RAIS KIKWETE AELEKEZA NGUVU KATIKA ELIMU YA KIDATO CHA 5 & 6

Rais Jakaya Kikwete akipokea tuzo maalum kutoka kwa Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi, Dk.Shukuru Kawambwa kwa kutambua mchango wake katika kuendeleza na kuboresha elimu nchini wakati wa maadhimisho ya kilele cha wiki ya elimu yaliyofanyika katika uwanja wa michezo wa Jamhuri mjini Dodoma jana. Picha na Ikulu

Rais Jakaya Kikwete jana alitumia kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Elimu kuaga wadau wa sekta hiyo, akisema sasa nguvu zielekezwe katika kujenga majengo kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu ya sekondari.

Rais Kikwete, ambaye alikiri kuwapo udhaifu katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, alisema mafanikio pia ni makubwa kiasi kwamba sasa hakuna wanafunzi wanaokosa nafasi ya kwenda sekondari baada ya kufaulu na hivyo nguvu sasa inatakiwa kuwekwa katika kuongeza miundombinu ya kidato cha tano na sita.

Kikwete alitoa kauli hiyo jana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa alipohutubia maelfu ya wakazi wa Dodoma, wakiwamo wanafunzi wa shule za sekondari na msingi katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Elimu.

Rais alisema katika kipindi cha uongozi wake, amekuwa akitamani kutekeleza yale aliyoyaahidi bila ya kuacha jambo na akaongeza kuwa kuna haja ya kuongeza majengo kwa kidato cha tano na sita pamoja na kukamilisha majengo ya maabara.

Rais Jakaya Kikwete aliwataka wadau wa elimu na sekta binafsi kujenga shule za kidato cha tano na sita ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya elimu ambalo amelifikisha katika hatua nzuri katika kipindi chake cha miaka 10.

Kikwete, ambaye uongozi wake ulianzisha mkakati wa kujenga shule za sekondari za kata, alisema kwa sasa zipo za kutosha kumuwezesha kila mwanafunzi anayemaliza darasa la saba kupata nafasi ya kwenda sekondari kulingana na ubora na kiwango cha ufaulu wake.

“Ukiona mtoto amefeli, basi amefeli kweli na siyo kama zamani tulipokuwa tunasema hakuchaguliwa kwani nafasi zilikuwa chache. Hivi sasa anayefaulu kulingana na vigezo anapata nafasi hayo ni mafanikio makubwa katika elimu,” alisema Rais Kikwete.

Alifafanua kuwa hata bajeti ya elimu kwa miaka yake 10 aliyokuwa madarakani imekuwa ikiongezeka kila mwaka huku mwaka ya mwaka 2014/15 ikiwa kubwa kuliko miaka miaka iliyopita.

Alitoa mfano wa bajeti ya mwaka 2005/2006 wakati anaingia madarakani zilitengwa Sh669.5 bilioni wakati mwaka 2014/2015 zimetengwa Sh3.1 trilioni ili kuhakikisha kunakuwapo na elimu bora inayopatikana katika nyanja zote.

Alifafanua kuwa hata bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu imeongezeka kutoka Sh56.1 bilioni hadi Sh345 bilioni. Kwa sababu hiyo idadi ya wanafunzi wanaofaidika imeongezeka kutoka 16,345 mwaka 2005 hadi 98,000 mwaka 2014.  Huku shule za msingi zikiongezeka kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi 16,343 mwaka 2014.

Pamoja na kusifia mambo mengi ambayo alisema yamefanywa na utawala wake, Rais alikiri kuwa bado kunahitaji kazi ya ziada katika kufanikiwa kielimu kama ilivyo kwa nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tumefanikiwa katika mambo mengi kwenye elimu ingawa bado tunakabiliwa na changamoto. Kazi iliyopo mbele yetu ni kuhakikisha elimu inakuwa bora zaidi na kwa wote,” alisema JK.

“Tumefanya mambo mengi kwa pamoja. Nawaageni bai bai kwani sherehe zijazo mtakuwa na Rais Mwingine, mkitupa nafasi tena haya.”

Alisema mpango wa Tekeleza Matokeo Makubwa Sasa (BRN) aliutoa nchini Malaysia ambako alikuta kuna utaratibu wa kufuatilia masuala ya utekelezaji wa ahadi za Serikali.

“Wenzetu kule waliamua kuwafanyia mitihani walimu wao ili kujua kama kweli walikuwa na uelewa wa kile walichokuwa wanafundisha, walimu wengi walifeli hivyo wakagundua wanachokifundisha nao hawakijui,” alisema.

Kutokana na hilo, alisema kuwa Tanzania nao waliamua kuwapa mtihani walimu kwa baadhi ya masomo na kwamba nao walifeli.

Katika mkutano wa jana, Rais aliwatunuku vyeti na zawadi mbalimbali zikiwamo fedha wanafunzi na shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya kumaliza darasa la saba na kidato cha nne 2014.

Nao Wizara ya Elimu waliamua kumtunuku Rais tuzo mbili ikiwemo ya uongozi bora na Weredi na Tuzo ya BRN, huku Mama Salma Kikwete akitunukiwa tuzo ya kumtunza Rais hadi kufikia kiwango cha kutekeleza majukumu yake ipasavyo ambapo alipewa ng’ombe wawili wa maziwa.



Chanzo: Mwananchi Communication Ltd

PINDA: CCM ITAELEZA HAYA KWENYE KAMPENI ZA UCHAGUZI MKUU

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, jana alihitimisha mjadala wa makadirio ya Bajeti ya Ofisi yake ya Sh trilioni 5.7 ambayo ilipitishwa na Bunge, huku akifafanua hoja zitakazotumiwa na CCM kuomba kura za wananchi katika Uchaguzi Mkuu ujao.


Pinda alisema hakuna haja ya kuandikia mate wakati wino upo na kufafanua kuwa katika Uchaguzi Mkuu, CCM itatakiwa kueleza mafanikio ya Serikali katika nishati ya umeme vijijini, miundombinu ya barabara, elimu, maji na afya.


Alitaka waliokuwa wakijiuliza nani atashinda katika uchaguzi huo, wapitie kidogo historia kuanzia mwaka 1995 mpaka katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uliofanyika Desemba mwaka jana, ili waelewe nani alipata kipigo.


Elimu


Akifafanua kwa ufupi mafanikio yaliyopatikana katika elimu, Pinda alisema watakapoulizwa katika sekta hiyo nini kimefanyika, wataweka wazi kuwa ingawa bado kuna changamoto lakini yapo pia mafanikio makubwa.


