MUME WA FROLA MBASHA ASEMA NI VIGUMU SANA NDOA YAO KUFIKIA MUAFAKA TENA
BAADA ya kudumu kwa zaidi ya miaka 10, imebainika kuwa ndoa ya mwanamuziki mahiri wa muziki wa Injili Bongo, Flora na mumewe Emmanuel Mbasha ipo chali kwa maana ya kuanguka huku ikidaiwa kuwa, kusimama imara tena inawezekana lakini ni kazi kubwa, Amani limefukunyua mazito
Hilo limejitokeza wiki moja baada ya madai ya mwanaume huyo kudaiwa kumbaka shemeji yake na kesi ipo polisi.
Imeelezwa Flora na mumewe ambao walifunga ndoa Agosti 22, 2002 wamepita katika migogoro mizito lakini wawili hao walikuwa wakiyamaliza kifamilia hadi kufikia hili la hivi karibuni ndilo lililoziba mataumaini ya wawili hao kuishi kama mume na mke.
Chanzo kilicho karibu na wawili hao kimeeleza kuwa, mzizi wa wawili hao kugombana ulichochewa na mwanamke mmoja (jina tunalo) ambaye alikuwa akikinzana na ushauri wa Mbasha mara kwa mara.
“Kuna vitu Mbasha alikuwa akimshauri huyo mama lakini walikuwa wakipishana Kiswahili na hapo ndipo tatizo lilipokua hadi kufikia hatua ya kumwagana,” kilisema chanzo.
TUJIUNGE NA MBASHA
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Emmanuel alizungumza na mwandishi wetu ambapo alikiri ndoa yake haina uhai tena na si rahisi kurejea katika hali ya kawaida licha ya kudai kuwa bado anampenda mkewe.
“Tulikuwa tunagombana sana na Flora lakini tulikuwa tukipatana ila mama… (anamtaja jina) alichangia ugomvi,
Flora naye alikuwa na nyendo zake mbaya, kuna wakati alikuwa anatoka kwenda gym (sehemu ya mazoezi) anachelewa kurudi ikafika wakati na nguvu ya ndugu wa mke ikawa kubwa kiasi cha kunizidi mimi na hapo ndipo mambo yalipofikia pabaya kabisa.”
FLORA ATIMKA NYUMBANI
Mbasha anaendelea: “Ugomvi ulizidi, ilifika wakati tulipishana kiasi cha yeye kuondoka nyumbani na kwenda kuishi katika nyumba ya wageni kwa miezi kadhaa wakati huo.
“Ndani ya ugomvi huo nilisikia mengi, baadhi ya watu wananiambia mke wangu anaonekana na Prado na mwanaume mwingine mwenye pesa, iliniuma sana ingawa sijawahi kumuona moja kwa moja,” alisema Emmanuel.
Kuhusu ugomvi huo, hivi karibuni Flora alikaririwa katika vyombo vya habari akisema hana tatizo na mumewe na ameshasamehe na kusahau yote yaliyopita hivyo ajitokeze tu ili akajibu mashitaka ya kudaiwa kubaka binti wa miaka 17 yaliyofunguliwa.
“Mimi sina tatizo kabisa na mume wangu, nimeshasamehe yote yaliyopita, kuhusu mashitaka ningeweza kuyafuta kama ningekuwa mimi ndiye niliyemshitaki,” alisema Flora.
FLORA ADAIWA KUHAMIA KWA GWAJIMA
Wakati gazeti hili likiendelea kusaka undani juu ya sakata hili, kuna chanzo kingine kilipenyeza data kuwa baada ya ugomvi kuwa mzito, Flora alihamia kwa Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Dar, Josephat Gwajima ambako ndiko alikuwa akisali kila Jumapili.
“Kwani nyinyi Global hamna habari? Flora amehamia kwa Gwajima Jumapili iliyopita, kwanza alihudhuria ibada jioni akaenda kuishi maana Gwajima ni mchungaji wake kwa sasa,” kilisema chanzo.
GWAJIMA ACHOMOA
Ili kupata mizani ya madai hayo, juzi Amani lilimpigia simu Mchungaji Gwajima na kumuuliza kama kweli Flora amehamia kwake kufuatia ugomvi kati yake na mumewe ambapo alikataa katakata.
“Flora hayupo hapa…mnataka niwaambiwe yuko hapa halafu vyombo vya habari muanze kuandika vibaya? Hakuna kitu kama hicho,” alisema Gwajima.
KWA NINI CHALI?
Ndoa kuwa chali ni ile ambayo imeanguka lakini inaweza kusimama tena tofauti na ndoa kuvunjika. Global iliwahi kuandika NDOA YA THEA CHALI baadaye ikasimama tena. Thea ni msanii wa filamu alifunga ndoa na Michael Sangu ‘Mike’ ambaye pia ni mwigizaji.
Wakati Emmanuel akizungumza na mwandishi wetu, alikiri kuwa Flora ameshamgeuka na nguvu kubwa imemuingia ndani ya moyo wake hivyo kuna ugumu sana wa kurudiana.
“Flora ambaye nilitegemea awe msaada katika hili lakini amefikia steji ya kuacha kunisikiliza, anasema haniamini, kwamba ninaweza kumfanyia lolote, sasa si bora kama anataka tuachane kwa heri kuliko kuniundia zengwe ambalo linataka kunipeleka mimi jela?” alihoji Mbasha.
Kutokana na mvutano huo pamoja na kesi hiyo ya kudaiwa kubaka inayomwandana Mbasha ni dhahiri kwamba kila mmoja hana imani na mwenzake tena hivyo suala la wawili hao kuishi kama zamani linakuwa gumu kuliko ngamia kupenya kwenye tundu la sindano.
Emmanuel Mbasha alishitakiwa katika Kituo cha Polisi cha Tabata Shule, Mei 30, mwaka huu kwa madai ya kumbaka shemejie.Uchunguzi juu ya tukio hilo unaendelea hadi sasa shitaka ambalo mwenyewe amelikanusha.
Canzo: GPL
Comments
Post a Comment