RAIS MSTAAFU ALI HASSAN MWINYI ATIMIZA MIAKA 93: TUJIKUMBUSHE HISTORIA YAKE KWA UFUPI
Mei 8, 1925 wkati huo Tanganyika ikiwa ni koloni la Uingereza alizaliwa Rais mstaafu wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mzee Ali Hassan Mwinyi.
Alipoingia
madarakani kumpokea aliyekuwa Rais wa Awamu ya kwanza,Mwalimu Julius
Nyerere mnamo tarehe 5 Novemba mwaka 1985, watanzania wachache sana
(kama wapo) waliweza kutabiri kwamba miaka kumi baadaye na zaidi baada
ya kustaafu rasmi, ataibuka kuwa mmojawapo wa maraisi wa Tanzania ambao
watabakia kupendwa na kuheshimika kwa namna ya kipekee kabisa.
Tunadiriki kusema “namna ya kipekee” kwa sababu ukweli unabakia kwamba
inapofanyika tathmini ya uongozi wake, bado mtu au watu mbalimbali
wanakuwa na maoni yao tofauti tofauti kuhusiana na suala hilo. Utoaji
huo wa tathmini ni suala ambalo haliwezi kukoma leo wala kesho, ni tukio
linaloendea na litakaloendelea, vizazi mpaka vizazi. Huo ndio uzuri au
ubaya wa historia na muda (history and time) huwa vina jinsi ya kipekee
katika kutoa hukumu zao.
Mpaka
anakabidhi madaraka yake ya Urais kwa Rais wa awamu ya tatu,
Mheshimiwa Benjamin William Mkapa mnamo tarehe 23 November mwaka 1995,
jina ambalo wengi tulipenda kulitumia ni “Mzee Ruksa” ingawa kamwe
hatukuwahi kusahau kwamba jina lake kamili ni Ali Hassan Mwinyi, Raisi
wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Ali Hassan Mwinyi alizaliwa tarehe 8 mwezi wa tano (Mei) mwaka 1923 katika
kijiji cha Kivure,wilayani Kisarawe, mkoa wa Pwani,Tanzania Bara. Kama
wengi wa viongozi wetu, Mwinyi naye alizaliwa katika iliyokuwa
Tanganyika. Akiwa bado mwenye umri mdogo sana familia yake ilihamia
Zanzibar. Kwa maana hiyo Mwinyi ni mzaliwa wa bara aliyekulia na
kuendelea kuishi visiwani Zanzibar.
Alianza
safari yake kielimu huko visiwani Zanzibar katika shule ya msingi
Mangapwani kuanzia mwaka 1933 hadi 1936 kabla ya kujiunga na shule ya
sekondari Dole kwa ajili ya elimu ya sekondari kuanzia mwaka 1937 mpaka
mwaka 1942. Baada ya hapo alijiunga na Chuo Cha Ualimu Zanzibar kusomea
ualimu kuanzia mwaka 1943 mpaka 1944.
Mwinyi katika picha rasmi ya wakati wa utawala wake. |
Kuanzia
mwaka 1945 mpaka mwaka 1950 alirejea tena katika shule ya
Mangapwani,shule aliyosomea,safari hii akiwa sio mwanafunzi tena bali
Mwalimu.Kuanzia mwaka 1950 mpaka 1954 alikuwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo
wakati huo huo alikuwa akiongeza elimu yake kwa njia ya posta ambapo
alijipatia General Certificate in Education (GCE) na pia alikuwa
amejiunga na Durban University Institute of Education, United Kingdom
(kwa njia ya posta tena) kusomea stashahada ya ualimu. Baada ya hapo
alijiunga tena na Chuo Cha Ualimu Zanzibar kama mkufunzi kuanzia mwaka
1956 mpaka mwaka 1961 huku pia akiendelea kujisomea kwa njia ya posta
kutoka Regent Institute kilichopo London nchini Uingereza ambapo alijipatia cheti cha ufundishaji lugha ya kiingereza.
