MFAHAMU WOLE SOYINKA GWIJI WA FASIHI YA KIAFRIKA MWENYE TUZO YA NOBEL KATIKA FASIHI 1986
Picha kwa hisani ya Oasis Magazine |
Bila shaka jina la Wole Soyinka sio geni masikioni mwako kwa sababu wengi wetu tumesoma tamthiliya (play) yake ya The Lion and The Jewel sekondari hasa kidato cha tatu na cha nne na The Trials of Brother Jero kwa wale waliosoma miaka ya nyuma.
Hapa nitamzungumzia Wole Soyinka, mwafrika wa kwanza kushinda tuzo ya Nobel katika fasihi. Haya ni mambo ambayo huwezi kufundishwa kwenye mitaala ya shuleni, hivyo unapaswa kuyafahamu nje ya mtaala wa shule kwa muda wako mwenyewe. Awali ya yote, ni kwamba wasifu huu niliuandika kwa mara ya kwanza katika mtandao wa Twitter Julai 13, 2020 kabla sijaamua kuuleta hapa.
MAISHA YA MWANZO
Soyinka alizaliwa Julai 13, 1934 huko Abeokuta jirani na Ibadan nchini Naijeria. Majina yake halisi ni Akinwande Oluwole Babatunde Soyinka lakini anafahamika sana kama Wole Soyinka. Alisoma Fasihi, Ibadan. Mwaka 1954 alijiunga na Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza mara baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo cha Serikali, Ibadan. Katika kipindi cha miaka 6 aliyokua Uingereza alikua akiandika na kuongoza uigizaji wa tamthiliya za majukwaani katika kampuni ya Royal Court Theatre mwaka 1958-1959. Akiwa hapo chuoni aliwahi kua mhariri wa jarida maarufu la chuoni hapo la The Eagle. Mwaka 1960 alifadhiliwa na taasisi ya Rockefellers kurudi nchini Naijeria kwa ajili ya kuifanyia utafiti tamthiliya ya Kiafrika katika chuo Kikuu cha Ibadan wakati huo kiitwa University College, Ibadan.
Amewahi kufundisha tamthiliya na fasihi katika Vyuo Vikuu vya Obafemi Owolowo (zamani Ife), Ibadan na Lagos ambapo mwaka 1975 alikua Profesa wa Fasihi Linganishi (Comparative Literature). Mwaka 1960 Soyinka alianzisha kundi la sanaa za jukwaani la The 1960 Masks na mwaka 1964 akaunda kampuni aliyoiita The Orisun Theatre Company. Kote alizalisha tamthiliya zake na pia alishiriki kama muigizaji. Lakini pia mwaka 1957 aliwahi kuwa mshiriki na mhariri katika jarida la Black Orpheus ambalo lilikua likichapisha kazi za washairi wa Afrika kama Christopher Okigbo wa Naijeria, Dennis Brutus na Alex La Guma wa Afrika ya Kusini pamoja na Tchicaya U Tam'si wa Kongo Brazzaville.
MSUKUMO KATIKA KAZI ZA FASIHI
Soyinka alivutiwa sana na uandishi wa John Millington Synge mwandishi wa Ireland, lakini alipenda sana kuzilinganisha kazi zake na utamaduni wa maigizo ya Afrika akichanganya na muziki, dansi pamoja na vitendo (uigizaji). Pia uandishi wake uliegemea katika masimulizi yaliyohusisha utamaduni wa kabila la Yoruba uliolenga hasa kumzungumzia Ogun ambaye ni mungu wa kabila hilo. Aliandika tamthiliya yake ya kwanza inaoitwa The Swamp Dwellers (1958) akiwa nchini Uingereza ambayo iliigizwa huko Ibadan 1958 na The Lion and the Jewel iliyoigizwa 1959, hizi zote zilichapishwa mwaka 1963.