“Wacha tubebe lawama katika changamoto, lakini tutaeleza kuwa katika vyuo vya ufundi mwaka 1995 na 1996, udahili katika vyuo vya ufundi ulikuwa 7,700 tu, mwaka 2005 wanafunzi 78,000 lakini takwimu za 2013, waliodahiliwa walikuwa wanafunzi 145,000,” alisema.


Katika vyuo vikuu, alisema mwaka 2005 walikuta vyuo vikuu vikiwa 23 lakini takwimu za 2013, zinaonesha kuwa vyuo vikuu vimefikia 50 na ongezeko hilo lisingewezekana kama si kuwepo kwa sera nzuri na usimamizi mzuri wa Serikali.


Kuhusu idadi ya wanafunzi waliodahiliwa katika vyuo hivyo, Pinda alisema mwaka 2005 walikuta wanafunzi 40,000 katika vyuo vikuu lakini mwaka 2015 wanaiacha nchi ikiwa na wanafunzi 200,000 waliopo katika vyuo vikuu mbalimbali.


Kuhusu ubora wa elimu aliosema kuwa una changamoto, lakini alikumbusha kuwa utafiti uliofanyika wa vyuo vikuu 100 bora Afrika, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),kiliibuka namba nne kwa ubora Afrika na kufuatiwa na Chuo Kikuu cha Capetown Afrika Kusini.


Katika elimu ya msingi, alisema alipokwenda Marekani alipatwa na mshangao kukabidhiwa Tuzo ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa katika Uandikishaji wa Wanafunzi wa Elimu ya Msingi.


Afya


Katika sekta ya afya, Pinda alisema umri wa kuishi wa Mtanzania umeongezeka huku vifo vya watoto chini ya miaka mitano vikipungua. “Tanzania ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika, zilizofanya vizuri katika kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano,” alisema.


Miundombinu ya barabara


Kuhusu miundombinu ya barabara, Pinda alihoji ni nani anayeweza kusimama kwa wananchi na kusema Serikali haijafanya chochote katika sekta hiyo.


“Hivi kuna anayeweza kusema kuwa katika barabara hatujafanya kitu na akasimama kwa wananchi kuomba kura? Njooni kule Rukwa nenda Kigoma useme hakuna kitu, nawahakikishia hamtapata kura,” alisema.


Aliwasema wabunge wa Kigoma ambao tangu Uhuru wamekuwa wakilalamika kuwa mkoa huo umetengwa na kushangazwa kwa hatua yao ya kutosema chochote kuhusu ujenzi mkubwa wa barabara kwenda katika mkoa huo na daraja kubwa la Kikwete.


Mbali na Daraja la Kikwete, Pinda alisema madaraja zaidi ya 20 yaliyokuwa kikwazo katika miundombinu ya barabara yamejengwa huku vivuko vingi katika mito, maziwa na bahari vikinunuliwa.


Maji, umeme


Kwa upande wa huduma ya maji, Pinda alisema kuna kazi kubwa imefanyika katika miaka miwili iliyopita na kutoa mfano wa Mradi wa Maji Karatu.


“Inasikitisha hata rafiki yangu wa Karatu akija hapa hasemi mradi huu ni mzuri. Wamejenga shule nzuri lakini hawasemi, lakini mimi nilipofika pale niliwasifia shule nzuri kwa kuwa najua wanatekeleza Ilani ya CCM,” alisema Pinda.


Kuhusu umeme vijijini, Pinda alisema ingawa hawajamaliza vijiji vyote lakini kazi imefanyika na kwa kuwa anaamini kuwa Serikali ijayo ni ya CCM, kazi hiyo itaendelezwa na Serikali ijayo.Kilimo
Katika kilimo, Pinda alisema changamoto kubwa iliyokuwa ikisumbua Taifa ilikuwa kukosekana kwa usalama wa chakula, jambo alilosema ilikuwa aibu kwa taifa kuomba chakula nje ya nchi.

Alisema Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, imejitahidi na leo Tanzania inatamba kuwa hata mikoa yenye njaa, italishwa kwa kutumiachakula kilichozalishwa ndani ya nchi.

AlisemaTanzania ni nchi ya nne barani Afrika kwa kuzalisha mahindi, duniani inashika nafasi ya 12 katika uzalishaji wa zao hilo huku akiongeza kuwa mwaka 2005 kulikuwa na matrekta 4, 000, sasa matrekta yaliyopo ni zaidi ya 10,000.

“Tusingewekeza katika uzalishaji wa mazao ya kilimo, tusingekuwa na jeuri ya kulisha mikoa yote yenye njaa. Kwa sasa tunaweza kulisha hata nje ya nchi na hivi karibuni, Sudan walikuja kuomba tuwasaidie. “Hata Kenya mwaka jana walikuja kuomba tuwasaidie tani 240,000 na tukawapa…nasema lazima tuone jeuri katika hilo,” alisema Pinda.

Uchumi


Pinda alisema yapo mambo mengi yanafanyika katika uchumi wa nchi na kutoa mfano wa utafiti wa wataalamu wa Benki ya Dunia (WB) wa mwaka 2012 kwa kushirikiana naTaasisi ya Business Insider kuhusu nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi.

Kwa kutumia vigezo vya ukuaji wa uchumi, Pinda alisema utafiti huo ulikuja na nchi 29 duniani ambazo zina uchumi unaokua kwa kasi na Tanzania ilishika namba 15.

Mbali na utafiti huo, mwingine ulifanywa na taasisi ya KPMJ ya Afrika Kusini kutafuta nchi kumi zenye uchumi unaokuwa barani Afrika na Tanzania ikashika nafasi ya sita.

Pia alitaja utafiti wa kikanda uliofanywa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) Aprili mwaka huu, ikabainishwa kuwa Tanzania inafanya vizuri. “Katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, sisi ndio tunaong’ara na hata hao watafiti wakija wanaona viashiria vilivyo bayana kabisa vya ukuaji wa uchumi,” alisema Pinda.

Alitoa mfano wa Mkoa wa Dodoma, kwamba alipokuwa anakuja na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere miaka ya 1980 na mkoa huo ulivyo sasa ni vitu viwili tofauti.

Ujenzi wa madarasa Pinda alisema anajua mafanikio hayo lazima yawaume Kambi ya Upinzani kwa kuwa wamenyang’anywa hoja za kuwaeleza wananchi katika uchaguzi mkuu.

