JIJI LA MBEYA KUKUSANYA BILIONI 64.8 MWAKA WA FEDHA UJAO
JUMLA ya shilingi bilioni 64.8 zinatarajiwa kukusanywa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya katika mwaka wa fedha 2014/2015.Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Musa Zungiza alipotoa taarifa ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka huo wa fedha kwenye kikao cha baraza la madiwani cha kujadili bajeti hiyo.Zungiza alisema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 11.3 sawa na asilimia 17.5 zitakusanywa kutoka katika vyanzo vya ndani vya halmashauri wakati michango ya nguvu ya wananchi itakuwa bilioni moja sawa na asilimia 1.5.Kutoka serikali kuu, halmashauri inatararajia kupokea Sh bilioni 37.7 sawa na asilimia 58 kwa ajili ya mishahara ya watumishi, Sh bilioni 3.4 sawa na asilimia tano kwa ajili ya matumizi mengineyo na Sh bilioni 11.4 sawa na asilimia 18 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.Zungiza alisema pia halmashauri inatarajia kutumia jumla ya Sh bilioni 64.8 katika mwaka huo wa fedha kwa ajili ya mishahara ya watumishi, utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida.Hata hivyo, baadhi ya madiwani akiwemo Meya, Athanas Kapunga na Diwani wa Kata ya Sinde, Fanuel Kyanula walihoji hatua ya miradi ambayo ujenzi wake haujakamilika ya Soko la Mwanjelwa na Hosteli iliyopo Sokomatola, kuingizwa katika matarajio ya kuwa sehemu ya vyanzo vya ndani vya mapato.Diwani Kyanula alisema ni kwa takriban miaka mitatu sasa, miradi hiyo imekuwa ikiingizwa katika bajeti kwa matarajio kuwa itakamilika kwa wakati na kuanza kuliingizia jiji fedha, lakini matokeo yake imekuwa ni kuzua hoja za ukaguzi.
Comments
Post a Comment