AJALI: BASI LAUA WATU 12 PAPO HAPO

Related image
Watu 12 wamekufa papo hapo na wengine zaidi ya 90 kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Korogwe, Tanga kwenda Dar es Salaam kuacha njia na kupinduka. Ajali hiyo ilitokea jana saa 1.30 asubuhi kwenye barabara kuu ya Segera-Chalinze katika kijiji cha Kwalaguru kata ya Kwedizinga wilayani hapa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alithibitisha jana kutokea kwa ajali hiyo ya basi la Burudani namba T 610 ATR aina ya Nissan. Majeruhi walipelekwa katika hospitali ya wilaya ya Korogwe ya Magunga, kwa matibabu ya awali na miili ya marehemu, akiwamo dereva wa gari hilo, Luta Mpenda (35) imehifadhiwa hospitalini hapo. 

“Tukiwa tunakaribia kwenye kona ile, tulipishana na lori hilo likiwa kasi upande wetu, dereva wetu akajitahidi kulikwepa lakini kutokana na ile kona kuwa kali, gari lilimshinda na kupinduka,” alisema Bendera. Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo walisema walisikia kishindo kutoka eneo hilo wakaenda na kukuta gari limepinduka na baadhi ya watu wamekufa. “Sisi tulikuwa tumekaa huku, ghafla tukasikia kishindo kikubwa tukakimbia kuangalia tukakuta ni basi la Burudani limepinduka, kusema kweli ile ajali ni mbaya sana,” alisema Zablon Mbaga.

Baadhi ya wakazi wa Korogwe waliofurika katika hospitali ya Magunga kutambua miili na majeruhi waliofikishwa hapo walisema idadi kubwa ya abiria waliokuwa wakisafiri katika basi hilo ni wafanyabiashara.“Wengi hapa ni wafanyabiashara ndio wanaotumia basi hili kwa sababu wana uhakika wakiondoka alfajiri saa 12, wanafika Dar es Salaam mapema na kugeuza jioni,” alisema Fatuma Bakari.

Mganga Mkuu wa Magunga, Dk Simon Mngiwa, alisema alipokea majeruhi ambao hali zao ni mbaya kutokana na kupasuka vichwa, kuvunjika miguu, mikono na kupata maumivu ya kifua.Baadhi ya majeruhi kwa mujibu wa Dk Mngiwa, walikimbizwa katika hospitali ya Bombo, KCMC Moshi na Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu ya Muhimbili (MOI). Rambirambi ya JK Kutokana na ajali hiyo, Rais Jakaya Kikwete, alimtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Galawa. “Nimepokea kwa mshituko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu 12 vilivyotokea na majeruhi baada ya basi la kampuni ya Burudani walilokuwa wakisafiria kutoka Korogwe kwenda Dar es Salaam kupinduka katika kijiji cha Taula,” alisema Rais Kikwete katika taarifa iliyotumwa jana na Ikulu.

Rais alisema vifo vya watu hao ni pigo kubwa si tu kwa familia za waliopoteza ndugu zao, bali pia Taifa kwa ujumla ambalo limepoteza nguvukazi muhimu iliyokuwa bado inahitajika kwa ujenzi wa Taifa. Rais Kikwete alimwomba Mkuu wa Mkoa kumfikishia salamu zake kwa familia, ndugu na jamaa waliopotelewa na wapendwa wao. Aliwahakikishia wafiwa kwamba yuko pamoja nao katika kipindi hiki cha maombolezo na kuwaomba wawe na uvumilivu, ujasiri na subira katika kipindi hiki kigumu wanachopitia wakiomboleza vifo vya ndugu zao. Aidha, aliwaombea kwa Mungu majeruhi wapone haraka na kurejea katika hali zao za kawaida, ili waungane na ndugu na jamaa zao na kuendesha maisha yao kama ilivyokuwa kabla ya kutokea kwa ajali.

Waliopoteza maisha katika ajali hiyo wametambuliwa kuwa ni dareva wa basi hilo, Luta Kimar, mkazi wa Kwasamangube Korogwe, aliyetajwa kwa jina la Mama Ally, mkazi wa National Housing Korogwe, Joyce Mokiwa (36) na mkazi wa Kambi ya Maziwa, Rehema Mandondo.Wengine ni Mwalimu wa Shule ya Mgombezi Korogwe, Msoke Mosha,mkazi wa Kilole Korogwe, Bashiri Shafii, mkazi wa Lutherani Korogwe, aliyetajwa kwa jina moja la Bryton, mkazi wa Bagamoyo Kilole Korogwe, Rehema Nassoro (23), Agnes Linus ambaye ni mkazi wa Mandera na Mariamu Juma ambaye hakutajwa eneo anakotoka.


Chanzo: Habari Leo

Comments

Popular Posts

MKUTAO WA G7 KUANGAZIA USALAMA NA MAZINGIRA

CHEKI PICHA HIZI ALIZOWEKA NICKI MINAJ INSTAGRAM

ZIFAHAMU NCHI ZINAZOZUNGUMZA KISWAHILI BARANI AFRIKA

WAFAHAMU WAIGIZAJI 10 WA KIUME WENYE MVUTO KOREA 2017

HISTORIA YA KOMBE LA DUNIA TANGU 1930, WAANDAAJI & WASHINDI

WAFAHAMU WAIGIZAJI 10 WA KIKE WA KOREA AMBAO NI WAREMBO KWA MWAKA 2017

BIBI WA MIAKA 85 AKAMATWA KWA KUIBA HERENI

MAMBO YA MUHIMU KUFAHAMU NA KUZINGATIA KABLA YA KUCHAGUA KOZI (TAALUMA) CHUO KIKUU

WAFAHAMU MATAJIRI 10 WA TANZANIA MWAKA 2018