RAIS WA UZBEKISTAN AZIKWA KWA HESHIMA YA DINI YA KIISLAMU
Karimov, mwenye umri wa miaka 78 na ambaye ameiongoza Uzbekistan kwa muda mrefu, alifariki dunia jana Ijumaa baada ya kuugua kiharusi mwishoni mwa wiki iliyopita. Waziri Mkuu wa Urusi, Dmitry Medvedev anatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo yatakayofanyika kwa heshima ya dini ya Kiislamu.
Mazishi hayo pia yatahudhuriwa na viongozi wengine wa mataifa ya iliyokuwa Umoja wa Kisovieti, akiwemo Rais wa Tajikistan, Emmomali Rakhmon, Rais wa Turkmenistan, Gurbanguly Berdymukhamedov na Waziri Mkuu wa Kyrgyzstan, Belarus na Kazakhstan. Rais wa Marekani, Barack Obama ameelezea kusikitishwa na kifo hicho na amethibitisha kwamba nchi yake iko tayari kuwasaidia wananchi wa Uzbekistan katika kipindi hiki.
Waombolezaji wajipanga barabarani
Uvumi ulianza kuzagaa siku chache zilizopita kuwa kiongozi huyo amefariki dunia, lakini kifo chake kilithibitishwa rasmi hapo jana. Maelfu ya wananchi wa Uzbekistan wameanza kujipanga tangu mapema asubuhi ya leo, huku waombolezaji wengi wakiwa wamebeba maua waridi, ambayo wamekuwa wakiyaweka kwenye barabara. Waziri Mkuu wa Uzbekistan, Shavkat Mirziyoyev, ameteuliwa kuwa kiongozi wa kusimamia mazishi ya Karimov, hatua inayoonyesha kuwa huenda akawa rais ajaye wa nchi hiyo.
Mapema jana, serikali ya Uturuki ilitoa salamu za rambirambi kutokana na msiba huo. Akizungumza katika mkutano na baraza la mawaziri, Waziri Mkuu wa Uturuki, Binali Yildirim amesema wanaungana na watu wa Uzbekistan katika kipindi hiki cha majonzi. Aidha, katika taarifa yake aliyoitoa jana Rais wa Urusi, Vladmir Putin amekielezea kifo cha Karimov kama pigo kubwa kwa watu wa Uzbekistan.
Karimov ameitawala nchi hiyo ya Asia ya Kati tangu mwaka 1989 akiwa kama mwenyekiti wa chama cha Kikomunisti na mwaka 1991 alikuwa rais wa Uzbekistan wakati nchi hiyo ilipokuwa huru kutokana na kuvunjika kwa uliokuwa Umoja wa Kisovieti. Karibu ya nusu ya raia milioni 32 wa Uzbekistan, walizaliwa wakati wa utawala wake.
Wengi wanamchukulia Karimov kama kiongozi dikteta kutokana na maamuzi ya kikatili aliyoyafanya wakati wa utawala wake na serikali yake imekuwa ikishutumiwa kwa kukiuka haki za binaadamu. Steve Swerdlow mtaalamu kutoka Shirika la kimataifa la haki za binaadamu, Human Rights Watch Asia ya Kati, anasema kuwa Karimov alikuwa na utawala wa kimabavu, kwani aliwafunga gerezani na kuwatesa wapinzani na mahasimu wake kisiasa. Kwa mujibu wa Swerdlow, kiongozi huyo aliamuru jeshi kuwapiga risasi waandamanaji katika mji wa mashariki wa Andijan mnamo mwaka 2005, mauaji mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini humo.
Hadi sasa kiongozi huyo wa kimabavu hana mrithi kamili, hali inayozusha wasiwasi kwamba kifo chake kinaweza kusababisha kukosekana kwa hali ya utulivu. Mtoto mkubwa wa kike wa Karimov, ambaye alionekana kama anaandaliwa kuchukua nafasi ya baba yake, hajaonekana hadharani tangu mwaka 2014, huku kukiwa na uvumi kwamba yuko katika kizuizi cha nyumbani. Amekuwa akishutumiwa na waendesha mashtaka wa nchini Marekani na Ulaya, kwa kuhusika na rushwa.
Mtoto wa pili wa kike wa Karimov, Lola Karimov-Tillyaeva, ni balozi wa Uzbekistan katika shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Elimu, Sayansi na Utamaduni-UNESCO. Nchi ya Uzbekistan ina utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu, gesi asilia na pia ni msafirishaji mkubwa wa pamba.
Chanzo: Deutsche Welle (DW)
Comments
Post a Comment