HABARI LEO TAHARIRI: TFF IFANYIE KAZI KASORO ZA MSIMU ULIOMALIZIKA

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara umemalizika Jumamosi iliyopita, huku timu za Polisi Morogoro na Ruvu Shooting ya mkoani Pwani zikishuka daraja.

Kushuka kwa timu hizo mbili kunatoa nafasi kwa timu nne kupanda daraja kukiwa na lengo la kuongeza timu shiriki kutoka 14 hadi 16 katika msimu ujao wa ligi hiyo.

Timu zilizopanda daraja ni Majimaji ya Songea, African Sports ya Tanga, Toto African ya Mwanza na Mwadui ya Shinyanga, ambazo zinakamilisha timu hizo nne.

Wakati msimu huo wa ligi ukifungwa, tayari Yanga na Azam FC walishajitangazia nafasi za kwanza na pili na kuwa na uhakika wa kuliwakilisha taifa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa na ile ya Shirikisho la Afrika.

Baada ya kumalizika kwa msimu huu wa ligi ndio mwanzo wa msimu unaokuja na timu zinatakiwa kujipanga vizuri kwa ajili ya msimu huo, ambao kama baadhi ya makosa yatarekebishwa, inaweza kuwa ligi bora zaidi.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), timu pamoja na wadau wengine wa ligi hiyo kama kamati mbalimbali, ambazo kwa njia moja ama nyingine zinahusika katika kuendesha ligi hiyo, zinatakiwa kufanya tathmini kwa yale yaliyopita.

Hakuna ubishi kuwa pamoja na kutojali uwezo wa kifedha, timu zilijitahidi sana hata zile ambazo hazina majina makubwa zilifanya vizuri uwanjani na kuvitoa jasho vigogo.

Lakini pamoja na uzuri wa msimu huo, bado kuna changamoto kibao zilizojitokeza, ambazo kwa kiasi fulani zilitia doa ligi hiyo, ambayo angalau ilikuwa na wadhamini waliosaidia timu kutoa lia njaa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

TFF wakati umefika sasa wa kuwa makini wakati wa upangaji wa ratiba na lazima mzingatie mazingira ya mikoa pamoja na miundo mbinu ya nchi yetu, ili kuziwezesha timu kucheza mechi zao bila tatizo.

Timu nyingi zililalamikia ratiba ambayo haikuwa rafiki kwani utakuta timu inacheza mchezo mmoja katika mkoa fulani ambao una timu zaidi ya moja halafu inaondoka na kurudi tena baadaye na kuzisababishia usumbufu na gharama zisizo za lazima.

Mfano mkoa wa Mbeya una timu mbili, hivyo timu ilitakiwa angalau inapokwenda icheze mechi zote mbili na ndipo iende mahali pengine ili iweze kubana matumizi na kutumia muda vizuri.

Mbali na kasoro hiyo ya upangaji mbovu wa ratiba, pia kulikuwa na kasoro zingine kama baadhi ya waamuzi kuchezesha ama kwa upendeleo au chini ya kiwango kwa kutojua sheria 17 za soka, ambazo ni muhimu.

Timu nyingi hasa zile ndogo zililalamikia sana waamuzi na wengi walidai kuwa walikuwa wakiumwa kwa makusudi ili kuzibeba timu kubwa na kuzipatia matokeo mazuri kwao.

TFF na wadau wengine wote wanatakiwa kujifunza kutokana na makosa ya msimu uliopita ili kuuboresha msimu ujao na kuifanya Ligi Kuu Bara kuwa ligi bora zaidi.

Ligi bora hutoa timu bora ya taifa, hilo halina ubishi, hivyo ni jukumu la TFF kuhakikisha ligi inakuwa bora ili kupata timu bora ya taifa itakayofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Chanzo: Kutoka Bodi ya Uhariri Gazeti la Habari Leo.

Comments

Popular Posts

MKUTAO WA G7 KUANGAZIA USALAMA NA MAZINGIRA

CHEKI PICHA HIZI ALIZOWEKA NICKI MINAJ INSTAGRAM

ZIFAHAMU NCHI ZINAZOZUNGUMZA KISWAHILI BARANI AFRIKA

WAFAHAMU WAIGIZAJI 10 WA KIUME WENYE MVUTO KOREA 2017

HISTORIA YA KOMBE LA DUNIA TANGU 1930, WAANDAAJI & WASHINDI

WAFAHAMU WAIGIZAJI 10 WA KIKE WA KOREA AMBAO NI WAREMBO KWA MWAKA 2017

BIBI WA MIAKA 85 AKAMATWA KWA KUIBA HERENI

MAMBO YA MUHIMU KUFAHAMU NA KUZINGATIA KABLA YA KUCHAGUA KOZI (TAALUMA) CHUO KIKUU

WAFAHAMU MATAJIRI 10 WA TANZANIA MWAKA 2018