EYMAEL: NIPENI YANGA NIIUE AL-AHLY
KOCHA Luc Eymael ambaye tayari ameshafanya mazungumzo ya awali na viongozi wa Yanga, ameuambia uongozi wa klabu hiyo kuwa anaijua vizuri Klabu ya Al-Ahly ya Misri na endapo watampatia kibarua hicho, atawasaidia kuwang’oa katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya mtandao, Eymael ambaye ni raia wa Ubelgiji, alisema amefanya mazungumzo ya awali na mmoja wa viongozi wa Yanga kupitia barua pepe, ambapo alisema kama klabu hiyo itampatia ajira hiyo hana wasiwasi na uwezo wake katika kuwang’oa Al-Ahly ambao Yanga inatarajia kukutana nao raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga itaanza michuano hiyo dhidi ya timu ya Comoronize ya Visiwa vya Comoro inayotajwa kuwa ni dhaifu na baada ya hapo itakuwa na kibarua kizito dhidi ya wababe hao wa Misri. Eymael aliyezaliwa miaka 54 iliyopita katika mji mdogo wa Tongeren, Ubelgiji alisema hajajua Yanga inaundwa na nyota wenye uwezo kiasi gani lakini anachoweza kuwaambia viongozi wa klabu hiyo ni kwamba anazijua timu nyingi hasa Wamisri hao ambao tayari wameshapata pigo kubwa kwa kuondokewa na nyota wao wawili muhimu akiwemo mkongwe Mohamed Aboutrika aliyetangaza kutundika daluga Desemba mwaka jana.
Eymael alisema tayari mezani kwake amepokea ofa mbili kutoka klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Algeria za CS Constantine na CR Belouizdad na amepanga kuzitupilia mbali kama Yanga watachangamka kuharakisha mazungumzo naye ya kumpa nafasi iliyoachwa na Ernest Brandts. Alisema kama Yanga watakuwa na nia ya kweli katika kumpa kibarua hicho anawapa mpaka mwisho wa wiki hii na kama hawatamtafuta katika muda huo ataingia katika mazungumzo ya kujiunga na Costantine ambayo inamtafuta kila wakati kupitia mwenyekiti wa klabu hiyo.
CS Constantine inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 48, katika ligi inayoongozwa na ES Setif yenye pointi 59, wakati Belouizdad inashika nafasi ya sita ikiwa na pointi 41, ambapo klabu zote zinamuwinda Mbelgiji huyo.
“Nilivyofuatilia Yanga ni timu nzuri, unajua nilikuwa Kenya na AFC Leopards na hadi sasa wananihitaji, sijui uwezo wa wachezaji wa Yanga na kuhusu akili zao na mbinu lakini kama watakuwa na ubora hakuna shida katika kushindana na hao Al Ahly,” alisema Eymael.
“Kama Yanga wana nia ya kweli waambie wanitafute mpaka kufikia mwisho wa wiki hii, wakichelewa baada ya muda huo nitaingia katika mazungumzo na hawa Constantine ambao wapo katika nafasi ya tatu kwenye ligi ya Algeria. Huenda mambo yakamnyookea Eymael kwa kuwa mpango wa Yanga kumpa ajira Bobby Williamson, kocha wa Gor Mahia umegonga mwamba baada ya kocha huyo kugoma kuja Tanzania na kubaki Kenya ingawa viongozi wa Yanga wamedai kuwa hawakati tamaa hadi kieleweke. Akizungumza na Mwanaspoti Bobby raia wa Scotland, alisema amezungumza na mwenyekiti wa Gor Mahia mara baada ya kusikia Yanga wanamhitaji.
Chanzo: Mwanaspoti
Comments
Post a Comment