TAMTHILIA
The Lion and the Jewel imekua ikifundishwa kwa muda mrefu sana katika somo la fasihi ya kiingereza hapa chini. Mchezo huu ni mchezo wa kuchekesha kuhusu mgongano kati ya maadili ya jadi ya Kiafrika na athari za ustaarabu wa kisasa wa Magharibi. Katika tamthilia nzima, Soyinka anagusia mada za mila dhidi ya usasa, nafasi ya wanawake katika jamii, na utata wa upendo na tamaa. Vipengele vya ucheshi vya tamthilia hii huifanya kuwa ya kuburudisha na kusisimua, kwani inatoa ufafanuzi kuhusu mivutano inayoendelea kati ya mila na mabadiliko katika Afrika ya baada ya ukoloni.
Picha kwa hisani ya Amazon |
Miongoni mwa kazi zake nyingine ni pamoja na The Trials of Brother Jero (1963) ambayo iliwahi kutafsiriwa katika lugha ya Kiswahili kama "Masaibu ya Ndugu Jero" na A. S. Yahya. Pia aliandika Jero's Metamorphosis (1973) ambao ni muendelezo. Hizi ni tamthilia za kejeli zinazomhusu mhusika Ndugu Jeroboamu, anayejulikana kama Ndugu Jero. Tamthilia hizi zinaeleza kuhusu matendo ya ufisadi ya baadhi ya viongozi wa dini na wepesi wa wafuasi wao. Kwa pamoja, tamthilia hizi hutoa ukosoaji mkali wa taasisi za kidini na kisiasa katika jamii za Kiafrika baada ya ukoloni. Soyinka anetumia ucheshi na kejeli kutoa mwanga juu ya ghiliba, unafiki, na unyonyaji ulioenea katika mifumo hii.
Picha kwa hisani ya Amazon |
Vingine ni A Dance of the Forests (1973), Kongi's Harvest (1967) na Madmen and Specialists (1971) hivi viliigizwa majukwaani kwa kufikisha ujumbe kama kejeli kwa kutumia ucheshi kwa walengwa ambao ulikuwa ni utawala wa kijeshi nchini Naijeria kwa wakati huo. Miaka niliyoandika kwenye mabano ni muda ambao kitabu husika kilichapishwa na sio uigizwaji jukwaani.
Picha kwa hisani ya Amazon |
Zipo tamthilia ambazo hazikuwa na kejeli kama vile The Strong Breed (1963), The Road (1965), The Bacchae of Euripides (1973) na Opera Wangosi (1981). Vitabu vingine alivyoandika ni Play of Giants (1984), Requiem for Futurologist (1985), Camwood on the Leaves (1960), Before the Blackout (1960), Death and the King's Horseman (1975) , From Zia, with Love (1992), The Beatification of Area Boy (1995), King Baabu (2001), Etiki Revu Wetin (2005), Alapata Apata (2011) na vitabu vingine vingi.
RIWAYA
Soyinka ameandika riwaya tatu: The Interpreters (1965) ambayo hadithi yake inawakutanisha wasomi kadhaa wa Naijeria: Egbo, Sekoni, Kola, Sagoe na Bandele wanaozungumzia kuhusu Uafrika na hasa kuikomboa nchi yao katika rushwa na mengine yasiyofaa. Wasomi hao wanajaribu kuangalia mabadiliko katika jamii yanayokuja kwa kasi hasa kusahaulika mila,desturi na tamaduni za kiafrika na ushawishi wa utamaduni wa Magharibi na Elimu.
Picha kwa hisani ya Amazon |
Nyingine ni Season of Anomy (1973) Hii anazumngumzia mawazo yake yeye kama mwandishi. Anagusia nafasi ya mtu mmoja mmoja katika kuleta mabadiliko kwenye jamii ilijawa na uovu na mmomonyoko wa maadili hasa rushwa. Ina wahusika wachache tu ambao wanachukua hatua kupambana na jamii ya Naijeria iliyojaa rushwa na mmomonyoko wa maadili.
