Kenya jana ilisherehekea miaka 50 ya uhuru walioupata chini ya utawala wa Uingereza.Mamia ya raia na wageni mbali mbali wamehudhuria katika sherehe hizo zilizofanyika katika mji mkuu wa Nairobi.Wageni mbali mbali pamoja marais wa mataifa mbali mbali wamehudhuria sherehe hizo akiwemo Rais Godluck Jonathan wa Nigeria, Jakaya Kikwete wa Tanzania, Joseph Kabila wa DRC, Pierre Nkurunziza wa Burundi, Ali Bongo wa Gabon, Mahinda Rajapaksa wa Sri Lanka.Usiku wa kuamkia Alhamis bendera ya Kenya ilipandishwa katika eneo hilo hilo siku bendera ya uhuru ilipopandishwa wakati nchi hiyo inapata uhuru katika bustani ya Uhuru Desemba 12, 1963.Siku hiyo ya uhuru Rais Jomo Kenyatta, baba yake rais wa sasa Uhuru Kenyatta alitawazwa kuwa kiongozi wa nchi hiyo.
KINGEREZA CHAMCHANGANYA MKALIMANI AFRIKA KUSINI

Wataalamu wa lugha za ishara wamesema mtafsiri huyo wa lugha za ishara, Thamsanqa Dyanty, alikuwa "akitapatapa" wakati wa ibada hiyo siku ya jumanne. Naibu Waziri wa Afrika Kusini Hendrietta Bogopane - Zulu amesema hakuna suala lolote la kukiuka taratibu za kiusalama wakati mtafsiri huyo alipokuwa akisimama kwani alikuwa na vibali halali.
Katika maoni yake mtafsiri huyo anayelalamikiwa, Bwana Dyanty , amesema alipatwa ugonjwa wa kuchanganyikiwa. Kwa upande wake mmiliki wa kampuni iliyomtoa mtafsiri huyo imetupilia mbali madai ya Naibu waziri Bogopane Zulu.
Awali Naibu Waziri huyo aliwaomba radhi jamii ya viziwi kwa kiwango cha chini cha kutafsiri kilichofanywa na Bwana Dyanty kutoka kampuni ya SA Interpreters."Mtafsiri huyo anazungumza lugha ya Xhosa hivyo kiingereza kilikuwa kigumu sana kwake," alisema Waziri huyo.
AJALI: BASI LAUA WATU 12 PAPO HAPO
Watu 12 wamekufa papo hapo na wengine zaidi ya 90 kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Korogwe, Tanga kwenda Dar es Salaam kuacha njia na kupinduka. Ajali hiyo ilitokea jana saa 1.30 asubuhi kwenye barabara kuu ya Segera-Chalinze katika kijiji cha Kwalaguru kata ya Kwedizinga wilayani hapa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alithibitisha jana kutokea kwa ajali hiyo ya basi la Burudani namba T 610 ATR aina ya Nissan. Majeruhi walipelekwa katika hospitali ya wilaya ya Korogwe ya Magunga, kwa matibabu ya awali na miili ya marehemu, akiwamo dereva wa gari hilo, Luta Mpenda (35) imehifadhiwa hospitalini hapo.
“Tukiwa tunakaribia kwenye kona ile, tulipishana na lori hilo likiwa kasi upande wetu, dereva wetu akajitahidi kulikwepa lakini kutokana na ile kona kuwa kali, gari lilimshinda na kupinduka,” alisema Bendera. Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo walisema walisikia kishindo kutoka eneo hilo wakaenda na kukuta gari limepinduka na baadhi ya watu wamekufa. “Sisi tulikuwa tumekaa huku, ghafla tukasikia kishindo kikubwa tukakimbia kuangalia tukakuta ni basi la Burudani limepinduka, kusema kweli ile ajali ni mbaya sana,” alisema Zablon Mbaga.
Baadhi ya wakazi wa Korogwe waliofurika katika hospitali ya Magunga kutambua miili na majeruhi waliofikishwa hapo walisema idadi kubwa ya abiria waliokuwa wakisafiri katika basi hilo ni wafanyabiashara.“Wengi hapa ni wafanyabiashara ndio wanaotumia basi hili kwa sababu wana uhakika wakiondoka alfajiri saa 12, wanafika Dar es Salaam mapema na kugeuza jioni,” alisema Fatuma Bakari.
