Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF, limesema mwaka 2017 ulikuwa miongoni mwa miaka mibaya zaidi kwa watoto wanaoishi katika maeneo ya vita na mizozo duniani. Ripoti ya shirika hilo la UNICEF imesema pande zinazozozana katika vita duniani zilikiuka wazi wazi sheria za kimataifa linapokuja suala la kuwalinda watozo. Mkurugenzi wa UNICEF kuhusu mipango ya dharura Manuel Fontaine amesema watoto walilengwa na kuwekwa katika hatari ya mashambulizi wakiwa nyumbani, shuleni na wakicheza. Fontaine ameongeza kusema ulimwengu haupaswi kuyafumbia macho mashambulizi haya akisisitiza maovu dhidi ya watoto hayapaswi kuwa matukio ya kawaida katika ulimwengu wa sasa. Maovu dhidi ya Watoto ni makubwa Watoto katika mataifa yanayoshuhudia vita wamekuwa waathirika wakubwa wakiuawa, kulemazwa, kusajiliwa kwa lazima kuwa wapiganaji, kuolewa kwa lazima, kutekwa nyara, kutumikishwa na kubakwa. Wapiganaji watoto wa Sudan Kusini. Wengi wa watot...