Picha kwa hisani ya Amazon |
Riwaya ya tatu ni Chronicles from the Land of the Happiest People on Earth (2020). Riwaya hii ni kejeli hasa ikizungumzia masuala ya kisiasa na kijamii katika jamii ya sasa ya Naijeria. Riwaya hii inazungumzia kuhusu rushwa ambayo ni tatizo hasa katika nchi za Afrika, usaliti wa kisiasa na matatizo mengine ya kijamii yanayoikabili Naijeria ya sasa. Jina la kitabu tu ni kejeli tosha kuhusu jinsi jamii ya nje inavyoichukulia Naijeria na uhalisia halisi wa yanayoendelea nchini humo. Soyinka anatumia kejeli, ucheshi na uchunguzi wa kina kuelezea hali halisi katika nchi za Afrika. Riwaya hii inasadifu mambo mengi ambayo nchi za Afrika zimepitia hasa baada ya ukoloni.
Picha kwa hisani ya Amazon |
TAWASIFU
Tawasifu (autobiography) ni masimulizi yanayoandikwa na msanii mwenyewe kumhusu yeye mwenyewe. Hii ni tofauti na wasifu (bibliography) ambayo ni mmasimulizi kuhusu maisha ya mtu yanayoandikwa na mtu mwingine. Tawasifu hizo ni The Man Died: The Prison Notes of Wole Soyinka (1972). Katika tawasifu hii ambayo ni kama insha, Soyinka anaelezea maisha yake ya gerezani ambako alitiwa nguvuni kwa kujaribu kuilingilia mazungumzo wakati wa vita ya Biafra. Kitendo hiko kikapelekea kutiwa nguvuni na kuwekwa jela kwa miezi 27 kati ya mwaka 1967-1969 bila hukumu na kutiwa hatiani. Soyinka anaelezea maisha yake akiwa gerezani hasa ukatili aliofanyiwa, vitendo vinavyokizana na haki za binadamu, unyanyasaji wa kisaikolojia na migongano na maofisa wa gereza, walinzi na wafungwa wenzie katika gereza la Gowon.
Picha kwa hisani ya 4Sahadows Books |
Tawasifu nyingine ni Aké: The Years of Childhood (1981) ambayo inaelezea maisha yake ya utotoni hadi kufikia miaka 11. Humo anaelezea maisha yake katika familia yake, utamaduni wa jamii ya Yoruba, kipindi cha ukoloni na nyakati ambazo zimetengeneza maisha ya mmoja wa waanshishi wa fasihi ya kiafrika. Soyinka anaelezea matukio ya utotoni mwake kujaribu kuelewa maisha ya ukubwani, matukio na vijana wa umri wake (peer) na jitihada za kufamu mazingira na mji wa Ake ambako ndiko alikozaliwa na kuishi. Mji huu uliopo Magharibi mwa Naijeria.
Picha kwa hisani ya Amazon |
Tawasifu nyingine ni Ìsarà : A Voyage around "Essay" (1989). Tawasifu hii ameielekeza (dedicated) kuwa kumbukumbu ya baba yake ambaye amemuita jina la Essay. Kitabu hiki ni mjumuisho wa masimulizi na hadithi kumhusu baba yake na kipindi cha ukoloni nchini Naijeria.
Picha kwa hisani ya Amazon |
Nyingine ni You Must Set Forth at Dawn (2006). Tawasifu hii ni muendelezo wa ile ya awali "Aké". Humo anaelezea maisha yake ya ukubwani, nafsi yake katika harakati za kisiasa nchini Naijeria kipindi alichoshikiliwa gerezani na maisha yuhamishoni (exile) na muingiliano na wanasiasa. Tawasifu nyingine ni Ibadan: The Penkelemes Years: a memoir 1946-65 (1994)
Picha kwa hisani ya Amazon |
INSHA
Ameandika insha kadhaa ambazo ni Myth, Literature and the African World (1975). Humu anaelezea nafsi ya hadithi katika fasihi ya kiafrika akiilinganisha na tamaduni za Magharibi na kuelezea mtazamo wake kuhusu mtazamo mpana wa kiafrika kupitia masimulizi na hadithi.
Picha kwa hisani ya Amazon |
Nyingine ni Art, Dialogue, and Outrage: Essays on Literature and Culture (1993). Huu ni mjumuisho wa mada mbalimbali kuhusu utamaduni wa Afrika, uhalisia wa maisha baada ya ukoloni, na nafasi ya fasihi katika jamii. Inajumuisha pia namna Soyinka anapokea uhakiki na ukosoaji wa kazi zake pamoja na mazungumzo na waandishi wengine.
