ACHINJWA KWA IMANI ZA KISHIRIKINA
MKAZI wa Kijiji cha Kakese-Mkwajuni, wilayani Mpanda, Shoma Salum (78) ameuawa kwa kuchinjwa kwa kile kinachodaiwa ni kutokana na imani za kishirikina.Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema mauaji hayo yalifanyika Desemba 29 , mwaka jana saa 2:30.Alikutwa nyumbani kwake mwili ukiwa na majeraha makubwa sikioni na kichwani. Mwanamke huyo inadaiwa alikuwa mganga wa kienyeji na mfinyanzi maarufu wa vyungu.Kwa mujibu wa Kamanda, siku moja kabla ya tukio, akiwa kwenye shughuli hizo, jirani na nyumbani kwake, walifika vijana wawili waliotajwa ni Shigela Majinja (25) na Mhoja Shilinde (18). Inadaiwa vijana hao ambao ni wakazi wa kijijini hapo.Walifika kwa kwa mama huyo wakijifanya kuwa ni wateja wake, ambapo walikuwa wakiulizia bei ya vyungu. Pia, walimwomba awasaidie kuwapatia tiba ya kienyeji .“Ndipo vijana hao walipoanza kumhoji juu ya mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutaka kujua mahali , alikokuwa akiishi na chumba alichokuwa akilala na alikuwa akilala na nani. Inadaiwa aliwajibu vijana hao kwa ufasaha bila kuwa na shaka nao huku mazungumzo hayo yakiwa yanasikilizwa kwa siri na Tausi Mlitoni, ambaye naye alikuwa karibu na eneo hilo ,” alisema Kamanda.Kwa mujibu wa Kamanda, Desemba 29 saa 2:30 asubuhi mke wa Lameck Mboka, aitwaye Zamda Militone, baada ya kuona mama mkwe amechelewa kuamka, alienda na kujaribu kufungua mlango wa chumba chake.Lakini, alibaini kuwa kilikuwa kimefungwa kwa nje. Kidavashari alisema Zamda alipofungua mlango huo wa chumba cha mama mkwe wake na kuingia ndani , alimkuta mama akiwa ameuawa.Kamanda alisema watu watatu wanashikiliwa kwa mahojiano, nao ni Majija, Shilinde na Masanja Ngasa (31), wote wakazi wa kijijini hapo. Watuhumiwa wengine wanne wanaendelea kusakwa baada ya kukimbia kusikojulikana.
Chanzo: Habari Leo
Comments
Post a Comment