WABUNGE: "BILA KILIMO KWANZA HAKUNA SERIKALI YA VIWANDA"
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamesema bila
kuwekeza katika kilimo, azima ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda
haitatimia.
Kadhalika, wameipongeza Serikali kwa kuondoa tozo 108 zilizokuwa kero
kwa wakulima na kuitaka Serikali kuhakikisha tozo zilizoondolewa
zinawanufaisha zaidi wakulima na Watanzania, badala ya kuwanufaisha
wafanyabiashara pekee. Waliyasema hayo jana kwa nyakati tofauti bungeni
Dodoma wakati wakichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na
matumizi ya bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa
Fedha 2017/18.
Mbunge wa Viti Maalum, Mariam Ditopile (CCM), alisema kama Tanzania
inataka kuwa ya viwanda, haina budi kuwekeza katika utafiti kwa ajili ya
sekta ya kilimo ili kubaini namna bora zaidi za kutumia rasilimali na
fursa zilizopo ili kuimarisha kilimo na hivyo kusaidia kufikia haraka
azima ya kujenga Tanzania ya viwanda. Alisema tayari fursa za kuinua
kilimo na kukifanya uti wa mgongo nchini zimeanza kuonekana kwani kwa
sasa Tanzania ndiyo inayouza vyakula na bidhaa za biashara katika nchi
mbalimbali duniani zikiwemo nchi za Sudan, Kenya na Uganda wanaonunua
mazao ya chakula kama mahindi.
“Nchi kama India inanunua kwetu korosho, choroko na tumbaku. Kwa sasa
mipango ni kuipeleka nchi kwenye viwanda ni wakati muafaka wa kuwekeza
kwenye kilimo kwa kufanya utafiti za kisayansi za namna bora ya
kuendeleza kilimo chetu kwa sababu kilimo ndio ajira, chakula na fedha,”
alisisitiza. Alisema Tanzania inasifika kwa kufanya utafiti, lakini
pamoja na kuwa na uwezo huo bado haujatumika vizuri kuendeleza mambo ya
msingi yakiwamo maeneo ya kilimo, mifugo na uvuvi.
“Kwa mfano sisi ndio wenye eneo kubwa katika Ziwa Victoria, lakini
takwimu za kidunia zinaonesha Uganda yenye sehemu ndogo katika ziwa hilo
ndiyo inayoshika nafasi ya juu; ya sita duniani kwa uvuvi huku sisi
Tanzania tukishika nafasi ya nane,” alisema. Mbunge wa Mbinga Mjini,
Sixtus Mapunda (CCM) aliitaka serikali iwekeze kwenye utafiti wa kilimo
ili kuyabaini maeneo ya kijiografia na kisayansi yanayoweza kuikuza kwa
kasi sekta hiyo ya kilimo inayokwenda sambamba na sekta ya viwanda.
“Kwa mfano Morogoro ina udongo wenye rutuba na mito inayotiririsha
maji kwa mwaka mzima, utafiti ukifanyika wa namna bora ya kutumia
rasilimali hizo, ni wazi kuwa Morogoro pekee inaweza kulisha Tanzania
nzima,” alisema. Pamoja na hayo mbunge huyo alisema si kweli utitiri wa
kodi zilizofutwa na serikali umewalenga zaidi wafanyabiashara na wenye
kampuni na si wakulima kwa kuwa wafanyabiashara na kampuni hizo kutokana
na kufutwa kwa tozo hizo kuanzia sasa watanunua mazao na bidhaa hiyo
kwa bei inayostahili.
Kwa upande wake Mbunge wa Hanang, Mary Nagu (CCM), alisema serikali
haina budi kuzingatia kuwa kilimo ndicho kinachochangia ajira kwa
Watanzania takribani asilimia 65, kinachozalisha chakula kwa Watanzania
kwa asilimia 100 na kuingiza asilimia 28 katika pato la taifa. “Hii ni
sekta muhimu sana, ni vema Serikali ione umuhimu wa kuifanyia mageuzi
sekta ya kilimo na kuongeza bajeti ya wizara ya kilimo kwani hali ilivyo
sasa badala ya kilimo kukua, kinashuka kwa kasi,”alisema.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2011 kilimo kilikuwa kwa
wastani wa asilimia 3.5 lakini miaka sita baadaye yaani mwaka2016 kilimo
hicho kilishuka na ukuaji wake kufikia asilimia 1.7 hali inayozidisha
umasikini kwa Watanzania,” alisema Dk Nagu. Alisema pamoja na ukuaji wa
kilimo pia bajeti ya Wizara ya Kilimo imekuwa ilishuka badala ya kupanda
kila mwaka kwani mwaka 2011 bajeti ya Wizara hiyo ilikuwa asilimia 7.8
ya bajeti nzima ya Serikali, lakini katika bajeti ya mwaka 2016, bajeti
ya Wizara hiyo ilishuka na kufikia asilimia 4.9.
Nagu aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika
Serikali ya Awamu ya Nne, kupongeza hatua ya Serikali kuondoa utitiri wa
kodi zenye kero kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, aliitaka
Serikali ihakikishe kuwa hatua hiyo inawanufaisha zaidi wakulima,
wafugaji na wavuvi na si kwa wafanyabiashara.
Kwa upande wake mbunge wa Malindi, Ally Saleh (CUF) aliishauri
serikali iwekeze zaidi kwenye fikra za kuleta mabadiliko ya kilimo,
mifugo na uvuvi kutokana na ukweli kuwa Tanzania imebarikiwa rasilimali
kama vile maziwa, mito, bahari na mikoa yenye rutuba ambayo endapo
itatumiwa vema itakuza sekta hizo.
“Sasa hivi tuna tatizo gani, badala ya kilimo kwenda mbele kinashuka.
Leo hii haiwezekani sisi tunaongoza kwa kuwa na ng’ombe wengi kuliko
Kenya, lakini wao wanatuzidi kwa kuzalisha maziwa. Tunahitaji fikra
mpya,” alisema. Alisema Tanzania kuna hekta takribani milioni 13.5
zinazolimika na hekta milioni 1.5 za mikoko, pia ni nchi ya tatu Afrika
lakini pia nchi ya 11 duniani kwa kuwa na wingi wa mifugo, lakini bado
rasilimali hizo haijatumiwa vizuri.
Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema), aliishauri Serikali iwekeze
zaidi katika kilimo kupitia mbolea ya uhakika, dawa za mimea, masoko na
miundombinu bora kwa kuwa huo ndio usalama wa watanzania katika
chakula.
Chanzo: Habari Leo
Comments
Post a Comment