Alisema hata kama inawauma hivyo, lakini ni vyema wanapojadili waheshimiane kuliko ilivyokuwa wakati wa kujadili makadirio ya Bajeti ya ofisi yake, ambapo baadhi ya wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani, walifikia hatua ya kuacha kuheshimiana na kuwaita mawaziri hawana akili.

“Ah! Inaonekana upande huo mna akili sana, lakini hivi Mbowe mkija kushika madaraka na sisi tukakaa huko tuache kuwaheshimu mtafurahi? Msiwatendee wenzenu lile msilopenda kutendewa,” alisema Pinda.

Alimtaka Mbowe na kundi lake la Umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA), katika mikutano yao ya kuchangisha fedha, wajaribu hata kujenga darasa moja ili wajue anachozungumzia cha kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo nini maana yake.



Chanzo: Habari Leo

RAIS NKURUNZINZA KULIPIZA KISASI KWA WAASI



 Burundi Pierre Nkurunziza amewapongeza wanajeshi wazalendo waliozuia mapinduzi na kurejesha hali ya usalama na utawala huru mjini Bujumbura.

Rais Nkurunziza amewataka waburundi wazalendo kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi utakaofanyika mwezi juni.

Rais huyo alikuwa Mjini Dar es Salaam Tanzania siku ya Jumatano kuhudhuria mkutano wa viongozi wa kanda ya Afrika Mashariki kundi la wanajeshi waasi walipotangaza ''Mapinduzi'' dhidi ya serikali yake.

Viongozi watatu miongoni mwa makamanda 6 wa jeshi waliounga mkono tangazo hilo la ''mapinduzi'' ilikupinga muhula wa tatu wa rais huyo tayari wamekamatwa.

Kufikia sasa watu 105,000 wameripotiwa kutorokea mataifa jirani kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.

Baada ya kurejea kutoka Tanzania rais Nkurunzinza alielekea Kaskazini mwa Bujumbura eneo alikotokea kabla ya kurejea katika kasri la rais lililoko katika mji mkuu wa Bujumbura.
Katika taarifa iliyochapishwa mtandaoni rais Nkurunzinza alisema kuwa ''
kuna amani na utangamano katika asilimia kubwa ya Burundi na hata katika mji mkuu wa Bujumbura ila tu watu wachache waasi ndio waliokuwa na hamu ya kuvuja damu''
''Jeshi la taifa lilionesha ukomavu wake lilipokabiliana na wasaliti hao''

''Ningependa kuwahimiza waburundi wazalendo walinde kwa dhati amani iliyoko sasa kwani ndio ngao na msingi wa demkrasia iliyoko Burundi''
''Shari msingi wa demokrasia yetu changa ilindwe isiyeyuke''
Nkurunziza aliahidi kulipiza kisasi dhidi ya ''yeyote aliyejaribu kuwasha moto wa uhasama baina ya waburundi''

Nkurunziza aliahidi kulipiza kisasi dhidi ya ''yeyote aliyejaribu kuwasha moto wa uhasama baina ya waburundi''
Rais Nkurunzinza aliwasili mjini Bujumbura Ijumaa akiwa ameambatana na maelfu ya wafuasi wake.

Mwandishi wa BBC aliyeko huko Ruth Nesoba anasema japo asilimia kubwa ya mji huo ulikuwa na amani, katika sehemu zingine kulikuwa na waandamanaji walioweka vizuizi barabrani wakipinga kuwania kwake kwa muhula wa tatu.

Polisi wa kupambana na ghasia walikuwa wakikabiliana nao kwa kuwafyatulia mabomu ya kutoa machozi.

Miongoni mwa makamanda waliokamatwa kwa kuchochea uasi ni pamoja na waziri wa zamani wa ulinzi Cyrille Ndayirukiye.

Makamanda watatu waliotangaza ''Mapinduzi'' wamekamatwa
Waziri wa sasa wa usalama Gabriel Nizigama aliiambia BBC kuwa maafisa wawili wakuu katika idara ya polisi pia walikamatwa pamoja na wadogo wao takriban 12 waliokuwa wakiwalinda.
Wawili hao walikamatwa baada ya ufyatulianaji wa risasi nje ya jumba walimokuwa
.
Kiongozi wa uasi huo meja jenerali Godefroid Niyombare,aliyetangaza ''mapinduzi'' hayo siku ya jumatano hajakamatwa japo alinukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa atajisalimisha.

''Nitajisalimisha kwa utawala, natumai hawataniua'' alisema meja jenerali Niyombare.

JACKLINE WOLPER ANASWA LIVE AKITOKA JUMBA LA FREEMASONS

Mshtuko! Staa wa sinema za Kibongo, Jacqueline Wolper Massawe ameibua maswali kwa mashuhuda walimuona ‘live’ akiingia kwenye hekalu la watu wa Jamii ya Siri (Secret Society) ya Freemasons yenye nguvu duniani inayohusishwa na imani za kishetani.

TUJIUNGE MTAA WA SOKOINE
Tukio hilo lililoibua kizaazaa kwa mashuhuda waliomuona Wolper, lilijiri juzikati, mishale ya jioni kwenye hekalu hilo lililopo Mtaa wa Sokoine mkabala na Hoteli ya Hyatt Regency, The Kilimanjaro jijini Dar jirani na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

SIMU ZAMIMINIKA
Likiwa kwenye majukumu ya kusaka habari kama kawaida yake, gazeti hili lilipokea simu kadhaa kutoka kwa mashuhuda hao wakiwataka wanahabari wetu kuwahi eneo la tukio.
Kufuatia umbali waliokuwa mapaparazi wetu, ilibidi kuwaomba mashuhuda hao ‘kumfotoa’ picha ambapo mmoja wao alifanya hivyo na kuziwasilisha kwenye meza ya gazeti hili.

ALINASWAJE?
Akidadavua mazingira aliyonaswa Wolper, shuhuda huyo alikuwa na haya ya kusema:
“Kwanza mwanzoni hatukumjua kama ni Wolper lakini kuna dada ambaye anamjua vizuri na ni shabiki wake mkubwa ndiye aliyetuhakikishia kuwa ni Jacqueline (Wolper).

“Kuna waliomuona akiingia. Nilipofika mimi nilimkuta getini anatoka. Walisema hakukaa muda mrefu kwani alitumia dakika kadhaa kisha akatoka na kwenda kwenye gari lake aina ya Prado (Toyota) alilopaki mbali kidogo na lango hilo,” alisema shuhuda huyo kwa sharti la kutotajwa jina na kuongeza:
“Baada ya hapo alitoka nduki maana nzi (watu) walikuwa wameanza kumjalia na kulizingira gari lake.”