Mganga Mkuu wa Magunga, Dk Simon Mngiwa, alisema alipokea majeruhi ambao hali zao ni mbaya kutokana na kupasuka vichwa, kuvunjika miguu, mikono na kupata maumivu ya kifua.Baadhi ya majeruhi kwa mujibu wa Dk Mngiwa, walikimbizwa katika hospitali ya Bombo, KCMC Moshi na Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu ya Muhimbili (MOI). Rambirambi ya JK Kutokana na ajali hiyo, Rais Jakaya Kikwete, alimtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Galawa. “Nimepokea kwa mshituko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu 12 vilivyotokea na majeruhi baada ya basi la kampuni ya Burudani walilokuwa wakisafiria kutoka Korogwe kwenda Dar es Salaam kupinduka katika kijiji cha Taula,” alisema Rais Kikwete katika taarifa iliyotumwa jana na Ikulu.
Rais alisema vifo vya watu hao ni pigo kubwa si tu kwa familia za waliopoteza ndugu zao, bali pia Taifa kwa ujumla ambalo limepoteza nguvukazi muhimu iliyokuwa bado inahitajika kwa ujenzi wa Taifa. Rais Kikwete alimwomba Mkuu wa Mkoa kumfikishia salamu zake kwa familia, ndugu na jamaa waliopotelewa na wapendwa wao. Aliwahakikishia wafiwa kwamba yuko pamoja nao katika kipindi hiki cha maombolezo na kuwaomba wawe na uvumilivu, ujasiri na subira katika kipindi hiki kigumu wanachopitia wakiomboleza vifo vya ndugu zao. Aidha, aliwaombea kwa Mungu majeruhi wapone haraka na kurejea katika hali zao za kawaida, ili waungane na ndugu na jamaa zao na kuendesha maisha yao kama ilivyokuwa kabla ya kutokea kwa ajali.
Waliopoteza maisha katika ajali hiyo wametambuliwa kuwa ni dareva wa basi hilo, Luta Kimar, mkazi wa Kwasamangube Korogwe, aliyetajwa kwa jina la Mama Ally, mkazi wa National Housing Korogwe, Joyce Mokiwa (36) na mkazi wa Kambi ya Maziwa, Rehema Mandondo.Wengine ni Mwalimu wa Shule ya Mgombezi Korogwe, Msoke Mosha,mkazi wa Kilole Korogwe, Bashiri Shafii, mkazi wa Lutherani Korogwe, aliyetajwa kwa jina moja la Bryton, mkazi wa Bagamoyo Kilole Korogwe, Rehema Nassoro (23), Agnes Linus ambaye ni mkazi wa Mandera na Mariamu Juma ambaye hakutajwa eneo anakotoka.
Chanzo: Habari Leo
PINDA: NITAFURAHI NIKIONDOLEWA
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda uwaziri mkuu ni mzigo anaobeba kama Msalaba na ikiwa ataondolewa, atafurahi kwa kuwa atapumzika. Alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Kassim Mohamed (CUF), katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo.“Rais akiniambia nimeshindwa majukumu nitaondoka, huku nikiwa na kicheko, hata ninyi wabunge mna nafasi ya kuniondoa, mnaweza kufanya hivyo mkiona inafaa kwani nitafurahi na kupumzika,” alisema.Rukia katika swali lake, alimtaka Pinda kutoa ufafanuzi kuhusu kauli za wabunge wa CCM kuwa yeye ndiye mzigo. Alisema licha ya jitihada anazofanya kutekeleza wajibu wake kwa kusimamia wizara 20, anashangaa kuhukumiwa kwa upungufu unaotokea katika wizara moja au mbili.Alifafanua, kuwa anasimamia wizara kama 20 na zote zinafanya kazi vizuri, lakini kama kuna wizara moja au mbili hazijafanya vizuri sana, hiyo haitoshi kudai atimuliwe kazi.Alisema uzuri wa nafasi ya uwaziri mkuu, mtu haombi, bali anateuliwa na Rais kwa majaaliwa ya Mwenyezi Mungu, hivyo isipompendeza, ni kazi rahisi kwa Rais ambaye atamwambia kuwa ameshindwa jukumu lake na kumwondoa.