WAKOREA KASKAZINI WAAGIZWA KUNYOA KIDUKU
Wanaume Korea Kaskazini wanakabiliwa na mtihani mpya katika taifa lao; wa kunyoa nywele kwa mtindo ulioamuliwa na rais wao. Watake, wasitake kuanzia sasa kila mwanamume atalazimika kunyoa nywele zake kwa mtindo anaoupenda Rais Kim Jong- un. Kiongozi huyo kijana, aliyerithi wadhifa huo baada ya kifo cha baba yake, hana mzaha hasa kutokana na nia yake ya kujenga mfumo mpya wa utawala ambao matakwa yake tu ndiyo ya kufuatwa. Ni wiki mbili sasa tangu serikali ya nchi hiyo kutoa agizo linalowataka wanaume kunyoa kama rais wao, huku wanawake nao wakielekezwa kutengeneza nywele zao kwa aina 18 tofauti na si zaidi ya hapo. Hilo ni moja ya maagizo yenye utata kuwahi kutolewa chini ya utawala wake, ambapo amekuwa akifanya jitihada za kujijengea mizizi, ikiwamo kuwaondoa na kuwaadhibu wale waliokuwa katika utawala wa baba yake wanaoonekana kutokubaliana na aina yake ya uongozi.