MAJARIBIO KATI YA ChatGPT, BING CHAT NA GOOGLE BARD

Maendeleo ya teknolojia ya Akili Bandia (AI) yamebadilisha jinsi tunavyofanya kazi na mambo mengine mengi katika miezi ya hivi karibuni na hivyo kumpa karibu mtu yeyote uwezo wa kuandika msimbo (code), kuunda sanaa na hata kuwekeza.

Kwa watumiaji wa kitaalamu na wale wenye mapenzi na teknolojia, programu zalishi za AI, kama vile ChatGPT, huangazia uwezo wa hali ya juu ili kuunda maudhui yenye ubora kutokana na maelezo rahisi anayotoa mtumiaji.

Microsoft imeongeza GPT-4 katika Bing, OpenAI inaongeza uwezo mpya kwenye ChatGPT na Bard inaunganisha kwenye mfumo mzima wa Google yani kwamba chochote kinachoweza kupatikana kupitia Google utakipata kwenye Bard pia. Uwepo wa robotisogozi hizi 3 za hivi punde za AI kunaweza kumtatanisha mtumiaji ipi inamfaa zaidi.

Kujua ipi kati ya robotisogozi tatu maarufu za AI ni bora kuandika msimbo, kutoa maandishi, au kusaidia kuunda wasifu ni changamoto, kwa hivyo nakueleza hapa tofauti kubwa zaidi ili uweze kuchagua inayolingana na mahitaji yako kwa wakati huo.

Majaribio kati ya ChatGPT, Bing Chat & Google Bard
Ili kubaini ni robotisogozi gani la AI linatoa majibu sahihi zaidi, tutatumia swali hili kuzilinganisha zote hizi tatu:
"Nina machungwa 5 leo, nilikula machungwa 3 wiki iliyopita. Nimebakiza machungwa mangapi?"
Jibu linapaswa kuwa tano, kwani idadi ya machungwa niliyokula wiki iliyopita haiathiri idadi ya machungwa niliyonayo leo. Tuangalie majibu ya robotisogozi hizi.

Tuanze na ChatGPT

Unapaswa kutumia ChatGPT kama:

1. Unataka kujaribu robotisogozi maarufu ya AI
ChatGPT iliyoundwa na OpenAI ililenea Novemba mwaka jana baada ya kuzinduliwa rasmi. Tangu wakati huo, robotisogozi hii imepata watumiaji zaidi ya milioni 100, na tovuti pekee ikishuhudia watembeleaji wapatao bilioni 1.8 kwa mwezi. Imekuwa ikighubikwa na shutuma mbalimbali hasa watu wanapoifichua uwezo wake wa kufanya kazi za vyuoni na kuchukua nafasi ya wafanyikazi wengine.
Toleo lisilolipishwa la ChatGPT, ambalo linatumia mfumo wa GPT-3.5, lilitoa jibu lisilo sahihi kwa swali letu.

Nimekuwa nikijaribu ChatGPT mara kwa mara tangu kutolewa kwake. Muonekano wake kwa mtumiaji umebaki kuwa rahisi, lakini mabadiliko madogo yameiboresha zaidi, kama vile kuongezwa kwa kitufe cha kunakili, uwezo wa kuhariri, maelekezo maalum na ufikiaji rahisi wa akaunti yako.

Ingawa ChatGPT imejidhihirisha kama app muhimu ya AI, inaweza kukabiliwa na habari potofu. Kama mifumo mingine mikubwa ya lugha (LLMs), GPT-3.5 si kamilifu bado kwani imefunzwa kuhusu taarifa iliyoundwa na binadamu hadi 2021. Pia mara nyingi inashindwa kuelewa nuances, kama vile katika mfano wa swali letu la hesabu ambapo ilijibu vibaya kwa kusema tuna machungwa mawili yaliyobaki wakati inapaswa kuwa matano.