“Bunge pia mnaweza kumwondoa Waziri Mkuu kwa uwezo wenu, hivyo dada Rukia kama unafikiri hilo na wabunge wote wakaona sawa, nipo tayari, tena nitafurahi kweli kweli angalau nimeutua Msalaba huu, mana’ke hii kazi ni ngumu,” alisema.Katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua kauli ya Waziri Mkuu iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuwa kuna baadhi ya mawaziri ni mizigo alipokuwa katika ziara yake mkoani Mbeya.Akijibu swali hilo, Pinda alisema hata yeye alisikia kauli hiyo kwenye vyombo vya habari akasema ni vema kumsubiri Kinana arudi kutoka katika ziara na kumsikiliza alichosema alikuwa na nia gani, ndipo wataona namna ya kwenda mbele zaidi.Hata hivyo, aliyesema bungeni kuwa Pinda ni mzigo kwa Serikali alikuwa Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) akisema ndiye ambaye anastahili aondolewe kwenye nafasi yake hiyo.Pia Waziri Mkuu alimwahidi Mbunge wa Mkanyageni, Habib Juma Mnyaa (CUF), kufuatilia kwa nini suala la kupeleka fedha za chenji ya rada hazijafikishwa Zanzibar. Alisema suala hilo lilishazungumzwa ndani ya Serikali wakakubaliana na likaisha.Aliongeza kuwa suala hilo ni la kisekta na litatolewa ufafanuzi zaidi na waziri husika. Katika swali lake la awali, Mnyaa alimwuliza Waziri Mkuu ni kwa nini hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya kauli iliyotolewa bungeni ya kushughulikia suala la chenji ya rada kupelekwa Tanzania Bara pekee.
UGANDA YAANZA KUILIPA TANZANIA FIDIA
SERIKALI ya Uganda tayari imeshaanza kulipa deni lake kwa Tanzania la dola za Marekani milioni 9.6 kati ya dola za Marekani milioni 18.4 ikiwa ni fidia kwa Tanzania kwa mchango wake katika kumuondoa Idd Amin Dada Uganda mwaka 1978.Hayo yalibainishwa bungeni jana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Shamsi Vuai Nahodha, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mbinga, John Komba (CCM).Katika swali lake Komba alitaka kujua kama Tanzania ilishaanza kudai fidia kwa Serikali ya Uganda kutokana na mchango wake wa kuisaidia nchi hiyo kumuondoa Idd Amin na kumfanya Rais wa sasa Yoweri Museveni kutawala kwa amani nchini humo.Akijibu swali hilo, Nahodha alikiri kuwa Tanzania ilipigana vita na Uganda kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka 1979 kutokana na uvamizi uliofanywa na Uganda chini ya utawala wa Idd Amin aliyevamia na kukalia sehemu ya ardhi ya Tanzania mkoani Kagera.“Kwa kuwa vita hivyo vilitokana na uvamizi wa Idd Amin, baada ya vita kumalizika Serikali ya Tanzania iliitaka Uganda kulipa fidia. Serikali hiyo nayo ilikubali kuilipa Tanzania fidia hiyo,” alisema Nahodha.Alisema kwa bahati mbaya Serikali ya Uganda haikutekeleza makubaliano hayo yaliyofanyika mwaka 1979 hivyo Serikali ya awamu ya tatu ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mstaafuma William Benjamin Mkapa ilifanya majadiliano tena na Uganda.Alisema kutokana na majadiliano hayo Serikali ya Uganda ilitakiwa kulipa fidia dola za Marekani milioni 18.4 na hadi sasa Serikali hiyo imeshalipa dola za Marekani milioni 9.6 fedha ambazo ziliwekwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali na nchi hiyo kubakiwa na deni la dola za Marekani milioni 8.8.Nahodha alisema majadiliano baina ya Tanzania na Uganda yanaendelea ili sehemu ya fidia iliyobaki iweze kulipwa chini ya Wizara ya Fedha ambayo ndio inayofuatilia deni hilo.Akijibu swali la nyongeza la Komba la kuitaka Tanzania imkumbushe Museveni juu ya namna Tanzania ilivyosaidia nchi yake hivyo aache kuihujumu kwa kusaidiana na Rais wa Rwanda Paul Kagame, Nahodha alisema siku zote Tanzania haimsaidii mtu ili kupata shukurani. Tanzania ni nchi ya kipekee sana, imebahatika kupata viongozi wenye sifa kubwa duniani kama Nyerere (Mwalimu Julius), kiongozi huyu aliwahi kusema Waafrika ni ndugu na Afrika yetu sote, tuliwasaidia Uganda kwa utu hatutegemei zaidi,” alisisitiza.Alisema hata juzi baada ya kifo cha Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Tanzania ilitoa tamko la kumuenzi kwa kusisitiza uvumilivu, jambo ambalo limeipatia sifa kubwa Tanzania. “Naomba tuendelee kuitunza sifa hii na si vinginevyo.”
