GOODALL MWANASAYANSI WA AUSTRALIA (104) AMEJITOA UHAI WAKE NCHINI USWISI
Mwanasayansi David Goodall, 104,
aliyesafiri kutoka Australia hadi Uswisi ili kujitoa uhai amefariki
katika kliniki moja nchini Uswisi, shirika linalotetea haki za watu
wanaotaka kufa limetangaza.
Mwanaikolojia huyo ambaye pia alikuwa
mtaalamu wa mimea hakuwa anaugua lakini alisema aliamua kujitoa uhai
kutokana na kudhoofika kwa 'ubora wa maisha yake'.
Goodall mwaka 1984 enzi za ujana. |
Bw Goodall alikuwa amezua mjadala kutokana na safari yake ya kutoka Australia kwenda kujitoa uhai.
Muda mfupi kabla ya kifo chake, alisema alikuwa na "furaha kuhitimisha" maisha yake.
"Maisha
yangu yamekuwa dhaifu sana kwa mwaka mmoja hivi uliopita na hivyo basi
nina furaha kuyahitimisha," alisema akiwa amezingirwa na jamaa wake
kadhaa.
"Nafikiria, kuangaziwa kwa kisa changu kutachangia kutetea
haki za wazee kuruhusiwa kujitoa uhai, jambo ambalo nimekuwa nikitaka."
Mtazame Goodall katika video hii hapa chini:
Alifariki
mwendo wa saa sita unusu mchana katika kliniki ya Life Cycle mjini
Basel baada ya kudungwa sindano ya Nembutal, kwa mujibu wa Philip
Nitschke mwanzilishi wa shirika la Exit International lililomsaidia
kujitoa uhai.
"Najuta kufika umri huu," Dkt Goodall alisema mwezi
uliopita katika sherehe ya kuzaliwa kwake, katika mahojiano na shirika
la utangazaji la Australia.
"Sina raha. Nataka kufa. Sio jambo la kuhuzunisha, kinachohuzunisha ni kwamba mtu anazuiwa kufa."
Ni
jimbo moja pekee Australia lililohalalisha kujitoa uhai mwaka jana
kufuatia mjadala mkali uliozusha mgawanyiko, lakini ili mtu kuruhusiwa,
ni sharti awe anaugua mahututi.
Je ni mataifa gani mengine yanaruhusu kujitoa uhai?
- Uswizi, ni nchi pekee iliyo na vituo vinavyotoa huduma hiyo kwa raia wa mataifa mengine.
- Uholanzi, Ubelgiji na Luxembourg zinaruhusu, hata kwa watoto lakini katika hali maalum.
- Colombia inaruhusu kujitoa uhai kwa hiari wakati mgonjwa akiwa hatibiki.
- Majimbo sita ya Marekani - Oregon, Washington, Vermont, Montana, California na Colorado - yannaruhusu kwa wagonjwa mahututi wasio tibika.
- Canada ililifuata jimbo la Quebec kuruhusu hilo mnamo 2016.
Mjadala unazua mgawanyiko Afrika
Katika nchi nyingi tu Afrika, njia zote za kujitoa uhai zinatizamwa kama mauaji. Wataalamu barani Afrika wamepinga wito wa watu kutaka kujitoa uhai kwa hiari. Mjadala mkubwa umezuka kuhusu kinachotajwa kuwa 'kuuawa kwa huruma' hususani kwa wagonjwa walio mahututi na wasioweza kutibika
Lakini
mkutano wa muungano wa wataalamu wa afya duniani katika mkutano mapema
mwaka huu mjini Abuja Nigeria waliamua kwamba hatua hiyo inakwenda
kinyume na kiapo cha matabibu na inakwenda kinyume na imani na maadili
ya jamii za Kiafrika badala yake viongozi katika muungano hao wametaka kuboreshwa kwa huduma za kuwashughulukia wagonjwa mahututi wasioweza kutibika.
Chanzo: BBC
Comments
Post a Comment