Picha kwa hisani ya Amazon |
Insha nyingine ni Of Africa (2012). Humu anaelezea historia ya Afrika, tamaduni, changamoto na nafasi ya barabla Afrika katika masimulizi. Anajadili mada kama vile dini, siasa na utambulisho (identity).
Picha kwa hisani ya Amazon |
Insha nyingine ni The Burden of Memory The Muse of Forgiveness (1999) ambapo anaelezea kuhusu mabadiliko ya kisiasa na kijamii baada ya ukoloni akijikita zaidi katika changamoto za kumbukumbu na historia za matukio ya ukoloni, na kuwepo haja ya kusameheana na kupatana.
Picha kwa hisani ya AmazonPia ameandika Climate of Fear (2004) ambayo ni mjumuisho wa mihadhara (lectures) alizoziwasilisha katika jukwaa la BBC Reith Lectures. Humo anazungumzia kuhusu hali ya hofu na wasiwasi ulimwenguni baada ya tukio la kigaidi la Septemba 11 huko Marekani, matokeo ya tukio hilo kwa jamii na mtu mmoja mmoja. Anazungumzia ugaidi na ukandamizaji wa kisiasa unavyochochea hali ya hofu. Anaeleza namna hofu inavyoweza kutumiwa kama dhana ya kukandamiza siasa za upinzani, kuminya uhuru wa kutoa maoni nakadhalika.
Picha kwa hisani ya Amazon |
Insha nyingine ni Beyond Aesthetics: Use, Abuse, and Dissonance in African Art Traditions (2019). Hii inaakisi nafasi ya sanaa na muingiliano wake na siasa na taaluma nyingine ikizama zaidi katika maisha ya Soyinka na mtazamo mpana kuhusu sanaa za utamaduni wa Afrika.
Picha kwa hisani ya Amazon |
USHAIRI
Licha ya kuwa umaarufu wa Soyinka unatokana na uandishi wa tamthilia hayuko nyuma pia katika ushairi. Miongoni mwa vitabu vya vya ushairi ni Idanre and Other Poems (1967). Hiki ni kitabu chake cha mwanzo cha mashairi. Chimbuko la kitabu hiki ni eno le Idanre ambayo ni sehemu ya muhimu katika masimulizi ya utamaduni wa jamii ya Yoruba kwa vile kinagusia sana tamaduni na simulizi za huko.
Picha kwa hisani ya Amazon |
Kingine ni A Shuttle in the Crypt (1972) ambacho alikiandika wakati akiwa gerezani kipindi cha vita ya Biafra. Dhamira za mashairi yake ni kuhusu kutengwa, mateso na uvumilivu katika kipindi kigumu.
Picha kwa hisani ya Amazon |
Kitabu kingine ni Ogun Abibiman (1976) hii ni mojawapo ya kazi zake nyingi zinazomuenzi mungu wa Yoruba, Ogun. Ogun ni mungu wa chuma, vita, na ubunifu, na anashikilia nafasi muhimu katika masimulizi na ya Kiyoruba. Soyinka ambaye ana ibada ya kibinafsi kwa Ogun, mara nyingi humwomba mungu katika kazi zake kama ishara ya ubunifu, mabadiliko, na mapambano yaliyomo katika uzoefu wa mwanadamu. Katika shairi hili Soyinka anachanganya Kosmolojia ya Kiyoruba na kisiasa na kijamii. mapambano ya Afrika. "Abibiman" ni neno linalorejelea Afrika. Shairi linaangazia changamoto zinazolikabili bara la Afrika, hitaji la umoja, na tumaini la kufufuliwa upya na mabadiliko. Shairi hili ni wito wa kuchukua hatua na maombolezo, likiangazia tofauti za Afrika baada ya ukoloni - urithi wake tajiri na changamoto zake za kisasa. Uelewa wa kina wa Soyinka wa mila za Kiyoruba na ushiriki wake wa kina na hali halisi ya Afrika baada ya ukoloni unakutana " Ogun Abibiman," na kuifanya tafakari ya kuhuzunisha juu ya siku za nyuma, za sasa na zijazo za bara.
