei ya miaka 25 ya Urais wa Rimlet FIFA. Kuanzia hapo kombe la dunia liliitwa jina la Kombe la Jules Rimet (Jules Rimet Cup) kwa heshima ya Rais huyu katika michuano hii hadi mwaka 1970. Baadaye mwaka 1974 kombe liliitwa Kombe la Dunia la FIFA (FIFA World Cup) hadi sasa.
Kombe la Dunia la Jules Rimet mwaka 1966.

Brazil ilichaguliwa kuandaa michuano ya mwaka 1949 lakini baadye iliahirishwa kwa sababu za muda na kusogezwa hadi mwaka 1950. Uswisi ilipewa nafasi ya kuandaa michuano ya mwaka 1954. Hii ndiyo ilikuwa historia ya michuano hii ya kombe la dunia mpaka kufikia mwaka 1949.

HISTORIA YA USHIRIKI

Katika historia ya kombe la dunia mwaka 1930 ni nchi 13 zilishiriki bila kufuzu, zilialikwa nchi wanachama wa FIFA tu. Michuano hiyo ilifanyika kati ya Julai 13 hadi 30, 1930. Mataifa yaliyoshiriki mwaka huo ni Argentina, Ubelgiji, Chile, Bolivia, Brazil, Ufaransa, Mexico, Paraguay, Peru, Romania, Uruguay, Marekani na Yugoslavia.

Mwaka 1934 zilishiriki timu 16 zikipitia kufuzu kwa hatua ya makundi. Michuano ilifanyika kuanzia Mei 27 hadi Juni 10, 1934. Hapa michuano hii ilihusisha mataifa kutoka kanda 4 za FIFA ambazo ni Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Shirikisho la Soka barani Amerika ya Kaskazini (CONCAF) na lile la Amerika ya Kusini (CONMEBOL) pamoja na Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA). Mataifa yaliyoshiriki ni Argentina, Austria, Ubelgiji, Brazil, Czechoslovakia kabla haijagawanyika kuunda nchi mbili za Jamhuri ya Czech na Jamhuri ya Slovakia, Misri, Ufaransa, Ujerumani, Hungaria (Hungary), Italia, Uholanzi, Romania, Uhispania (Spain), Uswidi (Sweden), Uswisi (Switzzerland) na Marekani.

Mwaka 1938 zilifuzu timu 16 lakini Austria alijitoa baadaye na hivyo kubaki na timu 15 kutoka mashirikisho ya CONMEBOL, CONCAF, UEFA na Shirikisho la Soka barani Asia AFC. Michuano ilichezwa kuanzia Juni 4 hadi 19, 1938. Mataifa yaliyoshiriki ni Ubelgiji, Brazil, Cuba, Ufaransa, Czechoslovakia, Ujerumani, Hungaria, Italia, Norway , Poland, Romania, Uholanzi, Uswisi, Sweden na Dutch East Indies ambayo kwa sasa inafahamika kama Indonesia.

Mwaka 1950 pia zilifuzu nchi 16 baadaye India, Uturuki na Uskochi (Scotland) zilijitoa na hivyo yakabaki mataifa 13. Hii ilichezwa kuanzia Juni 24 hadi Julai 16, 1950 ikihusisha kanda 3 za FIFA; CONCAF, CONMEBOL na UEFA. Mataifa yaliyoshiriki ni Bolivia, Brazil, Chile, Uingereza, Italia, Mexico, Paragwai, Uhispania, Sweden, Uswisi, Uruguay, Marekani na Yugoslavia.

Mwaka 1954 zilicheza timu 16 kutoka kanda nne za FIFA duniani. Hii ilifanyiaka Juni 16 hadi Julai 4, 1954. Kanza zilishiriki ni AFC, CONCAF, CONMEBOL na UEFA. Mataifa yaliyoshiriki ni  Austria, Ubelgiji, Brazil, Czechoslovakia, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Hungaria, Italia, Korea ya Kusini, Mexico, Uskochi, Uswidi, Uturuki, Uruguay na Yugoslavia.

