VITAMBULISHO VYA URAIA KUVUKIA MIPAKA KENYA, RWANDA NA UGANDA
Wananchi wa mataifa ya Rwanda, Uganda na Kenya wamepokea kwa shangwe kuanza kwa mpango wa kutumiwa kwa vitambulisho vya uraia kama cheti cha kuwaruhusu kuvuka mpaka na kuingia moja wapo wa nchi hizo.Mpango huu wa kutumia vitambulisho vya uraia kama hati ya kusafiria katika nchi hizo tatu umeanza kutumiwa rasmi tarahe Mosi Januari 2014, kufuatia makubaliano kati ya viongozi wa mataifa hayo.Mpango wenyewe unatokana na makubaliano kati ya viongozi wa nchi tatu waliofikia wakati wa mkutano uliofanyika nchini Uganda mwezi Juni mwaka jana.Pia mpango huu unalenga kurahisisha usafiri wa watu wa jumuiya katika mataifa wanachama kama awamu ya pili ya ushirikiano kati ya mataifa wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki.Hata hivyo siku moja tu baada ya kuanzishwa kwa mpango wa kutumia vitambulisho vya uraia kama hati ya kuwaruhusu raia wa nchini tatu, Uganda, Kenya na Rwanda kuvuka mpaka na kuingia mojawapo ya nchi hizo sasa inaonekana mpango huo huenda ukawanufaisha watu wachache peke yake.Sio raia wote wa Uganda , Kenya au Rwanda wanafahamu hayo . Watu wengi nchini Rwanda bado waliwasili katika mipaka ya nchi hiyo wakiwa wamejihami kwa Pasipoti zao ili waweze kuruhusiwa kuvuka mpaka na kuingia katika nchi jirani. Hali ni vivyo hivyo nchini Uganda.Hata hivyo baadhi ya watu wanahisi ingekuwa vyema kama mpango huu pia ungewanufaisha raia wa Burundi na Tanzania.Kwa sasa ni raia wa Rwanda na Kenya peke yao ambao wana vitambulisho vya kitaifa ikimaanisha kuwa raia wa Uganda watalazimika kutumia kadi zao za kupigia kura hadi taifa hilo litakapoanza kutoa vitambulisho vya uraia.
Comments
Post a Comment