WOLPER AJITETEA
Baada ya kuzikagua picha za Wolper akiwa katika mazingira hayo na kujiridhisha kuwa ni yeye, gazeti hili lilimbana mwigizaji huyo ambapo alijitetea:

“Jamani nilikuwa sina hili wala lile. Kuna jengo nilikuwa nalitafuta ndiyo nikajikuta nimetokea maeneo hayo.
“Mimi mwenyewe nilishtuka kuona watu wananiangalia sana kumbe ndiyo nikagundua nipo kwenye lango la Freemasons.”
Risasi Jumamosi: Mbona kuna mashuhuda walikuona wakati unaingia na wakati unatoka?
Wolper: Unajua mimi sikuona kibao chao lakini sikuingia kabisa hadi kule ndani.

Risasi Jumamosi: Lakini kuna madai kwamba wewe ni mwanachama. Unasemaje?
Wolper: Mimi siyo Freemasons, nakumbuka kuna siku watu walinifuata wakaniambia nijiunge Freemasons nitakuwa na mafanikio lakini sijakubaliana nao.

TUJIKUMBUSHE
Mwaka 2012 wakati wa kifo cha aliyekuwa mwigizaji mkubwa Bongo, marehemu Steven Kanumba ‘The Great’ kuliibuka madai ya baadhi ya wasanii ambao ilisemekana ni ‘memba’ wa Freemasons

Mbali na Kanumba, wengine waliotajwa kwenye listi hiyo mwaka huo alikuwepo Wolper na mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye madai hayo yamekuwa yakiendelea kumganda huku wengi wakiwa na imani potofu kuwa ukijiunga na jamii hiyo unapata utajiri wa ghafla.

Source:Global Publishers

HABARI LEO TAHARIRI: TFF IFANYIE KAZI KASORO ZA MSIMU ULIOMALIZIKA

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara umemalizika Jumamosi iliyopita, huku timu za Polisi Morogoro na Ruvu Shooting ya mkoani Pwani zikishuka daraja.

Kushuka kwa timu hizo mbili kunatoa nafasi kwa timu nne kupanda daraja kukiwa na lengo la kuongeza timu shiriki kutoka 14 hadi 16 katika msimu ujao wa ligi hiyo.

Timu zilizopanda daraja ni Majimaji ya Songea, African Sports ya Tanga, Toto African ya Mwanza na Mwadui ya Shinyanga, ambazo zinakamilisha timu hizo nne.

Wakati msimu huo wa ligi ukifungwa, tayari Yanga na Azam FC walishajitangazia nafasi za kwanza na pili na kuwa na uhakika wa kuliwakilisha taifa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa na ile ya Shirikisho la Afrika.

Baada ya kumalizika kwa msimu huu wa ligi ndio mwanzo wa msimu unaokuja na timu zinatakiwa kujipanga vizuri kwa ajili ya msimu huo, ambao kama baadhi ya makosa yatarekebishwa, inaweza kuwa ligi bora zaidi.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), timu pamoja na wadau wengine wa ligi hiyo kama kamati mbalimbali, ambazo kwa njia moja ama nyingine zinahusika katika kuendesha ligi hiyo, zinatakiwa kufanya tathmini kwa yale yaliyopita.

Hakuna ubishi kuwa pamoja na kutojali uwezo wa kifedha, timu zilijitahidi sana hata zile ambazo hazina majina makubwa zilifanya vizuri uwanjani na kuvitoa jasho vigogo.

Lakini pamoja na uzuri wa msimu huo, bado kuna changamoto kibao zilizojitokeza, ambazo kwa kiasi fulani zilitia doa ligi hiyo, ambayo angalau ilikuwa na wadhamini waliosaidia timu kutoa lia njaa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

TFF wakati umefika sasa wa kuwa makini wakati wa upangaji wa ratiba na lazima mzingatie mazingira ya mikoa pamoja na miundo mbinu ya nchi yetu, ili kuziwezesha timu kucheza mechi zao bila tatizo.

Timu nyingi zililalamikia ratiba ambayo haikuwa rafiki kwani utakuta timu inacheza mchezo mmoja katika mkoa fulani ambao una timu zaidi ya moja halafu inaondoka na kurudi tena baadaye na kuzisababishia usumbufu na gharama zisizo za lazima.

Mfano mkoa wa Mbeya una timu mbili, hivyo timu ilitakiwa angalau inapokwenda icheze mechi zote mbili na ndipo iende mahali pengine ili iweze kubana matumizi na kutumia muda vizuri.

Mbali na kasoro hiyo ya upangaji mbovu wa ratiba, pia kulikuwa na kasoro zingine kama baadhi ya waamuzi kuchezesha ama kwa upendeleo au chini ya kiwango kwa kutojua sheria 17 za soka, ambazo ni muhimu.

Timu nyingi hasa zile ndogo zililalamikia sana waamuzi na wengi walidai kuwa walikuwa wakiumwa kwa makusudi ili kuzibeba timu kubwa na kuzipatia matokeo mazuri kwao.

TFF na wadau wengine wote wanatakiwa kujifunza kutokana na makosa ya msimu uliopita ili kuuboresha msimu ujao na kuifanya Ligi Kuu Bara kuwa ligi bora zaidi.

Ligi bora hutoa timu bora ya taifa, hilo halina ubishi, hivyo ni jukumu la TFF kuhakikisha ligi inakuwa bora ili kupata timu bora ya taifa itakayofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Chanzo: Kutoka Bodi ya Uhariri Gazeti la Habari Leo.