Mwaka 1958 timu 16 zilishiriki lakini hakukua na timu ya bara la Asia wala Afrika. Hii ilifanyika kuanzia Juni 8 hadi 29, 1958. Kanda 3 za FIFA; CONCAF, CONMEBOL na UEFA ndizo zilishiriki mwaka huu. Mataifa washiriki ni Argentina, Austria, Brazil, Czechoslovakia, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Hungaria, Mexico, Ireland, Paraguay, Uskochi, Umoja wa Kisovieti (USSR), Uswidi, Wales na Yugoslavia.

Mwaka 1962 zilishiriki timu 16 bila nchi za Asia na Afrika kwa mara nyingine. Mechi zilichezwa kuanzia May 30 hadi June 17, 1962 kutoka Kanda 3 za FIFA; CONCAF, CONMEBOL na UEFA. Mataifa yaliyoshiriki ni Argentina, Brazil, Bulgaria, Chile, Colombia, Czechoslovakia, Uingereza, Ujerumani, Hungaria, Italia, Mexico, Umoja wa Kisovieti (USSR), Uhispania, Uswisi, Uruguay, na Yugoslavia.

Mwaka 1966 zilishiriki timu 16 katika kanda 4 za FIFA huku Korea Kaskazini ikishiriki kwa mara ya kwanza. Michezo ilianza Julai 11 hadi 30, 1966 safari hii ikihusisha kanda 4 za FIFA; AFC, CONCAF, CONMEBOL na UEFA. Mataifa washiriki ni Argentina, Brazil, Bulgaria, Chile, Korea ya Kaskazini, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Hungaria, Italia, Mexico, Umoja wa Kisovieti, Uhispania, Uswisi, Ureno na Uruguay.

Mwaka 1970 zilishiriki timu 16 kutoka kanda 5 za FIFA; CAF, AFC, CONCAF, CONMEBOL na UEFA huku Morocco ikiwa ni nchi ya kwanza ya Afrika kufuzu kucheza michuano hii. Michuano ilifanyika kuanzia Mei 31 hadi Juni 21. Mataifa yaliyoshiriki ni Ubelgiji, Brazil, Bulgaria, Czechoslovakia, El Salvador, Uingereza, Ujerumani, Israel, Italia, Mexico, Morocco, Peru, Romania, Umoja wa Kisovieti, Uswidi na Uruguay.

Mwaka 1974 timu 16 kutoka kanda 5 za FIFA; AFC, CAF, CONCAF, CONMEBOL na UEFA. Michuano ilichezwa kuanzia Juni 13 hadi Julai 7, 1974. Mataifa ya Argentina, Australia, Brazil, Bulgaria, Chile, Ujerumani ya Mashariki na Magharibi, Haiti, Italia, Uholanzi, Poland, Uskochi, Uswidi, Uruguay, Yugoslavia na Zaire (kwa sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) yalishirki.

Mwaka 1978 zilishiriki timu 16 kutoka kanda 5 za FIFA, AFC, CAF, CONCAF, CONMEBOL na UEFA. Michezo ilifanyika kuanzia Juni 1 hadi 25, 1978. Mataifa washiriki ni Argentina, Austria, Brazil, Ufaransa, Ujerumani, Hungaria, Iran, Italia, Mexico, Uholanzi, Uskochi Peru, Poland, Uhispania, Uswidi na Tunisia.

Mwaka 1982 ushiriki wa timu ukaongezeka hadi timu 24 kutoka kanda 6 za FIFA ikiwa ni mara ya kwanza kwa kanda zote kushiriki. Kanda hizo ni AFC, CAF, CONCAF, CONMEBOL, UEFA na OFC; Ukanda wa Visiwa vya Bahari ya Pasifiki ama kwa jina moja la kingereza, Oceania. Michuano ilianza Juni 13 hadi Julai 11, 1982 ikihusisha mataifa ya Algeria, Argentina, Austria, Ubeligiji, Brazil, Cameroon, Chile, Czechoslovakia, El Salvador, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Honduras, Hungaria, Italia, Ireland, Peru, New Zealand, Kuwait, Poland, Uskochi, Umoja wa Kisovieti, Uhispania na Yugoslavia.