Picha kwa hisani ya Goodreads |
Pia ameandika Mandela's Earth and Other Poems (1988). Mjumuisho wa mashairi katika kitbu hiki yalikuwa ni mahsusi kwa Nelson Mandela, kiongozi na mpigania haki dhidi ya sera ya ubaguzi nchini Afrika Kusini. Pia kinazungumzia kuhusu uhuru wa watu, uthabiti na udhalimu.
Picha kwa hisani ya Amazon |
Soyinka aliandika Samarkand and Other Markets I Have Known (2002). Katika ushairi huu Soyinka aliakisi maeneo aliyotembelea na mambo aliyoyaona.
Picha kwa hisani ya Amazon |
Pia aliandika Early Poems (1998). Kitabu hiki ni mjumuisho wa mashairi ya mwanzo kabisa ya Soyinka. Katika kitabu hiki mashairi yanasadifu historia ya Naijeria, utamaduni, siasa na maisha baada ya ukoloni. Pia ameandika Poems from Prison" (1969)
Picha kwa hisani ya Amazon |
FILAMU
Soyinka amewahi kuandika na kuongoza filamu Blues for a Prodigal (1984) hii ni filamu ambayo Soyinka alihusika katika uandishi na uongozaji. Filamu hii ina muundo wa baadhi ya vipengele vya kazi za awali za Soyinka na uzoefu wake wakati wa Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Nigeria. Inahusu mtu mpotevu anayerejea katika mji wake na kuangazia mada mbali mbali za kijamii na kisiasa kwa kuzingatia ukosoaji wa Soyinka kuhusu jamii ya Nigeria.
Ingawa filamu hii haitambuliwi sana au kujadiliwa kwa upana kama kazi nyingine nyingi za Soyinka bado inasimama kuonesha umahiri wake katika mambo mengi na kujiingiza kwake katika tasnia ya filamu na kuleta mtindo wake wa kipekee wa masimulizi na masuala ya dhamira kwa hadhira tofauti.
TUZO, HESHIMA NA SIFA
Soyinka ametunukiwa tuzo nyingi sana kutokana na uandishi wake hasa wa tamthilia na harakati zake katika demokrasia na haki za binadamu. Tuzo hizi ni kuanzia nchini mwake Naijeria na kimataifa. Ametunukiwa tuzo nyingi na kutajwa katika tuzo nyingi. Hizi ni baadhi ya tuzo na heshima alizotunukiwa:
(i) Tuzo ya Nobel katika Fasihi (1986). Hii ni tuzo ya maarufu ambayo Soyinka amewahi kutunukiwa na kuwa Mwafrika wa kwanza kutunukiwa tuzo hiyo katika kipengele cha Fasihi. Katika maelezo kumhusu alielezewa kuwa ni mtu "ambaye katika mtazamo mpana wa kitamaduni na kwa sauti za kishairi ametengeneza drama ya kuwepo".
Wole Soyinka akipokea tuzo ya Nobel mwaka 1986. Picha kwa hisani ya Nairaland |
(ii) Tuzo ya Agip katika Fasihi kwa tawasifu yake ya Aké: The Years of Childhood.
(iii) Udaktari wa Heshima kwa kutambua mchango wake katika Fasihi na Harakati za utetezi Haki za Binadamu. Soyinka ametunukiwa Shahada hizo za Heshima na vyuo na vyuo vikuu zaidi ya 16 ikiwemo Havard, Oxford, Yale, Cambridge, Leeds, Cornell, Ibadan, Princeton, Obafemi Owolowo, Ibadan, École Normale Supérieure, Cape Town, Alberta, Neuchãtel, Toronto, Morehouse na vyuo vingine vingi.