KUONDOKA KWA NGASA YANGA NI PENGO KUBWA KWA TIMU HIYO


KATIBU Mkuu wa klabu ya Yanga, Jonas Tiboroha amekiri kuondoka kwa mshambuliaji Mrisho Ngassa ni pengo kubwa kwa timu yao, lakini amewataka mashabiki na wanachama wa timu hiyo kuhakikisha wanapambana kumbakiza kiungo Haruna Niyonzima.
Tiboroha alisema ana uhakika watafikia makubaliano na kiungo huyo bora Afrika Mashariki katika siku chache zijazo ili aendelee kuichezea timu yao msimu ujao na kwa kushirikiana na nyota wengine waliopo na watakaowasajili.
Akizungumza na gazeti hili jana, Tiboroha alisema itakuwa wamefanya kosa kubwa endapo watamruhusu nyota huyo kuondoka kwani itakuwa ni pengo jingine baada ya Ngassa kuhamia Free State ya Afrika Kusini kwa mkataba wa miaka minne.
“Bado tupo kwenye mazungumzo na imani yangu kama Katibu Mkuu wa Yanga ni kwamba msimu ujao Niyonzima atabaki kuichezea Yanga kwa sababu mazungumzo yapo kwenye hatua nzuri na hata yeye mwenyewe ameonekana kutaka kubaki,” alisema Tiboroha.
Kiongozi huyo alisema wamekuwa na vikao virefu na viongozi wa juu wa Yanga kwa ajili ya kujadili suala la mchezaji huyo kwa lengo la kumalizana naye kwa kumpa kile alichowaomba kumboreshea katika usajili wake mpya na viongozi wamelipokea na kuahidi kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo.
“Sidhani kama kuna kitakachoshindikana kwa sababu pande zote mbili zimeonekana kuelekea kuelewana na kizuri ni kwamba Niyonzima mwenyewe ameonyesha nia ya kutaka kuendelea kubaki Yanga endapo tutamboreshea maslahi yake aliyoyahitaji kwenye mkataba mpya,” alisema.
Alisema mbali na Niyonzima pia wanatarajia kuanza mazungumzo na wachezaji wao wengine waliomaliza mikataba yao ambao wangependa kuendelea nao msimu ujao ili kuwapa mikataba mipya.
Tiboroha alisema baada ya kuondoka kwa Ngassa kocha wao Hans van der Pluijm, aliwataka kufanya kila linalowezekana nyota hao kuwabakisha kwenye kikosi hicho ili kikosi chake kisipoteze uwezo wa kutetea ubingwa wao msimu ujao.
“Kocha Pluijm ametushauri kuhakikisha tunawabakiza baadhi ya nyota wetu waliomaliza muda wao akiwemo Mbuyu Twite, makipa Ally Mustapha ‘Barthez’ Deogratius Munishi ‘Dida’ na Kelvin Yondani ili asipate tabu ya kuanza kujenga upya timu yake na kupata tabu katika mbio za kutetea ubingwa wake,” alisema Tiboroha.
Niyonzima ameonekana kuitikisa klabu ya Yanga akitaka wampe dola 50,000 kama pesa ya usajili ili kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea timu hiyo kwa miaka mingine miwili.









KAMANDA WA WAASI ADF KUREJESHWA UGANDA

Waasi wa kikundi cha ADF.
SERIKALI ya Tanzania inatarajia kumpeleka Uganda Kamanda wa Kikosi cha Waasi cha ADF cha Uganda, Jamil Mukumu aliyekuwa akitafutwa muda mrefu hapa nchini na Shirika la Kimataifa la Polisi (Interpol).

Atapelekwa Uganda baada ya taratibu za kumfikisha mahakamani kukamilika.

“Baada ya kukamatwa mtu huyo tuliwauliza Umoja wa Mataifa kama watamchukua, lakini walikataa njia iliyobaki sasa ilibidi tumfikishe mahakamani na kisha mahakama kwa kufuata sheria ya kubadilishana wafungwa na mahabusu atapelekwa Uganda kwenye mashitaka yake,” alisema Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Alisema utaratibu huo wa kumpeleka Uganda unafanyika kisheria kwa sababu ndio njia pekee iliyobaki.

Membe alisema pamoja na tukio la wanajeshi wawili kuuawa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na wengine 15 kujeruhiwa, wanajeshi wa Tanzania wanafanya kazi nzuri.

Kundi la waasi la ADF limejikita mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) na limehusika kuua wanajeshi wa Tanzania.


Chanzo: Habari Leo

ALBINO AKATWA VIUNGO KATAVI

Katavi. Mwanamke mmoja mwenye ulemavu wa ngozi, Remi Luchoma (30), Mkazi Kijiji cha Mwamachoma, wilayani Mlele amekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana na kutokomea nacho.

Luchoma alikatwa mkono juzi saa sita usiku akiwa nyumbani kwa wazazi wake na sasa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda.

Kaimu mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dk Joseph Mkemwa alisema majeruhi huyo anaendelea vizuri na matatibu.

Akisimulia tukio hilo, Luchoma alisema akiwa amelala chumbani, alishtukia akivamiwa na watu wawili baada ya mlango kuvunjwa.

“Walipoingia ndani walinishika na mmoja alitoa panga na kunikata kiganja cha mkono wangu,” alisema Luchoma.

Ndugu wa karibu wa Luchoma, Maliselina Jackson alidai kuwa alisikia kelele za kuomba msaada kutoka kwa dada yake na alipoamka aliwaona watu wawili wakitoka chumbani.

“Niliwaona watu wawili wakitoka chumbani alikolala dada wakiwa na kiganja cha mkono, nilipiga kelele za kuomba msaada,” alisema Jackson.

Alisema dada yake alishindwa kufungua mlango kwa vile watu hao waliufunga kwa nje hadi walipofika majirani na kufanikiwa kumtoa.

“Baada ya majirani kufika, tulitoa taarifa kwenye Kituo cha Polisi Majimoto na muda siyo mrefu askari walifika na kuanza msako,” alisema.

Chanzo: Mwananchi

ANGALIA TRELA YA MUVI MPYA 'MINIONS' KUTOKA UNIVERSAL


Movie mpya inayoitwa Minions imetengenezwa na kampuni kongwe kwa utengenezaji wa movie duniani, Universal. Itaoneshwa kwa mara ya kwanza kwenye sinema mnamo tarehe 10/07/2015. Imetengenezwa kwa wahusika ambao ni wanyama (Animated). Waongozaji wa movie hiyo ni Kyle Balda & Pierre Coffin ambapo Waandishi ni Ken Daurio & Brian Lynch na stering wa movie ni Chris Renaud, Pierre Coffin & Sandra Bullock. Waongozaji wa movie hii wamewahi kuongoza muvi inayoitwa Despicable Man. Tazama video hapo juu au bofya HAPA.


© VENANCE BLOG 2015.