Mwaka 1986 zilishiriki timu 24 zikicheza jumla ya mechi 52. Kanda 5 za fifa zilishiriki isipokuwa Ukanda wa Oceania, OFC.  Mei 31 hadi Juni 29, 1986 ndiyo kipindi michuano hii ilichezwa. Mataifa yaliyoshiriki ni Algeria, Argentina, Ubelgiji, Brazil, Bulgaria, Canada, Denmark, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Hungaria, Iraq, Italia, Korea ya Kusini, Mexico, Morocco, Ireland, Paraguay, Poland, Ureno, Uskochi, Umoja wa Kisovieti, Uhispania na Uruguay.

Mwaka 1990 zilishiriki timu zaidi ya 24 kukiwa na timu zaidi ya moja kutoka Asia. Kanda 5 za FIFA zilishiriki isipokua Ocenia kuanzia Juni 8 hadi Julai 8,1990.  Mataifa yaliyoshiriki ni Argentina, Austria, Ubelgiji, Brazil, Cameroon, Colombia, Costa Rica, Czechoslovakia, Misri, Uingerea, Ujerumani, Italia, Korea ya Kusini, Uholanzi, Jamhuri ya Ireland, Romania, Uskochi, Umoja wa Kisovieti, Uhispania, Uswidi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Uruguay, Marekani na Yugoslavia.

Mwaka 1994 zilishirki timu 24 kama kawaida kutoka kanda 5 za FIFA isipokua Ocenia. Michuano ilifanyika kuanzia Juni 17 hadi Julai 17, 1994. Mataifa washiriki ni Argentina, Ubelgiji, Bolivia, Brazil, Bulgaria, Cameroon, Colombia, Ujerumani, Ugiriki, Italia, Korea ya Kusini, Mexico, Morocco, Uholanzi, Nigeria, Norway, Jamhuri ya Ireland, Romania, Urusi, Saudi Arabia, Uhispania, Uswidi, Uswisi na Marekani.

Mwaka 1998 timu ziliongezeka hadi 32 katika makundi 8 ya timu 4 kila kundi. Mashirikisho kutoka kanda 5 za FIFA yalishiriki isipokua ukanda wa Ocenia. Michuano hii ilifanyika kati ya Juni 10 hadi Julai 12, 1998. Mataifa 32 yaliyoshirki ni Argentina, Austria, Ubelgiji, Brazil, Bulgaria, Cameroon, Chile, Colombia, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Iran, Jamaica, Japan, Croatia, Denmark, Korea ya Kusini, Mexico, Morocco, Uholanzi, Naijeria, Norway, Paragwai, Romania, Saudi Arabia, Uskochi, Afrika ya Kusini, Uhispania, Tunisia, Marekani na Yugoslavia.

Mwaka 2002 timu 32 huku ikiwa ni mara ya kwanza kwa michuano hii kuchezwa barani Asia. Ilifanyika katika nchi mbili tofauti; Korea ya Kusini na Japan kuanzia Mei 31 hadi Juni 30, 2002 ikihusisha Kanda 5 za FIFA  isipokua Ocenia. Mataifa washiriki ni Cameroon, Nigeria, Senegal, Afrika ya kusini, Tunisia, Argentina, Brazil, Ecuador, Paraguay, Uruguay, China, Japan, Korea ya Kusini, Saudi Arabia, Costa Rica, Mexico, Marekani, Ubelgiji, Croatia, Denmark, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Poland, Ureno, Jamhuri ya Ireland, Urusi, Slovenia, Uhispania, Uswidi na Uturuki.

Mwaka 2006 timu zilikua 32 zikiweka rekodi ya kucheza mechi 64. Michuano ilianza June 9 hadi Julai 9, 2006 ikihusisha kanda 5 za FIFA isipokua Ocenia. Mataifa washiriki ni Angola, Ivory Coast (Cote D'Ivore), Ghana, Togo, Tunisia, Australia, Iran, Japan, Korea ya Kusini, Saudi Arabia, Argentina, Brazil, Ecuador, Paraguay, Costa Rica, Mexico, Trinidad & Tobago, Marekani, Croatia, Jamhuri ya Czech, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Uholanzi, Poland, Ureno, Serbia na Montenegro, Uhispania, Uswidi, Uswisi na Ukraine.