Wole Soyinka na wenzie walipotunukiwa Udaktari wa Heshima na Chuo Kikuu Cambridge mwaka 2022. Picha kwa hisani ya tovuti ya Cambridge |
(v) Tuzo ya Academy of Achievement Golden Plate (2009)
(vi) Tuzo Maalumu (Special Prize) ya Kumbi za Michezo ya Maigizo ya Ulaya (European Theatre Prize) mwaka 2017. Alitunukiwa kwa "kuchangia katika utambuzi wa matukio ya kitamaduni ambayo yanakuza uelewa na kubadilishana maarifa kati ya watu"
(vii) Tuzo ya Anisfield-Wolf Books (1983) kwa tawasifu yake ya Aké: The Years of Childhood.
(viii) Mwanachama wa Jumuiya ya Kifalme ya Fasihi (the Royal Society of Literature) mwaka 1983.
(ix) Mwanachama katika Chama cha Lugha ya Kisasa (Fellow of the Modern Language Association)
(x) Alipewa Heshima ya kuwa Mwanachama wa Heshima katika jumuiya ya American Academy of Arts and Letters mwaka 1986.
(xi) Tuzo ya Kimataifa kuhusu masuala ya kibinadamu (International Humanist Award) na Umoja wa Kimataifa wa Kibinadamu na Maadili (International Humanist and Ethical Union) mwaka 2014.
(xii) Tuzo ya Desmond Tutu kwa Haki za Binadamu na Amani mwaka 2017.
(xiii) Tuzo ya Mafanikio katika Maisha (Lifetime Achievement Award) ya Anisfield-Wolf Book mwaka 2013.
(xiv) Medali ya The Benson aliyotunukiwa na Royal Society of Literature.
(xv) Tuzo ya Premi Internacional Catalunya mwaka 2007 ambayo alitunukiwa kwa kazi yake ya kukuza maarifa ya kitamaduni na kijamii.
(xvi) Tuzo ya Prince Claus mwaka 2008 ambayo alitunukiwa kwa kuthamini mafanikio yake kama mwandishi wa tamthilia.
(xvii) Medali ya William Edward Burghardt Du Bois ya Chuo Kikuu Harvard mwaka 2014.
(xviii) Tuzo ya Pak Kyong-ni mwaka 2017. Hii ni tuzo ya Kimataifa ya Fasihi iiliyoanzishwa Korea Kusini kama heshima ya kumuenzi maandishi wa riwaya wa Korea Kusini Pak Kyong-ni. Soyinka ni Mwafrika wa kwanza kutunukiwa tuzo hii.
(xix Mwanachama wa Heshima katika jumuiya ya Fasihi ya Naijeria (Literary Society of the Nigerian Academy of Letters)
(xx) National Order of Merit of the Federal Republic of Benin.
MAISHA YA NDOA NA WATOTO
Soyinka amewahi kuoa mara 3 na katika ndoa zote alibahatika kupata watoto. Mwaka 1958 alimuoa Barbara Dixon huyu alikua mwandishi wa Uingereza.
Mwaka 1963 alimuoa Olaide Idomu mkutubi huko Naijeria.
Mwaka 1989 alimuoa Folake Doherty ambaye ni mke wake mpaka sasa.
Soyinka ameyaweka mbali maisha yake binafsi kwa umma kwa hivyo hata taarifa zake binafsi nyingine wakati mwingine ni vigumu kuzifahamu. Jambo ambalo ameliweka wazi sana ni kazi zake kama mwandishi.
Soyinka anao watoto 8 kutoka katika ndoa zote 3 alizowahi kufunga. Watoto wake wanaishi Naijeria na kufanya kazi katika kada tofauti tofauti.
KUFUNGWA GEREZANI NA MAISHA YA UHAMISHONI
Licha ya kuwa na wasifu mzuri katika taaluma ya fasihi duniani Soyinka amewahi kuwa na mgogoro na Serikali ya Naijeria. Mwaka 1967 alikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na kuchochea vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Naijeria maarufu kama Biafra. Bila shaka unaikumbuka vita hii ambayo majimbo ya Kusini Mashariki mwa Naijeria yalijitangazia uhuru kamili na kutengeneza Jamhuri ya Biafra. Soyinka aliwekwa jela bila kutiwa hatiani kwa kosa lolote. Hii ilipelekea Soyinka kushikiliwa kama mfungwa wa kisiasa kwa miezi 27 (1967-1969) alipoachiliwa. Mwenyewe hukiri kwamba kipindi hiki cha ufungwa wa kisiasa kina mchango mkubwa katika uandishi wake na mtazamo kuhusu siasa na haki za binadamu.