2. Uko tayari kulipa ziada kwa ajili ya kutumia toleo la juu zaidi
OpenAI huruhusu watumiaji kufikia ChatGPT inayoendeshwa na mfumo wa GPT-3.5 bila malipo kwa akaunti iliyosajiliwa. Lakini ikiwa uko tayari kulipia toleo la juu zaidi, unaweza kufikia GPT-4 kwa kulipia $20 kwa mwezi.

GPT-4 ndiyo LLM kubwa zaidi inayopatikana kwa matumizi ikilinganishwa na robotisogozi nyingine zote za AI na imefunzwa kwa taarifa za hadi 2022. Inasemekana kuwa GPT-4 ina zaidi ya maingizo trilioni 100 wakati GPT-3.5 ina maingizo bilioni 175. Maingizo zaidi inamaanisha kwamba kimsingi, mfumo umefunzwa kwa taarifa zaidi, ambayo inafanya uwezekano mkubwa wa kujibu maswali kwa usahihi.
ChatGPT Plus, inayotumia mfumo wa GPT-4, ilijibu swali kwa usahihi.

Kwa mfano, unaweza kuona mfano wa GPT-4, unaopatikana kwa kulipia toleo la juu la ChatGPT, ulijibu swali la hesabu kwa usahihi, kwani ulielewa muktadha kamili wa hesabu hiyo tangu mwanzo hadi mwisho.

Hebu sasa tuiangalie Bing Chat, ambayo ni njia nzuri ya kufikia GPT-4 bila malipo, kwani imeunganishwa katika toleo lake jipya la Bing.

Unapaswa kutumia Bing Chat ikiwa:

1. Unataka AI zalishi inayofikiwa kwa mtandao
Tofauti na ChatGPT ambayo inadhibitiwa kuwa programu ya AI ambayo hutoa maandishi kwa mtindo wa mazungumzo na habari hadi kufikia 2021. Bing sasa ina chaguo la gumzo ambalo linapangilia matokeo ya utafutaji kama mazungumzo na robotisogozi ya AI.

Kuna faida nyingine, pia. Bing Chat inaendeshwa na GPT-4, mfumo mkubwa wa lugha wa OpenAI na ni bure kabisa kutumia.
Mtindo sahihi wa mazungumzo ya Bing ulijibu swali kwa usahihi, ingawa mitindo mingine ilikuwa na utata. 

Muonekano wa mtumiaji wa Bing Chat si wa kupendeza sana kama cha ChatGPT, lakini ni rahisi kutumia.

Ingawa Bing Chat inatumika kwa kuunanisha na mtandao ili kukupa matokeo ya kisasa zaidi ikilinganishwa na ChatGPT, ina uwezekano mkubwa wa kukwama katika kujibu na kukosa vidokezo kuliko mshindani wake.

2. Unapendelea vipengele zaidi vya kuona
Kupitia mfululizo wa matoleo kwenye jukwaa lake, Microsoft iliongeza vipengele vya kuona kwenye Bing Chat. Kwa wakati huu, unaweza kuuliza maswali ya Bing kama, 'Shetani wa Tasmania ni nini?' na upate maelezo inayojibu kwa picha, muda wa kuishi, chakula, na zaidi kwa matokeo ya kuchanganua zaidi ambayo ni rahisi kuchimba kuliko ukuta wa maandishi.

Unapotumia Bing katika muundo wa gumzo, unaweza pia kuiomba ikutengenezee picha. Andika maelezo ya jinsi unavyotaka picha ionekane, na kisha acha Bing ikutengenezee picha nne ambapo utachagua uipendayo.

Bing Chat pia huangazia mitindo tofauti ya mazungumzo unapokuwa unaitumia ikijumuisha Ubunifu (Creative), Uwiano (Balanced) na Usahihi (Precise), ambayo hubadilisha jinsi utumiaji ulivyo, mwepesi au wa moja kwa moja.
Mitindo yote miwili ya mazungumzo ya Usawazishaji (Balanced ) na Ubunifu (Creative ) ilijibu swali isivyo sahihi.

