| | KATIBU Mkuu wa klabu ya Yanga, Jonas Tiboroha amekiri kuondoka kwa mshambuliaji Mrisho Ngassa ni pengo kubwa kwa timu yao, lakini amewataka mashabiki na wanachama wa timu hiyo kuhakikisha wanapambana kumbakiza kiungo Haruna Niyonzima. |
| Tiboroha alisema ana uhakika watafikia makubaliano na kiungo huyo bora Afrika Mashariki katika siku chache zijazo ili aendelee kuichezea timu yao msimu ujao na kwa kushirikiana na nyota wengine waliopo na watakaowasajili. |
| Akizungumza na gazeti hili jana, Tiboroha alisema itakuwa wamefanya kosa kubwa endapo watamruhusu nyota huyo kuondoka kwani itakuwa ni pengo jingine baada ya Ngassa kuhamia Free State ya Afrika Kusini kwa mkataba wa miaka minne. |
| “Bado tupo kwenye mazungumzo na imani yangu kama Katibu Mkuu wa Yanga ni kwamba msimu ujao Niyonzima atabaki kuichezea Yanga kwa sababu mazungumzo yapo kwenye hatua nzuri na hata yeye mwenyewe ameonekana kutaka kubaki,” alisema Tiboroha. |
| Kiongozi huyo alisema wamekuwa na vikao virefu na viongozi wa juu wa Yanga kwa ajili ya kujadili suala la mchezaji huyo kwa lengo la kumalizana naye kwa kumpa kile alichowaomba kumboreshea katika usajili wake mpya na viongozi wamelipokea na kuahidi kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo. |
| “Sidhani kama kuna kitakachoshindikana kwa sababu pande zote mbili zimeonekana kuelekea kuelewana na kizuri ni kwamba Niyonzima mwenyewe ameonyesha nia ya kutaka kuendelea kubaki Yanga endapo tutamboreshea maslahi yake aliyoyahitaji kwenye mkataba mpya,” alisema. |
| Alisema mbali na Niyonzima pia wanatarajia kuanza mazungumzo na wachezaji wao wengine waliomaliza mikataba yao ambao wangependa kuendelea nao msimu ujao ili kuwapa mikataba mipya. |
| Tiboroha alisema baada ya kuondoka kwa Ngassa kocha wao Hans van der Pluijm, aliwataka kufanya kila linalowezekana nyota hao kuwabakisha kwenye kikosi hicho ili kikosi chake kisipoteze uwezo wa kutetea ubingwa wao msimu ujao. |
| “Kocha Pluijm ametushauri kuhakikisha tunawabakiza baadhi ya nyota wetu waliomaliza muda wao akiwemo Mbuyu Twite, makipa Ally Mustapha ‘Barthez’ Deogratius Munishi ‘Dida’ na Kelvin Yondani ili asipate tabu ya kuanza kujenga upya timu yake na kupata tabu katika mbio za kutetea ubingwa wake,” alisema Tiboroha. |
| Niyonzima ameonekana kuitikisa klabu ya Yanga akitaka wampe dola 50,000 kama pesa ya usajili ili kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea timu hiyo kwa miaka mingine miwili. |
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Comments
Post a Comment