DIRISHA LA UFADHILI WA MASOMO "SAMIA SCHOLARSHIP" 2023/2014 LIMEFUNGULIWA
TANGAZO LA SAMIA SCHOLARSHIP MWAKA 2023/2024
UFADHILI KUPITIA SAMIA SCHOLARSHIP KWA WAHITIMU WENYE UFAULU WA JUU KATIKA MITIHANI YA KIDATO CHA SITA MWAKA 2023 KATIKA TAHASUSI ZA SAYANSI
1.0 UTANGULIZI
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatangaza programu ya Ufadhili iitwayo SAMIA SCHOLARSHIP kwa masomo ya shahada ya kwanza kwa wanafunzi waliopata ufaulu wa juu katika mitihani ya Kidato cha Sita mwaka 2023 iliyoendeshwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) katika Tahasusi za Sayansi (PCB, PCM, PGM, CBG, CBA, PMC na CBN).
SAMIA SCHOLARSHIP itagharamia kwa asilimia mia moja (100%) masomo ya Elimu ya Juu kwa wanafunzi hao ambao wamepata udahili katika fani za Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba.
2.0 SIFA ZA KUPATA UFADHILI
Ufadhili huu utatolewa kwa wahitimu wa kidato cha sita wenye sifa zifuatazo:
1. Awe Mtanzania;
2. Awe na ufaulu wa juu kwenye mitihani ya taifa ya kidato cha sita mwaka 2023 iliyoendeshwa na NECTA katika tahasusi za sayansi;
3. Awe amepata udahili katika Chuo cha Elimu ya Juu hapa nchini kinachotambuliwa na Serikali katika programu za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati au Tiba ambazo zimetajwa katika kundi la kwanza (Cluster 1) katika Mwongozo wa utoaji mikopo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka 2023/2024 unaopatikana kupitia www.heslb.go.tz
4. Awe ameomba ufadhili kwa usahihi kwa njia iliyoelekezwa.
3.0 MAENEO YA UFADHILI
Ufadhili utazingatia viwango na miongozo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ya kugharamia maeneo yafuatayo:
a. Ada ya Mafunzo
b. Posho ya chakula na malazi
c. Posho ya Vitabu na Viandikwa
d. Mahitaji Maalum ya Vitivo
e. Mafunzo kwa Vitendo
f. Utafiti
g. Vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu
h. Bima ya Afya
4.0 MUDA WA UFADHILI
Wanafunzi watakaofadhiliwa, watagharimiwa kati ya miaka mitatu (03) hadi mitano (05) kulingana na programu husika walizodahiliwa.
5.0 UTARATIBU WA KUOMBA UFADHILI
Maombi ya Samia Scholarship yatawasilishwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa njia ya mtandao https://olas.heslb.go.tz kwa siku 14 kuanzia Septemba 25, 2023
6.0 WAJIBU/MASHARTI YA UFADHILI
Mwanafunzi atakayepata ufadhili wa SAMIA SCHOLARSHIP atawajibika kuzingatia masharti yafuatayo:
a. Anapaswa kusoma, kuelewa na kusaini Mkataba wa Makubaliano ya Ufadhili wa Masomo kati yake na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia;
b. Anapaswa kuwa na akaunti ya Benki kwa ajili ya fedha atakazolipwa moja kwa moja.
c. Mnufaika hataruhusiwa kubadilisha programu ya masomo aliyopatia ufadhili bila barua ya idhini ya maandishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia;
d. Mnufaika hataruhusiwa kuahirisha masomo, isipokuwa kwa sababu za kiafya, na kuthibitishwa na chuo husika;
e. Ikiwa mnufaika ataghairi fursa ya ufadhili kabla ya kuanza masomo, atapaswa kuwasilisha taarifa ya maandishi kwenda kwa:
Katibu Mkuu,
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Mji wa Serikali Eneo la Mtumba Mtaa wa Afya,
S.L.P 10,
40479 DODOMA, TANZANIA.
Barua pepe: ps@moe.go.tz
f. Iwapo kiwango cha ufaulu wa mnufaika kitashuka chini ya GPA 3.8 katika mwaka wa masomo, ufadhili utasitishwa;
g. Mnufaika anapaswa kujisajili katika Mfumo wa Usimamizi wa Wanafunzi (Students Management System) unaopatikana kupitia https://scholarships.moe.go.tz/
MUHIMU KUZINGATIA
a. Ufadhili huu ni wa asilimia mia moja ambao kikomo chake kitazingatia miongozo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
b. Orodha ya majina ya wanafunzi husika inapatikana kupitia www.moe.go.tz na www.heslb.go.tz
Imetolewa na:
Comments
Post a Comment