Hatimaye, hebu tugeukie Google Bard, ambayo inatumia LLM tofauti na imekuwa matoleo mengi katika miezi michache iliyopita.

Unapaswa kutumia Google Bard ikiwa:

1. Unataka uzoefu wa haraka na usio na kikomo
Katika wakati wa kujaribu robotisogozi tofauti za AI, nimeona Google Bard ikipata dosari nyingi kwa mapungufu tofauti. Ingawa sitasema kuwa sio za kuzingatia sana, nitasema kuwa robotisogozi la AI ya Google lina mazuri yake na mojawapo ni kasi.

Google Bard ina kasi na majibu yake, hata kama inajibu kwa makosa baadhi ya nyakati. Haina kasi zaidi kuliko ChatGPT Plus, lakini inaweza kuwa haraka zaidi katika kutoa majibu kuliko Bing na toleo lisilolipishwa la GPT-3.5 la ChatGPT, ingawa umbali wako unaweza kutofautiana.
Bard pia alipata jibu lisilo sahihi katika swali hili.

Bard ilifanya makosa sawa na roboti zingine kwa kutumia kanuni isiyo sahihi ya 5 - 3 = 2.

Bard pia haizuiliwi na idadi fulani ya majibu kama vile Bing Chat ilivyo. Unaweza kuwa na mazungumzo marefu na Google Bard, lakini Bing ina kikomo cha majibu 30 katika mazungumzo moja. Hata ChatGPT Plus huwawekea watumiaji kikomo cha jumbe 50 kila baada ya saa tatu.

2. Unataka matumizi zaidi ya 'Google'
Google ilitangaza maboresho mengi ya AI wakati wa mkutano wake wa I/O miezi michache iliyopita pamoja na jinsi inavyopanga kuiboresha Bard na injini yake ya utafutaji. Tangu wakati huo Bard imepata toleo jipya la PaLM 2, toleo la hivi punde na kubwa zaidi la Google LLM, ambalo lilitangazwa wakati wa hafla ya Mei.

PaLM 2 ilisaidia Bard kutumia zaidi ya lugha 100 kwa wakati, na pia kuboresha pakubwa ujuzi wake wa usimbaji (coding), utatuzi (debugging) na hesabu. Kwa wakati huu, hata hivyo, ChatGPT inasemekana kutumia zaidi ya lugha 80.

Google pia ilijumuisha vipengele vingi vya kuona kwenye jukwaa lake la Bard kuliko vile vinavyopatikana kwenye Bing Chat. Google iliamua kwamba watumiaji wanaweza kupakia picha kupitia Google Lens na utengenezaji wa picha kupitia Adobe Firefly (ingawa bado uamuzi huu haujajumuishwa) pamoja na programu jalizi za Kayak, OpenTable, Instacart, na Wolfram Alpha.


MAKALA HII IMEANDIKWA NA MARIA DIAZ KATIKA TOVUTI YA ZDNET NA KUSIMULIWA KWA KISWAHILI NA VENANCE GILBERT.

Comments

Popular Posts

CHEKI PICHA HIZI ALIZOWEKA NICKI MINAJ INSTAGRAM

MKUTAO WA G7 KUANGAZIA USALAMA NA MAZINGIRA

ZIFAHAMU NCHI ZINAZOZUNGUMZA KISWAHILI BARANI AFRIKA

WAFAHAMU WAIGIZAJI 10 WA KIKE WA KOREA AMBAO NI WAREMBO KWA MWAKA 2017

WAFAHAMU WAIGIZAJI 10 WA KIUME WENYE MVUTO KOREA 2017

HISTORIA YA KOMBE LA DUNIA TANGU 1930, WAANDAAJI & WASHINDI

WALIOCHAGULIWA CHUO CHA MIPANGO MAJINA HAYA HAPA

BIBI WA MIAKA 85 AKAMATWA KWA KUIBA HERENI

MAMBO YA MUHIMU KUFAHAMU NA KUZINGATIA KABLA YA KUCHAGUA KOZI (TAALUMA) CHUO KIKUU