Baada ya kuachiwa Soyinka alishiriki katika utengenezaji wa filamu aliyoiita Kongi ili kuhakikisha maudhui yanabaki kama alivyoandika. Filamu hii inatokana na kazi yake kwa jina Kongi's Harvest. Katika filamu hiyo Soyinka alitoa mtazamo wake kuhusu kupinga vikali utawala wa kijeshi nchini Naijeria.
Baada ya kutoka jela aliondoka Naijeria kwa kipindi kilichokadiriwa kuwa miaka 5. Katika miaka hiyo Soyinka alifanya kazi nchini Uingereza, Ufaransa na Ghana. Katika kipindi hicho Soyinka aliandika muswada wa tamthilia ya Jero's Metamorphosis (1973) ambayo ni muendelezo wa ile ya awali ya The Trials of Brother Jero. Humo kuna muunganiko wa ucheshi na kuonesha ukatili uliofanywa na utawala wa kijeshi kwa kutumia silaha dhidi ya watuhumiwa. Japokuwa Soyinka alituma nakala kwa waongozaji wa tamthilia nchini Naijeria hakuna aliyeonesha kuvutiwa na muswada wake kwa vile bado utawala wa kijeshi ulikua madarakani kwa hiyo waongozaji walihofia uhuru wao.
Mwaka 1994 aliondoka tena Naijeria kutokana na ukosoaji wake kwa Serikali ya kijeshi ya Jenerali Sani Abacha baada ya ule uhamishoni wa baada ya kutoka jela. Akiwa uhamishoni mara kwa mara alipaza sauti yake katika jumuiya za kimataifa kuingilia kati hali ya usalama nchini Naijeria hasa katika utawala wa Abacha. Alikosoa kuhusu rushwa, kukosekana kwa demokrasia na mauaji ya Ken Saro-Wiwa na washirika wenzie 8. Pia aliandika kitabu The Open Sore of a Continent (1996) ambacho kinazungumzia sana hali ya kisiasa barani Afrika hasa utawala wa kijeshi nchini Naijeria chini ya Jenerali Sani Abacha. Anakosoa na kuufananisha utawala wa kijeshi wa Jenerali Sani Abacha na kidonda kinachosababisha maumivu kwa taifa la Naijeria.
Picha kwa hisani ya Amazon |
HARAKATI ZA HAKI ZA BINADAMU NA DEMOKRASIA
Soyinka amekuwa mstari wa mbele katika harakati za haki za binadamu na demokrasia nchini Naijeria tangu enzi za ukoloni, kabla, wakati na baada kipindi cha kufungwa na kuishi uhamishoni.
Ameshiriki katika makundi mbalimbali ya kisiasa kama vile National Democratic Organization, National Liberty Council of Nigeria na PRONACO.
Alikua ni mkosoaji mkubwa wa utawala wa kijeshi wa Jenerali Sani Abacha (1993-1998)
Pia, mwaka 2010 alianzisha chama cha Democratic Front for a People's Federation na akahudumu kama mwenyekiti.
Mwaka 2016, alisema kama Donald Trump angeshinda uchaguzi mkuu wa nchi ya Marekani basi angechana kibali chake cha kuishi katika nchi hiyo (American Green card) hii ni kwa sababu anasema hakuvutiwa na sera za Trump ambazo aliziona ni za kibaguzi na zinakinzana na haki za binadamu. Trump aliposhinda alitimiza ahadi yake hiyo japo si kwa kuchana kibali hicho bali alikifanya kisiweze kutumika. Ukosoaji wake kwa Trump na msimamo wake dhidi ya Marekani kwa wakati huo, sera na matamshi ya Rais yanaakisi wasiwasi wake mpana kuhusu siasa za kimataifa na haki za binadamu. Maoni ya Soyinka kuhusu Trump yanawiana na dhamira yake ya muda mrefu ya kuzungumza dhidi ya kile anachokiona kuwa dhuluma, ukandamizaji na ukosefu wa haki katika mazingira mbalimbali duniani.