Kikwete kumuaga Mandela leo
RAIS Jakaya Kikwete leo ataungana na viongozi wenzake kutoa heshima za mwisho na kuuaga rasmi mwili wa kiongozi mashuhuri wa Afrika Kusini na duniani, Nelson Mandela. Mwili wa Mandela unatarajiwa kuwekwa kwenye majengo ya Urais wa Afrika Kusini ya Union Buildings mjini Pretoria, ambayo sasa yataitwa Majengo ya Kumbukumbu ya Mandela.Jana Rais Kikwete aliungana na viongozi wa mataifa mbali mbali duniani na maelfu ya wananchi wa Afrika Kusini, kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Mandela.Maelfu kwa maelfu ya wananchi walihimili mvua kubwa iliyokuwa inanyesha kwa nguvu kwenye Uwanja wa Michezo wa FNB mjini Johannesburg, kumwaga Mzee Mandela ambaye alikuwa ishara kuu ya upinzani wa siasa za ubaguzi wa rangi za makaburu wa Afrika Mashariki.Baada ya kutoka jela, Februari 1990, Mandela alichaguliwa kuwa Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini mwaka 1994.Hata hivyo, Mandela alitumikia kipindi kimoja tu cha miaka mitano na kukataa kutumikia kipindi cha pili. Viongozi 91 kutoka sehemu mbalimbali duniani walihudhuria kumbukumbu hiyo iliyokuwa na kila aina ya mchanganyiko wa hisia, wengine wakiwa na majonzi na wengine wakicheza na kuimba kwa muda wote wa shughuli hiyo iliyochukua saa tano.Mbali na Rais Kikwete ambaye amefuatana na mkewe Mama Salma, marais wengine mashuhuri duniani waliohudhuria kumbukumbu hiyo ni Barack Obama wa Marekani, Francois Hollande wa Ufaransa, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroun na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon.Kumbukumbu hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi wa zamani wa Marekani wakiwemo marais watatu wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter, Bill Clinton na George Bush na mawaziri wakuu wawili wa zamani wa Uingereza, Tony Blair na Gordon Brown.
Jina la JK laongoza marais 100 watakaomzika Mandela
Johannesburg. Serikali ya Afrika Kusini, imetoa
orodha ya majina ya wakuu wa nchi na Serikali 91 ambao wamethibitisha
kushiriki katika shughuli zinazohusiana na safari ya mwisho ya Rais wa
kwanza mzalendo wa taifa hilo, Nelson Mandela.
Jina la Rais Jakaya Kikwete ni la kwanza katika
orodha hiyo inayowaweka viongozi hao katika makundi kutokana na mabara
wanakotoka. Rais Kikwete alitarajiwa kuwasili jana usiku tayari
kuhudhuria Ibada ya Kitaifa ya Mandela ambayo imepangwa kufanyika leo
kwenye Uwanja wa FNB (Soccer City).
Kabla ya Serikali kutoa orodha hiyo, Waziri wa
Uhusiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Maite Nkoana-Mashabane alisema
wakuu wa nchi na Serikali 53 walikuwa wamethibitisha lakini jana mchana
idadi hiyo ilikuwa imeongezeka na kufikia 91. Kulikuwa na wasiwasi
kwamba huenda idadi hiyo ikaongezeka na kuzidi 100.
Msemaji wa Wizara ya Uhusiano wa Kimataifa ya
Afrika Kusini, Clayson Monyela aliwataja marais wengine kutoka Afrika
kuwa ni kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Joseph Kabila,
Hifikepunye Pohamba wa Namibia, Mike Sall wa Senegal, Allessane Ouattara
wa Cote d’Ivoire, Goodluck Jonathan wa Nigeria, Robert Mugabe wa
Zimbabwe, Dennis Sassou-Nguesso wa Congo Brazaville, John Dramani wa
Ghana na Ali Bongo wa Gabon.
Kutoka Amerika ya Kusini ni marais Nicolus Maduro
Moros wa Venezuela na Dilma Rousseff wa Brazil ambaye ataambatana na
marais wanne wastaafu wa nchini kwake.