Mwaka 2010 zilicheza timu 32 huku ikiwa ni mara ya kwanza kwa michuano hii kuchezwa barani Afrika. Huenda michuano hii iliyochezwa katika ardhi ya bara la Afrika ilikua na msisimko sana kutokana na kuchezwa kwa mara ya kwanza katika ardhi hii ya kifahari. Ilikua ni kati ya Juni 11 hadi Julai 11, 2010. Pamoja na yote binafsi huwa nazikumbuka zile nyimbo 3 ambazo zilikua na msisimko wa kipekee tangu kuanzishwa kwa michuano hii; wimbo wa kwanza ni ule wa Shakira - Waka Waka (This Time for Africa) ambao umetazamwa zaidi ya mara bilioni 3.4 katika mtandao wa YouTube, Shakira aliutendea haki huu wimbo na huenda ndiyo maana Mwenyezi Mungu akamkutanisha na Gerard Pique kabla hawajatengana 2022. Wimbo mwingine ni ule wa R. Kelly - Sign of Victory, huu nao ulikua ni 'wa moto' hadi dakika hii unaposoma hapa, mashairi yake yako 'relevant' sana. Kuna ule wa 3 aliuimba K'Naan - Wavin' Flag, nadhani unapata picha ya msisimko. Mataifa yaliyoshiriki kukipiga pale kwa Madiba ni  Algeria, Cameroon, Ivory Coast, Ghana, Nigeria, Afrika ya Kusini, New Zealand, Honduras, Mexico, Marekani, Argentina, Brazil, Chile, Paraguay, Uruguay, Australia, Japan, Korea ya Kaskazini na Kusini, Denmark, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Ugiriki, Italia, Uholazi, Ureno, Serbia, Slovakia, Slovenia, Uhispania na Uswisi.

Mwaka 2014 zilicheza timu 32 kutoka kanda 5 za FIFA isipokua Oceania. Michuano hii ilianza Juni 12 hadi Julai 13, 2014. Mataifa washiriki yalikua ni Algeria, Cameroon, Ivory Coast, Ghana, Nigeria, Ubelgiji, Bosnia & Herzegovina, Croatia, Italia, Ugiriki, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Ureno, Urusi, Uhispania, Uswisi, Australia, Iran, Japan, Korea ya Kusini, Argentina, Brazil, Chile, Colombia, Ecuador, Uruguay, Costa Rica, Honduras, Mexico na Marekani.
 
Mwaka 2018 zilicheza timu  32 kutoka kanda 5 za FIFA isipokua Ocenia. Michuano ilianza Juni 14 hadi Julai 15, 2018. Mataifa washiriki ni Misri, Morocco, Nigeria, Senegal, Tunisia, Argentina, Australia, Ubelgiji, Brazil, Colombia, Costa Rica, Croatia, Denmark, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Iceland, Iran, Japan, Korea ya Kusini, Mexico, Panama, Peru, Poland, Ureno, Urusi, Saudia Arabia, Serbia, Uhispania, Sweden, Uswisi na Uruguay.

Mwaka 2022 zilicheza jumla ya timu 32. Michuano hii ilifanyika nchini Qatar kuanzia Novemba 21 hadi Desemba 18 mwaka 2022 ikijumuisha kanda 5 za FIFA isipokua Ocenia. Mataifa yaliyofuzu kushiriki michuano hiyo yenye msisimko wa kipekee duniani ni Qatar, Senegal, Ecuador, Uholanzi, Uingereza, Iran, Marekani, Wales, Argentina, Mexico, Poland, Saudi Arabia, Australia, Denmark, Ufaransa, Tunisia, Ujerumani, Japan, Uhispania, Costa Rica, Morocco, Ubelgiji, Canada, Croatia, Brazil, Cameroon, Serbia, Uswisi, Ghana, Ureno, Korea ya Kusini na Urugwai.

