CHADEMA 'YAIBIPU' POLISI
Ni wazi sasa kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeamua kujipima nguvu na Jeshi la Polisi baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kutangaza kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima kuanzia Septemba mosi, mwaka huu.
Kamati Kuu hiyo katika maazimio yake yaliyosomwa kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, ilisisitiza kuwa azma yake hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kupinga agizo la jeshi hilo la kuzuia kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.
Sababu nyingine zilizoisukuma Kamati Kuu kufikia azma hiyo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe ni pamoja na kupinga zuio la urushwaji wa moja kwa moja wa mijadala ya Bunge, kupinga wabunge wa upinzani kudhibitiwa bungeni, kuingiliwa kwa mhimili wa mahakama, upuuzwaji wa utawala wa sheria na haki ya kupata habari.
Katika hatua nyingine, Kamati Kuu ya Chadema imezindua operesheni Ukuta yenye lengo la kupambana na kile ilichokiita kuwa ni udikteta nchini, huku ikitangaza kushirikiana na wale tu watakaoona umuhimu wa kuwepo kwa haki na demokrasia nchini.
Mbowe aliyeambatana na viongozi mbalimbali wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, aliagiza maagizo hayo kupewa umuhimu na ngazi zote za chama hicho kuanzia vijiji, kata, majimbo, wilaya, mikoa, kanda, mabaraza hadi taifa.
Alisema Jeshi la Polisi nchini limeamua kuvidhibiti vyama vya siasa ili visiweze kufanya mikutano ya kisiasa, wakati serikali inaongozwa na viongozi ambao ni wanasiasa na ambao wamekuwa wakifanya kazi zao za kisiasa kupitia nafasi zao za kiserikali.
Mwenyekiti huyo wa Chadema Taifa alisema katika maandalizi ya mikutano hiyo, chama hicho kitafuata taratibu, kanuni na sheria zinazostahili ili waweze kupata ruhusa huku akisisitiza kwamba si nia ya chama hicho kuanzisha vurugu, bali kutumia haki ya msingi ya kukosoa akisema ndiyo njia sahihi ya kufuatwa katika ukuzaji wa haki na demokrasia nchini.
Alisema Kamati Kuu imeagiza ngazi zote za chama kuanzia ngazi ya msingi, kata, majimbo, wilaya, mikoa, kanda, mabaraza na Taifa kukaa vikao vyake vya kikatiba haraka na ajenda za vikao hivyo iwe ni kujadili maandalizi ya mikutano hiyo ya hadhara, kujadili hali ya siasa na pia hali ya uchumi nchini.
Alisema Kamati Kuu imewataka wanasheria wa chama hicho wakiongozwa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kukaa na kuyatazama mambo yote ambayo yametokea na kuchukua hatua za kisheria kwa lengo la kuyatafutia suluhisho la kisheria.
“Inaonekana kwamba wao ndio wana haki lakini sio sisi. Viongozi wetu wakubali kukosolewa na waamini kuwa taifa ni letu sote, hali ya sasa imesababisha Taifa kuwa lenye uoga wa kupindukia,” alisema na kuongeza kuwa Septemba mosi ni siku ya kukata misingi ya uonevu wa demokrasia.
Kuhusu ni nini kitazungumzwa na viongozi wa chama hicho katika mikutano hiyo ya hadhara Mbowe alisema kwa kifupi; “Lazima tufanye mikutano ya hadhara. Tutaelezana namna ya kukatiza mto pindi tutakapoufikia.
” Kuhusu operesheni Ukuta, Mbowe alisema jana ni siku ya kwanza ya utekelezaji wa operesheni hiyo yenye maana ya ‘Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania’ huku akisisitiza kuwa inatokana na chama hicho kutokuwa tayari kuruhusu nchi kuongozwa nje ya misingi ya demokrasia.
Alisema kupitia operesheni hiyo chama hicho kitashirikiana na wale wote ambao wanaona umuhimu wa kuzingatiwa kwa misingi ya haki na demokrasia, na kuongeza kuwa hiyo haina maana kwamba chama hicho hakiungi mkono hatua za serikali katika kupambana na matendo maovu nchini.
Kauli yapingana na agizo la Polisi
Msimamo huo wa Chadema ni wazi kwamba sasa utakifanya chama hicho kukabiliana na Jeshi la Polisi ambalo limezuia kufanyika kwa mikutano ya hadhara kwa vyama vyote vya kisiasa nchini.
Agizo hilo la Jeshi la Polisi lilitolewa na Kamishina wa Polisi Operesheni na Mafunzo kutoka Makao Makuu ya jeshi hilo, Nsato Mssanzya. “Katika siku za hivi karibuni, Jeshi la Polisi nchini, limepokea taarifa kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa wakitaka kufanya mikutano na maandamano.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi kupitia vyanzo vyake mbalimbali vya habari limebaini kuwa mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi.
“Aidha vyama vingine vya siasa vimeonesha dhamira ya kupinga kile ambacho kitasemwa na wapinzani wao. Vyanzo hivyo vya habari vimebainisha kwamba upo uwezekano mkubwa wa kutokea vurugu baina ya makundi mawili ya kisiasa.
“Kwa hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini linapiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara kuanzia Juni 7, mwaka huu hadi hapo hali ya usalama itakapotengemaa. Jeshi la Polisi linawataka wanasiasa kuacha mara moja kuwashinikiza wananchi kutotii sheria za nchi. “Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua kali za kisheria mtu yeyote au chama chochote cha siasa kitakachokaidi agizo hili.
Aidha Jeshi la Polisi linawataka wananchi kuwa makini na wanasiasa wenye lengo la kutaka kuvuruga amani ya nchi hii na badala yake linawasihi waendelee kushirikiana katika kujenga umoja wa nchi hii,” alisema Kamishna Mssanzya katika agizo hilo la Jeshi la Polisi.
Katika tukio jingine, Mwandishi Wetu John Mhala kutoka Arusha anaripoti kwamba wabunge wawili na wenyeviti wawili wa Chadema wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa kufanya mkutano wa hadhara katika Wilaya ya Karatu bila ya kibali.
Waliokamatwa na polisi ni pamoja na Mbunge wa Karatu, Willey Kaboroo (58) na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha kupitia chama hicho, Cecilia Pareso (35).
Wengine waliokamatwa na kuhojiwa na polisi Arusha kwa zaidi ya saa tatu ni pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Jubilet Mnyenye (55) na Makamu wake Lazoro Kajuta ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ganako.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Yusuph Ilembo alisema kuwa viongozi hao walifanya mkutano wa hadhara Julai 23, mwaka huu, bila kufuata tararibu kama inavyotakiwa.
Kamanda Ilembo alisema wabunge hao na wenyeviti hao wa halmashauri waliamua kukiuka taratibu za kufanya mkutano wa hadhara hivyo polisi iliamua kuwaita na kuwahoji sababu za kushindwa kufuata tararibu.
Alisema wamefunguliwa jalada la uchunguzi na wote wamehojiwa na kuachiwa kwa dhamana yao wenyewe na upelelezi wa shauri hilo unaendelea.
Hata hivyo, wabunge hao na wenyeviti baada ya kuhojiwa walisema kuwa wamesikitishwa na hatua ya kuitwa polisi na kuhojiwa kwa kufanya mikutano ya hadhara wakati Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu alikuwa anajua kila kitu.
Chanzo: Habari Leo
Comments
Post a Comment