ASTON VILLA YAPIGWA FAINI


Chama cha soka cha England FA, kimeipiga faini ya pound 200,000 klabu ya soka ya Aston Villa, kwa kitendo cha mashabiki kuvamia uwanja kwenye mechi ya robo fainali ya FA Cup dhidi ya West Bromwich Albion.
Katika mtanange huo uliopigwa March 7 kwenye dimba la Villa Park, mashabiki wa Aston Villa waliingia uwanjani wakati wachezaji walipopata majeraha na hata mwisho wa mchezo huku viti vikirushwa kutoka kwa mashabiki waliokuwa wamesimama mbali.
FA inasema klabu hiyo imeonywa vikali hasa juu ya mwenendo wake katika siku zijazo. Lakini kwa upande wao Villa waliomba msamaha baada ya mechi kuisha na kuongeza kuwa ushindi wao walioupata siku hiyo ulitiwa doa na vitendo vya wale walioshindwa kujizuia wao wenyewe.
Naye boss wa West Brom Tony Pulis amewakosoa walinda usalama wa uwanja huo na kuongeza kuwa usalam wa wachezaji wake ulikuwa mashakani.

TIMU ZA SEVILLA NA DNIPOPETROVSK ZATINGA FAINALI EUROPA LIGI

Mashabiki wa timu ya Dnipopetrovsk wakiishangilia timu yao.
Nusu fainali ya pili ya Europa ligi iliendelea usiku wa kuamkia leo wakati Dnipopetrovsk ilipomenyana na Napoli huku Fiorentina ikiialika Sevilla. Hadi mwisho wa michezo yote miwili, Dnipro imeingia fainali kwa jumla ya bao 2 kwa 1 bada ya jana kushinda bao 1-0.
Nayo Fiorentina imetupwa nje kwa jumla ya bao 5-0 baada jana kuzabuliwa bao mbili nyumbani walipocheza dhidi ya Sevilla.
Fainali itapigwa mnamo May 27 huko nchini Poland kati ya Sevilla dhidi ya Dnipropetrovsk.

HALI BADO NI TETE NCHINI BURUNDI

HALI ya Burundi imezidi kuwa tete huku makundi mawili hasimu ya wanajeshi, yamekuwa yakipigana, kila moja likitaka kutawala jiji la Bujumbura.

Mapigano hayo ni kati ya wanajeshi wanaomtii Rais Pierre Nkurunziza, ambao wanapambana na wanajeshi wanaompinga, ambao wanamuunga mkono mwanajeshi aliyetangaza mapinduzi, Meja Jenerali Godefroid Niyombare.

Ofisa Mwandamizi wa Jeshi nchini humo, alisema wanajeshi wanaomtii Rais Nkurunziza wamefanikiwa kudhibiti na kurejesha maeneo muhimu ya jiji hilo chini ya utawala wa Serikali, ukiwamo uwanja wa ndege.

Hata hivyo, viongozi wa wanajeshi wanaompinga Rais huyo, wameendelea kudai kuwa wameipindua Serikali ya nchi hiyo.

Hali ya machafuko nchini humo, ilianza baada ya kiongozi huyo kutangaza kuwa ana nia ya kuwania tena kipindi cha tatu cha urais, jambo ambalo wapinzani nchini humo wamedai ni kinyume cha Katiba.

Kwa mujibu wa mashuhuda nchini humo, milio ya risasi na mabomu imekuwa ikisikika usiku kucha kuanzia juzi katika mapigano baina ya vikosi vinavyomtii Rais na vile vinavyotaka mapinduzi, lakini hadi sasa haijafahamika nani aliyefanikiwa kulidhibiti jiji hilo.

“Hatujaweza kulala kutokana na hofu tuliyonayo, milio ya milipuko na risasi imekuwa ikisikika kila sehemu, watu anaogopa kwa kweli,” mmoja wa mashuhuda aliwaambia waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari ndani ya kikosi kinachomtii Rais Nkurunziza, jeshi hilo limeweza kurejesha maeneo muhimu chini ya Serikali kama vile Ikulu, Redio na Televisheni ya Taifa na uwanja wa ndege.

Mitaa ya jiji hilo imejaa askari na polisi wanaomtii Rais na hadi majira ya jioni uwanja wa ndege, ulifunguliwa tayari kwa kutoa huduma za usafiri.

Hata hivyo, bado mapigano yanaendelea eneo ambapo televisheni na redio za taifa zipo, huku vikosi vinavyotaka mapinduzi vikijaribu kuingia ndani ya vituo hivyo vya habari.

Kila kikundi kinataka kudhibiti vituo hivyo vya utangazaji wa taifa, kwa kuwa ndio vyombo vya habari pekee vyenye uwezo wa kusikika hadi nje ya jiji hilo la Bujumbura.

Tayari Mkuu wa Majeshi na Rais Nkurunziza wametangaza na kudai kuwa jaribio la kupindua nchi hiyo, limeshindikana.

Hata hivyo, kauli hizo zimekuwa zikipingwa na viongozi wanaotaka mapinduzi nchini humo, na mmoja wao alisema kuwa wamefanikiwa kudhibiti takribani mji wote wa Bujumbura.

Msemaji wa kundi hilo la waasi, Venon Ndabaneze, alisema askari wanaotawanywa katika jiji hilo, wote wako upande unaotaka mapinduzi na si wanaomtii Rais Nkurunziza.

Juzi, Meja Jenerali Godefroid Niyombare, aliyekuwa Mkuu wa Usalama, alitangaza kumpindua Rais Nkurunziza akiwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, hali iliyozua shangwe kwenye mitaa mbalimbali jijini humo.

Niyombare alifukuzwa kazi na Rais Nkurunzinza Februari mwaka huu. Majengo ya kituo cha binafsi cha Televisheni Renaisance ya Burundi, iliyotumiwa na Meja Jenerali Niyombare, yameripotiwa kuharibiwa vibaya usiku wa kuamkia jana.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kituo hicho, Innocent Muhozi, moja ya ofisi zake ilichomwa moto usiku huo na kusababisha kila kilichokuwepo ndani kuteketea.

Jenerali Niyombare, alitoa tangazo hilo, saa chache tu baada ya Rais huyo kupanda ndege kwenda Dar es Salaam Tanzania kuhudhuria mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliojadili suala hilo la Burundi.

Hata hivyo, iliripotiwa kuwa baada ya tangazo la kupinduliwa kwake, Nkurunziza, alirejea Burundi bila kuhudhuria mkutano huo, lakini alipofika Bujumbura alilazimika kurejea Dar es Salaam baada ya Uwanja wa Ndege wa Bujumbura kufungwa.

Habari zilizopatikana kutoka BBC baadaye jana jioni zilidai wanajeshi watano walikuwa wameuawa, silaha nzito zilikuwa zikitumika, mirindimo ya risasi ilisikika kila kona na waandamanaji walilazimika kujifungia ndani.