Mwaka 2026 kwa mara ya kwanza dunia itashuhudia michuano hii ikichezwa katika majiji 16 ya mataifa matatu ya bara la Amerika ya Kaskazini; Marekani, Canada na Mexico. Ni kwa mara ya kwanza pia michuano hii itajumuisha jumla ya timu 48 kutoka katika kanda sita za FIFA. Marekani itahusika katika mechi 60 ikiwa ni pamoja na mechi zote za robo fainali hadi fainali. Canada na Mexico zitachezwa mechi 10 kila taifa na kufanya jumla ya mechi kuwa 80. Katika michuano hii ukanda wa Afrika (CAF) utakuwa na uhakika kupeleka timu 9 na moja italazimika kucheza play-off na timu kutoka ukanda mwingine wa FIFA. Ocenia (OFC) pia ina uhakika wa timu 1 na nyingine kama itafuzu kwenye play-off.

WAANDAAJI (1930-2026)

1930 Uruguay.
1934 Italia.
1938 Ufaransa.
1950 Brazil.
1954 Uswisi.
1958 Sweden.
1962 Chile.
1966 Uingereza.
1970 Mexico.
1974 Ujerumani.
1978 Argentina.
1982 Hispania.
1986 Mexico.
1990 Italia.
1994 Marekani.
1998 Ufaransa.
2002 Japan/Korea ya Kusini.
2006 Ujerumani.
2010 Afrika Kusini.
2014 Brazil.
2018 Urusi.
2022 Qatar.
2026 Canada/Marekani/Mexico.

WASHINDI WA KOMBE LA DUNIA (1930-2022)

1930 Uruguay ilitwaa ubingwa kwenye fainali dhidi ya Argentina.

1934 Italia ilitwaa ubingwa kwenye fainali dhidi ya Czechoslovakia.

1938 Italia ilitwaa ubingwa mara ya pili kwenye fainali dhidi ya Hungaria.

1950 Uruguay ilitwaa ubingwa kwenye fainali dhidi ya Brazil.

1954 Ujerumani ilitwaa ubingwa kwenye fainali dhidi ya Hungaria.

1958 Brazil ilitwaa ubingwa kwenye fainali dhidi ya Sweden.

1962 Brazil ilitwaa ubingwa mara ya pili kwenye fainali dhidi ya Czechoslovakia.

1966 Uingereza ilitwaa ubingwa kwenye fainali dhidi ya Ujerumani.

1970 Brazil ilitwaa ubingwa mara ya tatu kwenye fainali dhidi ya Italia.

1974 Ujerumani ilitwaa ubingwa mara ya pili kwenye fainali dhidi ya Uholanzi.

1978 Argentina ilitwaa ubingwa kwenye fainali dhidi ya Uholanzi.

1982 Italia ilitwaa ubingwa mara ya tatu kwenye fainali dhidi ya Ujerumani.

1986 Argentina ilitwaa ubingwa mara ya pili kwenye fainali dhidi ya Ujerumani.

1990 Ujerumani ilitwaa ubingwa mara ya tatu kwenye fainali dhidi ya Argentina.

1994 Brazil ilitwaa ubingwa mara ya nne kwenye fainali dhidi ya Italia.

1998 Ufaransa ilitwaa ubingwa kwenye fainali dhidi ya Brazil.

2002 Brazil ilitwaa ubingwa mara ya tano kwenye fainali dhidi ya Ujerumani.

2006 Italia ilitwaa ubingwa mara ya nne kwenye fainali dhidi ya Ufaransa.

2010 Hispania ilitwaa ubingwa kwenye fainali dhidi ya Uholanzi.
 
2014 Ujerumani ilitwaa ubingwa mara ya nne kwenye fainali dhidi ya Argentina.
 
2018 Ufaransa ilitwaa ubingwa mara ya pili kwenye fainali dhidi ya Croatia.

2022 Argentina ilitwaa ubingwa mara ya tatu kwenye fainali dhidi ya Ufaransa. 

REKODI ZA MICHUANO  (1930-2022)