Waziri Mkuu wa Bahamas, Perry Christie, Rais wa
Guyana, Donad Ramotar, Rais wa Haiti, Michael Martelly na Rais wa
Jamaica, Portia Miller, wakati kutoka Asia, kutakuwa na marais Pranab
Mukherjee wa India na Hamid Karzai wa Afghanistan.
Rais Francois Hollande wa Ufaransa, Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbot, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon
Tayari Rais wa Marekani, Barrack Obama na mkewe
Michelle walishathibitisha kushiriki, pia watangulizi wake, Bill
Clinton, George W. Bush na Jimmy Carter wanatarajiwa kushiriki katika
mazishi ya Mandela yatakayofanyika Qunu, Mthatha Jumapili.
Armando Guebuza wa Msumbiji, , Abdelkader Bensalah
wa Algeria, Makamu wa Rais wa Angola, Manuel Vicente, Rais wa Niger,
Issoufou Mahamdou, Kaimu Rais wa Agentina, Amado Boudou, Waziri Mkuu wa
New Zealand, John Key na Rais wa Bangladesh, Abdul Hamid MD Abdul.
Malkia Haakon wa Norway, Mfalme wa Philippe wa
Ubelgiji, Rais wa Pakistan, Mamnoon Hussain, Rais wa Benin, Boni Yayi,
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas, Rais wa Botswana, Seretse Ian Khama,
Rais wa Ureno, Anibal Cavaco Silva na Mfalme wa Saudi Arabia, Muqrin bin
Abdulaziz Al-Saud, Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, Rais wa
Saharawi, Mohamed Abdelaziz, Waziri Mkuu wa Canada,
Stephen Harper wa Chad, Idriss Deby Itno, Rais wa
Serbia, Tomislav Nikolic, Makamu Rais wa China, Yuanchao, Rais wa
Shelisheli, James Alix Michel, Rais wa Comores, Dr Ikiliou Dhoinine na
Mfalme wa Hispania, Felipe de Borbon.
Rais wa Sri Lanka, Mahinda Rajapaksa, Makamu Rais
wa Sudan, Hassan Salih, Rais wa Suriname, Desire Delano Bouterse, Rais
wa Slovenia, Pahor, Rais wa Croatia, Josipovic Ivo, Rais wa Sudan
Kusini, Salva Kir Mayardit, Rais wa Cuba, Raul Castro Ruz, Rais wa
Djibouti, Ismail Omar Guelleh, Waziri Mkuu wa Swaziland, Dr Sibusiso
Dlamini, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Ato Hailemariam Dessalegn na Rais wa
Equatorial Guinea, Obiang Mbasogo.
SERIKALI YAJITENGA NA KESI YA UBAKAJI SOMALIA
Serikali ya Somalia imesema haiwezi kuhusishwa na kesi ya mwananamke ambaye amehukumiwa kifungo jela baada ya kusema kwamba alibakwa, ikisema hili ni suala la kisheria.Msemaji waserikali Ridwaan Haji amesema polisi na mahakama walifanya uchunguzi wa kina, ambao matokeo yake ni kuwa mwanamke huyo mwenye umri wa miaka kumi na tisa kuhukumiwa kifungo jela na waandishi wawili wa habari walioripoti habari hiyo nao pia wakahukumiwa.Mwananamke huyo ambaye amehukumiwa miezi sita kifungo cha nyumbani, atabakia nyumbani kwake kipindi chote hicho. Amesema alibakwa akiwa ameelekezewa bunduki na wanaume wawili.Sio mara ya kwanza kwa mwanamke Somalia kudai kuwa amebakwa.
