RAIS MTEULE WA MISRI KUAPISHWA JUMAPILI
Abdel Fatah al-Sisi ambaye amempinduwa kiongozi wa kwanza aliechaguliwa kwa njia ya demokrasia nchini Misri ataapishwa kuwa rais wa nchi hiyo Jumapili baada ya kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa rais wiki iliopita.
Tume ya uchaguzi hapo juzi imesema Sisi alishinda kwa asilimia 96.91 ya kura sawa na asilimia 47.5, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kumpinduwa Mohamed Mursi wa itikadi kali za Kiislamu.
Ushindi wake huo mkubwa dhidi ya mpinzani pekee kiongozi wa sera za mrengo wa shoto Hamdeen Sabahi ulikuwa haukutiliwa mashaka kabisa kutokana na kupongezwa na watu wengi kwa jemedari huyo mkuu mstaafu kukomesha utawala wa mwaka mmoja wa Mursi uliowagawa wananchi miezi kumi na moja iliopita.
Sisi ataapishwa saa moja na nusu asubuhi hapo Jumapili katika baraza kuu la Mahakama Kuu ya Kikatiba.Sherehe za kuapishwa kwake zitahudhuriwa na rais wa kipindi cha mpito Adly Mansour, Waziri Mkuu Ibrahim Mahlab na baraza lake la mawaziri,Imamu Mkuu Ahmed al- Tayeb wa Taasisi kuu ya Kiislamu nchini humo Al Azhar,Papa wa Kanisa la Koptik Tawadros wa Pili na viongozi wengine wa kisiasa na wa serikali.
Sherehe hizo zitafuatiwa na tafrija itakayohudhuriwa na wafalme na wakuu wa nchi katika Kasri la Ittihadiya mjini Cairo.
Wananchi watekeleze wajibu wao
Rais wa mpito anayeondoka madarakani amesema wananchi lazima wasimame kutekeleza wajibu wao kutokana na changamoto kubwa zinazoikabili nchi hiyo ambayo imetibuliwa na ghasia za umwagaji damu, machafuko ya kisiasa na njama za kimataifa zenye kutishia utambulisho wake na heshima ya mamlaka ya dola.
Katika hotuba yake ya kuaga aliyoitowa leo hii Adly Mansour mara nyengine akionekana karibu kutokwa na machozi,ameorodhesha matatizo yanayoikabili Misri wakati alipochukuwa madaraka karibu mwaka mmoja uliopita.Amesema hivi sasa nchi hiyo iko katika hali nzuri baada ya kupitishwa kwa katiba na sasa kufanyika kwa uchaguzi ambapo mkuu wa majeshi wa zamani al-Sisi ameshinda.
Hotuba yake hiyo inalingana na ilani ya kampeni ya Sisi kwamba Wamisri lazima wakomeshe machafuko nchini humo na kuwezesha ujenzi mpya wa taifa hilo.
Changamoto ni nzito
Hapo jana Sisi alijaribu kupunguza wasi wasi ulioko nchini humo wakati aliporudia kauli mbiu ya uasi wa mwaka 2011 akiwataka wananchi wa Misri kufanya kazi kwa ajili ya kujipatia mkate,uhuru,utu wa binaadamu na haki ya kijamii.
Mashrika ya haki za binaadamu ,viongozi wa kimataifa na wataalamu wameonya kwamba changamoto nzito zinamkabili Sisi wakati akiongoza nchi hiyo iliogawika vibaya.
Marekani imesema inasubiri kwa hamu kushirikiana na Sisi lakini pia imeelezea wasi wasi wake juu ya mazingira ya kisiasa yenye vikwazo ambapo kwayo uchaguzi wa wiki uliopita ulifanyika.
Uchaguzi huo wa Mei 26 hadi 28 ulisusiwa na kundi la Mursi la Udugu wa Kiislamu na makundi ya vijana ya vuguvugu la uasi wa umma wa mwaka 2011 kutokana na ukandamizaji wa sauti za upinzani unaoendelea nchini humo.
Comments
Post a Comment