Soyinka amekua mstari wa mbele kukosoa vitendo vyote vinavyokinzana na haki za binadamu ikiwemo udikteta. Ipo nukuu yake maarufu ambayo hutumiwa sana na wanaharakati wa haki za binadamu, demokrasia na ukosoaji, "The greatest threat to freedom is the absence of criticism" kwa tafsiri rahisi "jambo la kuogopesha kuhusu uhuru wa watu ni kukosekana kwa uhuru wa ukosoaji". Nukuu hii inalenga san ukosoaji wa masuala yote yanayofanywa na watawala na yanakinzana na utawala bora.
KWA UFUPI
• Alizaliwa Julai 13, 1934.
• Baba yake, Samwel Ayodele Soyinka alikua ni Mchungaji wa Kanisa la Anglikana na Mkuu wa Shule.
•Mama yake Grace Eniola Soyinka alikua na duka lakini pia alishiriki katika harakati za kumkomboa mwanamke nchini humo.
• Familia yake ni ya watu wa Yoruba, ambao utamaduni wao umeathiri kazi zake.
• Ni mwandishi mahiri aliye na kazi mbali mbali zinazohusu maigizo, mashairi na nathari (prose)
• Ukosoaji wake wa wazi dhidi ya tawala za kisiasa za Nigeria umechangia kuishi kwake nje ya nchi haswa Marekani ambako amewahi kuwa profesa katika vyuo vikuu mbalimbali.
• Shahada yake ya Awali alisoma Lugha ya Kiingereza katika Fasihi Chuo Kikuu cha Leeds.
• Mwaka 2005-2006 aliwahi kuwa kwenye Bodi ya Washauri wa Wahariri wa Encyclopaedia Britannica.
• Amewahi kufundisha katika Vyuo Vikuu vifuatavyo: Havard, Oxford, Emory, Loyola Marymount, Yale, Chuo Kikuu cha Nevada na vingine.
• Maandishi ya Soyinka yanachukua miongo mingi na yanajumuisha dhamira mbalimbali, kimsingi yanahusu mila za Kiafrika, udhalimu wa kisiasa na haki za binadamu.
• Amewahi kuigiza majukwaani nchini kwao Naijeria na Uingereza.
MENGINEYO
Maisha ya Soyinka yamebainishwa na dhamira yake isiyoyumba kwa haki za binadamu na uhuru wa kujieleza, na anasalia kuwa sauti yenye ushawishi katika fasihi na siasa.
Ingawa shughuli zake za kifasihi na kisiasa zimeandikwa vizuri, Soyinka ana mwelekeo wa kuweka maelezo ya maisha yake ya kibinafsi mbali na macho ya umma, kwa hivyo habari kuhusu ndoa na uhusiano wake hazijaangaziwa sana kwenye vyombo vya habari ukianganisha na zake za kikazi.
Soyinka ni mmoja wa waandishi wa Kiafrika waliopambwa zaidi na amepokea tuzo nyingi na sifa katika kazi zake zake za uandishi na uanaharakati.
Soyinka amekuwa na makongamano mengi ya kitaaluma na ya kifasihi yaliyoelekezw kumuenzi kwa kazi zake. Amekuwa akialikwa kama mzungumzaji mkuu katika hafla nyingi za kimataifa na kazi zake nyingi zimebadilishwa kuwa aina tofauti za kazi na hivyo kumfanya kuwa wa tofauti zaidi katika sanaa.
Kazi zake za kishairi mara nyingi hujikita katika mada za mila za Kiafrika, hali halisi ya baada ya ukoloni, msukosuko wa kisiasa, haki za binadamu, na makutano ya mapambano ya kibinafsi na ya kijamii.
MAKALA HII IMEANDALIWA NA KUANDIKWA NA VENANCE GILBERT KWA MSAADA WA VYANZO MBALIMBALI. WASILIANA NAMI KUPITIA
📞 0753400208
📧 venancegilbert@gmail.com
Uandishi mzuri ndugu, lugha nyepesi inaeleweka. Keep up the good work.
ReplyDelete