SHAA AKIRI KUWA NA UHUSIANO WA KIMAPENZI NA MASTER JAY
Akihojiwa katika kipindi cha ng'ari ng'ari, Shaa alisema," mimi sikuwa sababu ya kuachana kwa wao wawili (Master Jay na mama watoto wake), kwani ugomvi au kuachana kwa watu wawili huwa inahusu wao wenyewe wawili ila sio mtu watatu, na kwakuwa mimi nilikuwa nimetoka kutendwa ilichukua muda kidogo hadi kuja kuwa na mahusiano na Master Jay hata yeye pia aliniambia alikuwa na maumivu yake ndio mana ilichukua muda hadi kuwa na mahusiano. Hivyo kwanini niachie bahati yangu, Nampenda sana Master"
BABY MADAHA ANUSIRIKA KUBAKWA
STAA wa filamu na muziki Bongo, Baby Joseph Madaha ‘Baby Madaha’ amenusurika kubakwa na vijana wa kihuni nchini Kenya maarufu kama machokoraa.Tukio hilo lilitokea pande za Mombasa nchini Kenya wakati nyota huyo alipokuwa akirekodi video ya wimbo wake uitwao The Gal Bladder ambapo vijana hao walikatisha shughuli nzima na kuanza kumkimbiza Baby Madaha.“Daah! Ilikuwa noma, ilikuwa usiku sasa wakati meneja wangu akinielekeza matakwa ya video hiyo ambayo yalihitaji vijana wa mtaani, ghafla wakatokea vijana wenyewe wa mtaani na kutaka kunibaka. Bahati nzuri nilifanikiwa kutimua mbio na kuwazidi,” alisema Baby.
WANAJESHI WAWAPOKONYA WAASI SILAHA AFRIKA YA KATI
Wanajeshi wa Ufaransa wameanza kuwapokonya silaha waasi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.Leo asubuhi makabiliano yalitokea kati ya wanajeshi hao na wapiganaji wa serikali mjini Bangui, wakati shughuli hiyo ilipoanza.Msemaji wa jeshi la Ufaransa, alisema kuwa wanajeshi waliwakamata wapiganaji kadhaa na kunasa silaha walizokuwa wanatumia.Kikosi cha wanajeshi 1,600, kimepelekwa nchini humo baada ya siku kadhaa za mapigano yaliyosababisha vifo vya watu 400.Kiongozi wa waasi, Michel Djotodia, aliingia mamlakani mwezi Machi kwa usaidizi wa wapiganaji wake ambao wengi wao ni waasi wa zamani. Djotodia amechukua mamlaka baada ya kumpindua aliyekuwa Rais Francois Bozize.Wanajeshi wa Ufaransa, sasa wanashika doria katika barabara na mitaa ya mji mkuu Bangui.Walikwenda Bangui siku ya Ijumaa baada ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuunga mkono azimio la kurejesha utulivu nchini humo kwa kutumia njia yoyote itakayofaa, hata kama ni kwa nguvu.Nyumba zimeharibiwa kwa maguruneti kufuatia makabiliano makali kati ya waasi hao na wanajeshi na pia kutokana na vita vya kidini ambavyo vimetokana na vurugu hizo.Wakati wa mapigano, mamia ya waumini wa kiisilamu walikimbilia katika nyumba ya Imamu mmoja ambako walikwenda kutafuta hifadhi.
MWANAMKE ALIYEDAI KUBAKWA AHUKUMIWA SOMALIA
Mahakama nchini Somalia, imemhukumu kifungo cha nyumbani mwanamke aliyedai kubakwa pamoja na waandishi wawili wa habari waliomhoji kuhusiana na madai hayo.Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 19, alipewa kifungo cha nje cha miezi sita kwa kile mahakama ilisema ni kutoa taarifa zisizokweli.Atalazimika kukaa nyumbani kwake bila kutoka nje kwa miezi sita.Mmoja wa waandishi wa habari, aliyemhoji mwanamke huyo naye alipewa kifungo cha nje cha mwaka mmoja huku mwenzake akipokea kifungo cha miezi sita.Waandishi hao wanafanya kazi na kituo cha redio Shabelle ambacho serikali ilifunga matangazo yake mwezi Oktoba baada ya polisi kuvamia ofisi zake.
GWIJI WA RHUMBA TABU LEY AZIKWA KINSHASA

Mazishi ya Gwiji wa Rumba nchini DRC, Tabu Ley Rochereau yalifanyika Jumatatu mjini Kinshasa.Mwili wake ukiwa ndani ya jeneza la rangi nyeupe lililotandwa bendera ya Jamhuri ya Congo, ulilazwa kwenye majengo ya Bunge ambako watu zaidi ya elfu kumi walifika kutoa heshima za mwisho kwa marehemu Pascal Sinamoyi Tabu Ley.Viongozi wa serikali ya DRC walihudhuria mazishi hayo huku waakilishi kutoka nchi jirani ya Congo Brazaville pia wakihudhuria mazishi hayo.
