UNICEF: WATOTO WALISHAMBULIWA KWA KIWANGO KIKUBWA SANA MWAKA 2017
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF, limesema
mwaka 2017 ulikuwa miongoni mwa miaka mibaya zaidi kwa watoto wanaoishi katika
maeneo ya vita na mizozo duniani.
Ripoti ya shirika hilo la UNICEF imesema pande zinazozozana katika vita
duniani zilikiuka wazi wazi sheria za kimataifa linapokuja suala la
kuwalinda watozo. Mkurugenzi wa UNICEF kuhusu mipango ya dharura Manuel
Fontaine amesema watoto walilengwa na kuwekwa katika hatari ya
mashambulizi wakiwa nyumbani, shuleni na wakicheza.
Fontaine
ameongeza kusema ulimwengu haupaswi kuyafumbia macho mashambulizi haya
akisisitiza maovu dhidi ya watoto hayapaswi kuwa matukio ya kawaida
katika ulimwengu wa sasa.
Maovu dhidi ya Watoto ni makubwa
Watoto
katika mataifa yanayoshuhudia vita wamekuwa waathirika wakubwa
wakiuawa, kulemazwa, kusajiliwa kwa lazima kuwa wapiganaji, kuolewa kwa
lazima, kutekwa nyara, kutumikishwa na kubakwa.
Wapiganaji watoto wa Sudan Kusini. |
Wengi wa watoto hao wanaathirika katika mataifa ya Syria, Yemen,
Nigeria, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Myanmar.
Mamilioni ya watoto wengine wanakumbwa na utapia mlo, magonjwa, msongo
wa mawazo na kukosa mahitaji ya kimsingi kama chakula, maji, na huduma
za afya.
Ripoti hiyo ya shirika la Umoja wa Mataifa la
kuwashughulikia watoto limetoa takwimu kuhusu jimbo la Kasai katika
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako ghasia zimesababisha takriban
watoto 850,000 kuyahama makazi yao na wengine 350,000 kukumbwa na utapia
mlo mbaya. Shule 400 nchini Congo zilishambuliwa kimakusudi.
Nchini
Nigeria na Cameroon, waasi wa kundi la Boko Haram waliwatumia kiasi ya
watoto 135 kama washambuliaji wa kujitoa muhanga kwa mabomu, hiyo ikiwa
mara tano ya idadi ya watoto waliotumika na waasi hao mwaka jana.
Wengi wanakumbwa na utapia mlo
Sudan Kusini, zaidi ya watoto 19,000 wamesajiliwa kwa lazima kuwa wapiganaji kuanzia mapigano yalipozuka nchini humo mwaka 2013.
Nchini Yemen, vita vilivyozuka mwezi Machi mwaka 2015 vimesababisha
watozo 5,000 kupoteza maisha yao au kujeruhiwa, huku idadi kamili
ikihofiwa kuwa hata juu ya hiyo. Uhaba mkubwa wa chakula nchini humo
umesababisha takriban watoto milioni mbili kukumbwa na utapia mlo mbaya.
Mtoto anayesumbuliwa na utapiamlo nchini Yemen. |
Nchini
Iraq na Syria, takribani watoto 700 wameuawa mwaka huu na UNICEF
imeripoti kuwa katika baadhi ya visa watoto nchini humo walitumika kama
ngao vitani. Zaidi ya watoto milioni 11 wanahitaji kwa dharura misaada
ya kibinadamu.
Ripoti hiyo ya UNICEF inalenga kuufanya ulimwengu
kuangazia masaibu wanayopitia watoto walioko katika maeneo ya mizozo
duniani na Jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kuwalinda watoto.
MAKALA HII IMELETWA KWAKO KWA HISANI YA DW.
Comments
Post a Comment