MFAHAMU WOLE SOYINKA GWIJI WA FASIHI YA KIAFRIKA MWENYE TUZO YA NOBEL KATIKA FASIHI 1986
Picha kwa hisani ya Oasis Magazine Bila shaka jina la Wole Soyinka sio geni masikioni mwako kwa sababu wengi wetu tumesoma tamthiliya (play) yake ya The Lion and The Jewel sekondari hasa kidato cha tatu na cha nne na The Trials of Brother Jero kwa wale waliosoma miaka ya nyuma. Hapa nitamzungumzia Wole Soyinka, mwafrika wa kwanza kushinda tuzo ya Nobel katika fasihi. Haya ni mambo ambayo huwezi kufundishwa kwenye mitaala ya shuleni, hivyo unapaswa kuyafahamu nje ya mtaala wa shule kwa muda wako mwenyewe. Awali ya yote, ni kwamba wasifu huu niliuandika kwa mara ya kwanza katika mtandao wa Twitter Julai 13, 2020 kabla sijaamua kuuleta hapa. MAISHA YA MWANZO Soyinka alizaliwa Julai 13, 1934 huko Abeokuta jirani na Ibadan nchini Naijeria. Majina yake halisi ni Akinwande Oluwole Babatunde Soyinka lakini anafahamika sana kama Wole Soyinka. Alisoma Fasihi, Ibadan. Mwaka 1954 alijiunga na Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza mara baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo cha Serikali, Ibadan...