Tabu Ley alifariki mwezi Novemba akiwa na umri wa miaka 76 akipokea matibabu nchini Ubelgiji. Aidha gwiji huyo alikiri rasmi kwamba ana watoto 49. Lakini mwandishi wa BBC katika mazishi hayo Lubunga Byaombe, alisema kuwa zaidi ya watu 80 walijitokeza na kusema kuwa baba yao ni mwanamuziki huyo na kwamba wengi wao walitaka kupewa nafasi kuzungumza katika mazishi hayo.
Tabu ley aliyejulikana kama mfalme wa muziki wa rumba aliaga dunia mwezi uliopita mjini Brussels, Ubelgiji akiwa na miaka sabini na sita.Wengi walimkumbuka Tabu Ley kwa mziki wake na kwa talanta yake kwa utunzi wa nyimbo zake zilizowagusa watu wengi Afrika. Tabu Ley amefanyiwa mazishi ya kitaifa.
Mwanamziki huyo ambaye pia alikuwa mwanasiasa, hakuwahi kupona tangu alipougua kiharusi mwaka 2008 na hali yake iliendelea kuwa mbaya hadi alipofariki Novemba 30 mwaka huu. Alizaliwa mwaka 1937 katika kijiji kimoja kidogo Magharibi mwa mkoa wa Bandundu, na hapo ndipo nyota yake ilianza kung'aa a katika fani ya muziki wa Rumba mapema miaka ya sitini. Baadhi ya nyimbo alizoimba zilikuwa Adios Thethe na Mokolo nakokufa, na zilisaidia katika kufanya mziki wa Rumba kupendwa sana.
Tabu Lei alitaka sana kuwa waziri wa utamaduni katika serikali ya Laurent-Desire Kabila-babake Rais Joseph Kabila, lakini badala yake akawa naibu gavana wa mji wa Kinshasa. Alikimbilia usalama wake wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais Mobutu Sese Seko kati ya mwaka 1965-1997, na mnamo mwaka 1990, serikali ya Mobutu ikapiga marufu album yake Trop, c'est trop.
Chanzo: BBC
BUNGE LA AFRIKA KUSINI KUMUENZI MANDELA
Bunge nchini Afrika Kusini, leo linatarajiwa kuwa na kikao maalum cha kumkumbuka Nelson Mandela, huku viongozi duniani wakijiandaa kwa misa ya wafu itakayofanyika Jumanne.Kikao cha leo kinafanyika mwonzoni wa wiki ya shughuli mbali mbali za kumuenzi Mandela kabla ya mazishi yake tarehe 15 Disemba.Zaidi ya viongozi miamoja wa sasa na wa zamani wanatarajiwa kuhudhuria misa hiyo au mazishi mwishoni mwa wiki hii.Mnamo siku ya Jumapili, mamilioni ya wanachi walijitokeza kuhudhuria maombi maalum ya kumkumbuka Mandela aliyekuwa rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo.Kikao cha leo cha Bunge kitakuwa kikao maalum kwa ajili tu ya kumkumbuka Hayati Mandela.Mke wa zamani wa Mandela, Winnie Madikizela-Mandela na mjukuu wake Mandela Mandla, wote ni wabunge katika bunge la taifa, lakini haijulikani ikiwa watahudhuria kikao cha leo.Msemaji wa chama tawala, ANC, Moloto Mothapo amesema, anatumai kuwa baadhi ya jamaa za familia ya Mandela, watakuwepo bungeni.Rais wa zamani wa nchi hiyo, FW de Klerk, amealikwa kwa kikao hicho.
MAANDAMANO YAKITHIRI BANGKOK, THAILAND
Maelfu ya waandamanaji wanaopinga serikali wamefurika katika barabara za mji mkuu wa Thailand ,Bangkok licha ya serikali kutangaza uchaguzi wa mapema nchini humo.Waziri mkuu Yingluck Shinawatra alitoa taarifa katika Runinga kabla ya maandamano hayo kuanza na kusema kuwa analivunja bunge ili kuitisha uchaguzi mpya nchini humo hivi karibuni.Kiongozi wa maandamano hayo Suthep Thauksuban amesema kuwa ataendelea na vita hivyo na akawaambia waandamanaji kuwa wameshinda vita vikubwa dhidi ya serikali.Kiongozi huyo alikuwa amekataa kufanyika kwa uchaguzi mpya na badala yake anataka kubadilishwa kwa serikali hiyo na kile alichokitaja kama baraza la raia.Wabunge wote wa chama cha upinzani cha Demokrat walijiuzulu bungeni hapo jana.