Ofisa Mwandamizi wa Usalama wa Taifa kutoka Ikulu ya Dar es Salaam, alipozungumza na AFP, alikiri kuwa Rais Nkurunziza bado yupo Tanzania, jijini Dar es Salaam, lakini haifahamiki ni sehemu gani alipo.

Nkurunzinza yuko wapi?

Suala sehemu alipo Rais Nkurunziza baada ya kufanyika ribio la kumpindua nchini kwake, limeendelea kuwa tete baada ya Tanzania kusema haijui alipo.

Hatua hiyo imetokana na tetesi kuwa Rais huyo yupo nchini baada ya kuhudhuria mazungumzo ya kutafuta amani kwa marais wa nchi za Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam na baadaye kutangazwa nchi hiyo kupinduliwa na kueleza kushindwa kurejea nchini mwake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo.

Awali , alipoulizwa alipo Rais huyo, alisema hawezi kujibu swali hilo lakini baadaye alisema hajui huku akiondoka na kucheka.

Membe alisema baada ya tamko la viongozi wa nchi za Afrika Mashariki, kulaani jaribio la kufanya mapinduzi katika nchi hiyo zaidi ya hayo Baraza la Mawaziri lililokutana kwa siku mbili Jumanne na Jumatano, litakutana tena Jumatatu wiki ijayo na kufanya tathmini ya hali halisi ya Burundi kwa siku tatu hizi mpaka Jumatatu.

“Kwa sasa sitaweza kuzungumza jambo jingine lolote kuanzia sasa mpaka Jumatatu jioni baada ya kikao cha baraza la mawaziri wenzangu, ambapo tutajua mambo ya kuzungumza.”

“Naomba kuwatahadharisha Watanzania kuwa hali ni tete Burundi lolote unalosema wewe na kudhani dogo linaweza kugharimu maisha ya mtu naomba mnielewe na mkae mkielewa haya mengine tutazungumza siku hiyo ya Jumatatu,” alisisitiza.

Alisema wananchi wa Burundi wako katika matatizo na vizuri kuvuta subira, badala ya kuendelea kuzungumza, kwani uhai wa mtu unaweza kuwa matatani.

Membe alipoulizwa alipo Rais wa Burundi, kwani inasemekana alirudi nchini Tanzania baada ya ndege yake kushindwa kutua nchini kwake , alisema yeye hajui.

Alisema hali ya Burundi ni tete na sababu hiyo, walikutana kutafuta ufumbuzi wa kudumu na wananchi waache kufanya ghasia na badala yake watulie na kuchagua viongozi wao kwa amani.

Alisema imeelezwa kuwa jaribio la jana la baadhi ya askari kutaka kuipindua Burundi, lililaaniwa na viongozi wote wa Afrika. Alisema Afrika haitaki nchi yoyote, kwa sababu zozote, kuhalalisha kuchukua madaraka kwa njia ya mtutu wa bunduki.

Wakimbizi wafa kwa kipindupinduKigoma

Wakati hali ya utawala nchini Burundi ikiwa tete , wakimbizi wa nchi hiyo waliopo mkoani Kigoma, wameanza kupatwa na majanga mengine baada ya kuripotiwa watu wanne kufa kwa ugonjwa wa kipindupindu.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Leonald Subi alisema mjini Kigoma kwamba watu wawili walikufa wakiwa tayari wanaumwa ugonjwa huo na kufariki hapa nchini.

Alisema watu wawili wengine, walipatwa na ugonjwa huo wakisubiri msaada wa kibinadamu katika kijiji cha Kagunga wilaya Kigoma, mwambao wa Kaskazini wa Ziwa Tanganyika.

Subi alisema kuwa kwa sasa hali ya upatikaji wa huduma za kibinadamu, ikiwemo chakula, maji, mahala pa kujihifadhi na huduma ya choo ni mbaya sana kutoka na idadi kubwa ya wakimbizi hao kuwepo kijijini hapo kwa kipindi kifupi na hivyo kijiji hicho kuzidiwa katika kuwapatia huduma watu hao.



Chanzo: Habari Leo

WATU 23 WANADAIWA KUUAWA NA WAASI WA UGANDA HUKO DRC

Maafisa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanasema kuwa watu ishirini na watatu wameuawa kikatili na wanaodaiwa kuwa waasi wa Uganda.
Wanane kati ya waliofariki ni wanajeshi wa DRC.

Shambulizi hilo lilifanyika Jumatano usiku.

Waasi wengi wao wakiwa wa Allied Democratic Forces (ADF) wamefanyana mashambulizi kadhaa kusini mwa mji wa Beni katika siku za hivi karibuni.
Umoja wa mataifa unasema kuwa huenda walifanya makosa ya uhalifu wa kivita na vitendo vinavyokiuka ubinadamu
.
ADF imewaua mamia ya watu wakati mwingine na ndo, panga na visu.



Chanzo: BBC

MVUA ZINAZOENDELEA DAR ES SALAAM KUPUNGUA MAKALI JUMAMOSI HII

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua za mfululizo zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam zitaendelea kunyesha na kwamba zinatarajia kupungua mwishoni mwa wiki hii.

Taarifa hiyo inaweza kuwa habari njema kwa wakazi wa Dar es Salaam na miji mingine iliyoathirika kwa kiasi kikubwa na mvua hizo zilizonyesha mfululizo na kusababisha vifo, uharibifu wa mali na miundombinu, huku hali ya usafiri, upatikanaji wa bidhaa hasa za vyakula ikiwa ngumu katika maeneo mengi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa  Huduma za Hali ya Hewa kwa Jamii wa TAM, Hellen Msemo alisema mvua hizi zinatarajia kupungua mwishoni mwa wiki hii; lakini sio kuisha kabisa na kwamba kwa sasa wananchi waendelee kufuatilia taarifa zinazotolewa.

“Mvua hizi zitaendelea kunyesha mpaka Ijumaa ya wiki hii na tunaweza kuona jua kidogo Jumamosi lakini sio mvua za kukatika kabisa zitaendelea kunyesha kidogo kidogo,” alisema Msemo.

Shule zajaa maji

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msasani ‘B’, Jane Reuben alisema mvua zinazoendelea kunyesha zimeathiri kwa kiasi kikubwa mahudhurio ya wanafunzi shuleni hapo huku wengine wakichelewa kufika darasani.

Gazeti hili lilishuhudia hali tete katika shule ya Msingi Msasani ‘A’ ambapo baadhi ya madarasa yamejaa maji na kushindwa kutumika na kuwalazimu wanafunzi kuchangia vyumba vya madarasa.

Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wengi wanaosoma katikati ya jiji wameshindwa kufika shuleni kwa kuhofia usumbufu wa usafiri kutokana na mvua ambayo imekuwa ikiendelea kunyesha.

Baadhi ya shule katika Kata ya Goba zimefungwa kwa muda kutokana na athari za mvua hizo. Foleni zawa kero Mvua hizo pia zimeendelea kuleta usumbufu mkubwa katika barabara nyingi za Dar es Salaam kutokana na kuharibika na kusababisha msongamano unaowafanya wakazi wa jiji hilo kupata wakati mgumu wa kuyafikia maeneo mbalimbali ama kikazi au shughuli binafsi.

HabariLeo ilishuhudia maeneo ya Posta Mpya katika barabara za Samora Avenue, Mkwepu, Ocean Road, Uhuru na zile zinazoelekea Magomeni na Mwenge zikiwa na msongamano wa magari.

Bidhaa bei juu Kwa upande wa bidhaa katika masoko, bei zimepaa na kusababisha kuongezeka kwa ukali wa maisha miongoni mwa wakazi wa Dar es Salaam.

Katika soko la Kariakoo, mfanyabiashara Baraka Lisulile anayeuza karoti alisema kabla ya mvua kilo moja ilikuwa inauzwa kwa Sh 2,000 lakini sasa imefikia Sh 3,000.

“Vile vile kabla ya mvua hizi kunyesha tenga la nyanya lilikuwa ni kati ya Sh 20,000 hadi Sh 35,000 lakini hivi sasa ni kuanzia Sh 48,000 hadi Sh 50,000,” alisema mfanyabiashara huyo.

Bidhaa za unga, mchele, maharage na aina nyingine za vyakula, nazo ziko juu. Nyumba zabomoka Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Musa Natty alisema mvua hizo zimefanya wananchi kukumbwa na uharibifu mkubwa ambao ni nyumba kufurika maji, kubomoka na barabara na madaraja kukatika.

Alisema katika manispaa hiyo maiti nne za wanaume na mwanamke moja zimepatikana na zimeripotiwa kata za Wazo Kunduchi na Mbezi beach.

Katika manispaa hiyo pia eneo la Africana nyumba zimejaa maji huku maeneo ya Nyaishozi kaya 151 zinahitaji msaada wa haraka ikiwemo mahema na chakula.

Alisema kata ya Tandale maeneo ya bondeni maji yameingia katika mitaa ya Pakacha, kwa Tumbo, Mahalitani, Sokoni, Mtogole na kwa Mkunduge.

Nyumba 14 ndizo zilizoathirika kwa kubomoka ambapo wakazi wake wamehifadhiwa na majirani.

Kata ya Kwembe watu 23 wamepata majeraha baada ya nyumba kuezuliwa paa, Shule ya Msingi King’azi ambayo inamilikiwa na Manispaa nayo imepata maafa ya kutitia na kutoa ufa kati ya lenta na paa.

Kata ya Mbweni familia 128 zimeathirika kwa kuzungukwa na maji na kukosa makazi na kuhifadhiwa na majirani na kata ya Magomeni mwili wa mtu mmoja umeopolewa akiwa amekufa, katika mtaa wa Suna watu 450 wamekosa makazi na mtaa wa Makuti A watu 250 hawana makazi na wanahifadhiwa na majirani.

Mtaa wa Idrisa watu 180 hawana makazi na nyumba nyingine 450 kuzingirwa na maji Kata ya Mabwepande daraja la mto Nyakasangwa mtaa wa Mbopo limekatika na kutitia hakuna mawasiliano kati ya pande mbili na barabara ya kwenda Mabwepande imekatika karibu na njia panda iendayo kwa waathirika wa Mji Mpya na nyumba 20 zimezingirwa na maji.

Kata ya Hananasif nyumba 400 ambazo ziko mabondeni zimezungukwa na maji na wakazi wa nyumba hizo wamehama makazi yao. Nyumba hizo ni zile zilizopo bondeni ambazo zilizobaki baada ya kubomolewa na wamiliki kupelekwa Mabwepande.

Kata ya Mabibo daraja la Tasaf linalounganisha Kata ya Mabibo na Makuburi limekatika kwa sababu ya wingi wa maji pamoja na nyumba tisa na vyoo.

Kata ya Manzese kumeripotiwa kifo cha mtu mmoja na kubomoka kwa nyumba moja. Daraja la linalounganisha kata ya Mbezi juu kwa Londa na Makongo kukatika.

Kata ya Wazo mtaa wa Mivumoni nyumba 13 zimeezuliwa na upepo mkali na Kata ya Kawe Mtaa wa Mzimuni nyumba 64 zimebomoka na nyingine kuzunguka na maji.

Kata ya Makumbusho mwili wa mtu mzima miaka 45 umeokotwa na waathirika 109 waliobomokewa na nyumba na zingine kujaa maji wamehifadhiwa shule ya msingi Kisiwani ambao wanahitaji msaada.

Kata ya Msasani Shule ya msingi msasani A imejaa maji katika madarasa 7 na nyumba za walimu na shule imefungwa kwa muda, Kata ya Sinza maji yamejaa yanaelekea katika makazi ya watu huku mtaa wa Barafu nyumba 3 zimebomoka na watu kukosa makazi huku nyumba 275 zimezungukwa na maji na kuhatarisha makazi.

Kata ya Mwananyamala katika mitaa ya Msisiri A na Msisiri B, Bwawani na mtaa wa Mwinyijuma jumla ya nyumba 150 zimezingirwa na maji na kuleta taabu kwa wakazi wake.

Kata ya Makuburi nyumba mbili zimebomoka na daraja la waenda kwa miguu linalounganisha Kata za Makuburi na Kimara kusombwa.

Kata ya Kimara familia saba zimehamia katika Kituo cha Polisi cha Kilungule A baada ya nyumba yao kujaa maji na kukatika, Kata ya Mizimuni nyumba tano zimevunjika kuta na kaya 15 zimehamia kwa majirani huku kaya 30 nyumba zake zimezingirwa na maji.

Kufuatia maafa hayo, Halmashauri imechukua jitihada mbalimbali ili kuokoa maisha ya watu na kuwawezesha kurudi katika makazi yao. Jitihada hizo ni pamoja ni kununua pampu za kunyonya maji ambayo yamezunguka makazi ya watu.Kazi hiyo ya kunyonya maji imeanza pamoja na kuzibua mitaro.




Chanzo: Habari Leo