  • Tangu 1930 imechezwa michuano 22 ya Kombe la Dunia (1930-2022).
  • Hadi 2022 ni mataifa 80 tu ambayo yamecheza michuano hii.
  • Kwa sasa Argentina ndiye bingwa mtetezi (2022). Hii ni mara ya tatu kwa taifa hili kutwaa ubingwa huu wa dunia (1978, 1986 na 2022).
  • Ni nchi 8 tu duniani zimeshawahi kutwaa ubingwa wa michuano hii (Brazil, Ujerumani, Italia, Argentina, Ufaransa, Uruguay, Uingereza na Hispania).
  • Ni timu 13 tu katika michuano yote 22 ambazo zimefika hatua ya fainali (Brazil, Ujerumani, Italia, Argentina, Ufaransa, Uruguay, Uingereza, Hispania, Uholanzi, Hungaria, Czechoslovakia , Sweden na Croatia).
  • Ni timu za Ulaya na Amerika ya Kusini pekee zilizotwaa ubingwa wa kombe la dunia mpaka sasa.
  • Brazil ndiyo timu pekee ambayo imeshiriki michuano yote 22 tangu 1930 ikifuatiwa na Ujerumani mara 20. Italia na Argentina mara 18 na Mexico mara 17.
  • Brazil ndiyo timu iliyotwaa ubingwa mara nyingi kuliko nchi nyingine. Imetwaa ubingwa mara tano (1958, 1962, 1970, 1994 na 2002) wakifungwa katika fainali mbili (1950 na 1998).
  • Timu 5 zimecheza fainali bila Ubingwa (Uholanzi, Czechoslovakia, Hungaria, Sweden na Croatia).
  • Ujerumani na Italia zimetwaa ubingwa mara nne. Ujerumani ndiyo nchi iliyoshindwa kutwaa ubingwa mara nyingi katika fainali za kombe la dunia, imefungwa mara nne katika fainali (1966, 1982, 1986 na 2002). Italia imepoteza mara mbili tu (1970 na 1994).
  • Uholanzi ndiyo nchi pekee iliyofika finali na kucheza na timu zaidi ya mbili na kushindwa kutwaa ubingwa. Wamepoteza katika finali tatu (1974, 1978 na 2010).
  • Marekani na Uturuki ndiyo nchi pekee nje ya mabara ya Ulaya na Amerika ya Kusini kumaliza katika nafasi ya 3.
  • Ujerumani ndiyo timu inayoongoza kwa kucheza finali nyingi za kombe la dunia. Imecheza mara nane (1954, 1966, 1974, 1982, 1986, 1990, 2002 na 2014) Brazil inaifuatia Ujerumani kwa kucheza fainali mara 7, Italia na Argentina mara 6.
  • Ni nchi 2 tu ambazo zimetwaa ubingwa mara mbili mfululizo. Italia (1934 na 1938) na Brazil (1958 na 1962).
  • Mabingwa watetezi walioondolewa kwenye hatua za makundi michuano iliyofuata; Italia (1950), Brazil (1966), Ufaransa (2002), Italia (2010), Hispania (2014) na Ujerumani (2018).
  • Lionel Messi ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi katika michuano hii. Amecheza jumla ya mechi 26 katika michuano 5 (2006, 2010, 2014, 2018 na 2022).
  • Pele ni mchezaji pekee aliyetwaa ubingwa na timu yake ya Brazil mara tatu (1958, 1962 na 1970). Rekodi hii bado haijavunjwa. 
  • Norman Whiteside (Ireland Kaskazini) ndiye mchezaji mdogo kuwahi kucheza katika michuano hii akiwa na miaka 17 na siku 41 (Ireland Kaskazini vs.  Yugoslavia, Juni 17, 1982).
  • Pele anashikiria rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo kucheza katika fainali ya kombe la dunia akiwa na miaka 17 na siku 249, fainali hii ilikuwa ni Brazil vs. Sweden Juni 29, 1958.
  • Essam El-Hadary (Misri) ndiye mchezaji mwenye umri mkubwa kucheza katika michuano hii akiwa na miaka 45  na siku 161 (Misri vs. Saudi Arabia, Juni 25, 2018).
  • Dino Zoff (Ujerumani) ndiye mchezaji mwenye umri mkubwa aliyecheza katika fainali za kombe la dunia akiwa na miaka 40 na siku 133 (Italia vs. Ujerumani Magharibi Julai 11, 1982).
  • Kylian Mbape ndiye aliyefunga magoli mengi katika hatua ya fainali akifunga jumla ya magoli 4 dhidi ya Croatia (2018) na Argentina (2022).
  • Cristiano Ronaldo ndiye mchezaji pekee aliyefunga magoli katika michuano mingi, akifunga magoli 8 katika michuano mitano (2006, 2010, 2014, 2018 na 2022).
  • Lucien Laurent (Ufaransa) ndiye mfungaji wa bao la kwanza kabisa katika historia ya kombe la dunia (Ufaransa vs. Mexico, Julai 13, 1930).
  • Angelo Schiavio (Italia) ndiye mfungaji wa bao la 100 na michuano hii ya Kombe la Dunia (Italia vs. Marekani, Mei 27, 1934).
  • Miroslav Klose ndiye mfungaji mwenye magoli mengi katika michuano hii akifunga jumla ya magoli 16 katika mechi 24 kwenye michuano minne (2002, 2006, 2010 na 2014).
  • Asamoah Gyan ndiye mchezaji pekee barani Afrika kufunga magoli mengi katika michuano hii akifunga jumla ya magoli 6. Hii ni sawa na kusema Gyan ndiye mchezaji pekee nje ya bara la Ulaya na Amerika ya Kusini kufikia idadi hiyo ya magoli.
  • Mwaka 2022 yalifungwa jumla ya magoli 172 ikiwa ndiyo michuano yenye magoli mengi zaidi katika michuano yote 22.
  • Rekodi ya mechi iliyokuwa na watazamaji wengi uwanjani ilichezwa Julai 16, 1950 kati ya Uruguay vs Brazil katika uwanja wa Maracanã jijini Rio de Janeiro, Brazil. Mechi hii ilihudhuriwa na watu 173,850.
  • Vittorio Pozzo ndiye kocha mwenye mafanikio ya kubeba ubingwa wa kombe la dunia mara mbili kama kocha akiwa na timu ya Italia akishinda mara 2 mfululizo (1934 na 1938).