Kuanzia
mwaka 1961 mpaka 1962 alijiunga na Hall University, Uingereza katika
Tutors’ Attachment Course. Mzee Mwinyi pia ana cheti ya lugha ya kiarabu
alichokipatia Cairo nchini Misri kati ya mwaka 1972 na 1974.
Safari
yake ya kisiasa aliianza rasmi mwaka 1964 alipojiunga na Afro Shiraz
Party (ASP) huko Zanzibar ambapo alikitumikia chama katika ngazi na
nafasi mbalimbali. Kati ya mwaka 1964 na 1965 alikuwa ni Katibu Mkuu wa
muda katika wizara ya elimu Zanzibar kabla hajateuliwa kuwa Naibu
Mkurugenzi katika iliyokuwa Zanzibar State Trading Corporation
(ZSTC).Hiyo ilikuwa ni kati ya mwaka 1965 na mwaka 1970. Pia katika
miaka hiyo hiyo,kuanzia mwaka 1966 mpaka 1970, Mwinyi alikuwa mweka
hazina msaidizi katika tawi la ASP la Makadara,Zanzibar. Wakati huo huo
pia kati ya mwaka 1964 mpaka 1977 alikuwa ni mwenyekiti wa Baraza la
Kiswahili Tanzania (BAKITA)
Majukumu
mengine aliyokuwa nayo miaka hiyo ni pamoja na uenyekiti wa Zanzibar
Censorship Board (1964-1965), Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha
Dar-es-salaam na pia mwenyekiti wa Baraza la Chakula na Lishe.
Mwinyi (kushoto) akiwa na maraisi wenzake wastaafu Benjamini Mkapa (kulia) na Jakaya Mrisho Kikwete (katikati) |
Kuanzia
mwaka 1972 mpaka 1975, Mwinyi alikuwa ni Waziri wa Afya wa Tanzania
kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kuanzia 1975 mpaka
1977. Mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri cheo
alichokitumikia mpaka mwaka 1982 aliporejea nyumbani na kuwa Waziri wa
Maliasili na Utalii cheo ambacho alikutumia kwa muda mfupi tu kwani
mwaka 1983 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi katika ofisi ya Makamu wa
Raisi.
Mwaka
1984, kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Raisi wa Zanzibar wakati
huo,Alhaj Aboud Jumbe, Mwinyi alichaguliwa kuwa Raisi wa Zanzibar,
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar na wakati huo huo Makamu wa
Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuanzia mwezi August mwaka huo
huo wa 1984 Mwinyi alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha
Mapinduzi cheo alichoendelea nacho mpaka mwaka 1990 baada ya kung’atuka
kwa Hayati Mwalimu Nyerere kutoka katika kukiongoza Chama Cha
Mapinduzi(CCM)
Mwinyi (wa pili kutoka kushoto) akishuhudia mchezo wa bao kati ya hayati Mwalimu Nyerere (wa pili kutoka kulia) na mzee mmoja wa Butiama(jina halijulikani).Wengine wanaoshuhudia ni Mama Maria Nyerere(kulia) na kaka yake Nyerere,Chief Burito(wa tatu kutoka kulia).Picha ilipigwa Butiama. |
Lakini
kabla ya hapo, mwaka 1985,Mwinyi alichaguliwa kuwa Raisi wa Awamu ya
Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kustaafu kwa Mwalimu
Nyerere. Mwinyi ni mtaalamu wa lugha ya Kiswahili na pia hupenda michezo
hususani jogging. Mwinyi ameoa wake wawili (Sitti Mwinyi na Khadija
Mwinyi), ana watoto na wajukuu. Anaishi Msasani jijini Dar-es-salaam.
Rai mstaafu Mwinyi akiwa na wastaafu wenziye Mkapa, Kikwete na Rais Magufuli. Picha kwa hisani ya Mwananchi Communication Limited. |
MAKALA HII NI HAKIMILIKI YA JEFF MSANGI MWANDISHI WA TOVUTI YA BONGOCELEBRITY.
Comments
Post a Comment