MAKALA HII HUHARIRIWA MARA KWA MARA KUENDANA NA WAKATI TANGU MEI 2018. IMEANDALIWA NA KUANDIKWA NA VENANCE GILBERT KWA HISANI YA MTANDAO WA FIFA NA MITANDAO MINGINE.

KWA UANDISHI WA MAKALA MBALIMBALI ZA SOKA, ELIMU, BURUDANI, SIASA N.K WASILIANA NAMI KWA BARUA PEPE venancegilbert@gmail.com ama namba ya simu 0753400208.

Comments

  1. Kazi nzuri sana mkuu, ulieleza kila kitu cha muhimu.

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular Posts

MKUTAO WA G7 KUANGAZIA USALAMA NA MAZINGIRA

CHEKI PICHA HIZI ALIZOWEKA NICKI MINAJ INSTAGRAM

ZIFAHAMU NCHI ZINAZOZUNGUMZA KISWAHILI BARANI AFRIKA

BAADHI MAMBO AMBAYO HUKUYAFAHAMU KUHUSU BARA LA AFRIKA

WALIOCHAGULIWA CHUO CHA MIPANGO MAJINA HAYA HAPA

WAFAHAMU WAIGIZAJI 10 WA KIKE WA KOREA AMBAO NI WAREMBO KWA MWAKA 2017

WAFAHAMU MATAJIRI 10 WA TANZANIA MWAKA 2018

ZIFAHAMU GAUNI BORA 20 ZA MWAKA 2017