MAMBO YA MUHIMU KUFAHAMU NA KUZINGATIA KABLA YA KUCHAGUA KOZI (TAALUMA) CHUO KIKUU
Picha kwa hisani ya Debt.org |
1.0 UTANGULIZI
Nilipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu nilisikia manung'uniko miongoni mwa wanafunzi wenzangu wengi wa vyuo vikuu ambayo yalitokana na taaluma wanazosoma. Kuna sababu kadha wa kadha zinazopelekea manung'uniko hayo miongoni mwa wasomi hawa tukiachilia mbali suala la ucheleweshwaji wa mikopo miongoni mwa wasomi hawa (kwa sasa changamoto hii inapungua kadiri siku zinavyosonga). Tatizo lingine ambalo linawasumbua wasomi hawa ni suala la uchaguzi wa taaluma gani akaisome Chuo Kikuu.
Uchaguzi wa taaluma (career choice) ni jambo nyeti sana na la kuzingatia kwa muhitimu yeyote wa elimu ya kuanzia kidato cha nne. Jamii yetu ya Tanzania haifahamu kwa undani kuhusu umuhimu wajambo hili lakini huku ndiko msingi hundaliwa. Mtu anapohitimu kidato cha nne na kupata ufaulu wa kujiunga na masomo ya kidato cha tano ama ngazi ya astashahada (certificate) na stashahada (diploma) hapo ndipo uchanguzi wa taaluma huanza. Kwa kuandika makala haya ninakusudia kutoa hamasa kwa wazazi na walezi na jamii kwa ujumla kuwasaidia vijana hawa katika uchaguzi wa taaluma zao za baadaye kulingana na uwezo wao na mambo wanayoyapenda.
Uchaguzi wa taaluma huanza na uchaguzi wa michepuo/tahasusi (combination) anayokwenda kuisoma mwanafunzi shuleni. Hii huathiri kwa kiasi kikubwa taaluma yake kwa namna chanya ama hasi. Hapa ninamaanisha kwamba mchepuo atakaosoma una uhusiano mkubwa na taalumza zianzofundishwa chuo chuo kikuu ama kutokuwa na uhusiano kabisa.
Kuna mambo kadhaa
ambayo huwaathiri wanafunzi wawapo vyuo vikuu kwa kutozingatia uchaguzi wa
taaluma. Mambo hayo yaweza kuwa; kutoendelea na masomo ya Chuo Kikuu kutokana
na kufeli masomo (Discontinuation from studies), kufeli majaribio mara kwa mara
kutokana na kutoridhika na kile wanachosomea ama ugumu wa masomo. Sababu kubwa
hapa zaweza kuwa tatu; kwanza, uchaguzi wa taaluma kwa kufuata mkumbo wa
marafiki pili, kushawishiwa ama kuchaguliwa taaluma na mzazi ama mtu yeyote
aliyesoma taaluma husika na kupata mafanikio kwa hivyo na mchaguaji anaona naye
asome taaluma husika ili afanikiwe na tatu, ni upepo wa upatikanaji wa mkopo
kwa vyuo vikuu.
Tuwapo shuleni hasa kidato cha 5 & 6 wanafunzi wengi hua na ndoto kubwa sana wakati mwingine kuliko hata kutambua uwezo wao uko katika mambo yepi. Hili husababishwa na marafiki, suala hili linaitwa mkumbo. Kwa mfano wanafunzi wengi wa Kidato cha Sita hubagua taaluma za kusoma kutokana na matakwa yao bila kutambua uwezo wao. Wapo wengine ambao hawafikirii chochote zaidi ya kusikiliza marafiki zao wanataka kusoma taaluma zipi (mkumbo) matokeo yake baadaye wakiwa vyuoni huanza kujilaumu ama baadaye hushindwa kuendelea na masomo yaani 'Discontinuing from studies'.
Jambo lingine ni kushawishiwa ama kuchaguliwa taaluma ya kusoma na wazazi/mlezi; mara nyingi wazazi/mlezi huwalazimisha vijana wao wakasome taaluma fulani bila kutambua uwezo wa kijana husika. Lakini pia kwa sababu mzazi/mlezi kufanikiwa katika taaluma husika anamlazimisha kijana asome taaluma aliyosoma yeye. Wakati mwingine wazazi hualazimisha kabisa kwamba vijana wao wasipofuta maagizo wanayoambiwa watajijua wenyewe. Jambo hili huwa ni zito na changamoto sana kwa sababu wazazi/walezi mara nyingi ndiyo hugharamia fedha za masomo vijana wao wawapo masomoni.
Vilevile kuna suala la upatikanani wa mkopo. Hili ni suala ambalo linawalazimu wengi kusoma taaluma fulani Elimu/Ualimu wa Sayansi, Udaktari, Uuguzi na Uhandisi n. k. kwa sababu ya upatikanaji mkopo wa serikali ama ufadhili wa masomo. Wengi wao huchelewa kukubaliana na hali hii, lakini baadaye pia kutokana na ufadhili wa serikali hujikuta hawana namna kwa sababu ya hali ya familia kutoweza kugharamia masomo. Wengine hugundua mambo fulani katika taaluma husika na kuamua kukubaliana na hali na kuendelea na masomo. Huu ni mfano tu ila katika taaluma nyingine ambazo sijazitaja wapo wenye mambo kama haya.
2.0 MAMBO YA MUHIMU KUZINGATIA WAKATI WA KUCHAGUA TAALUMA
Kuna mambo kadhaa
unaweza kuyazingatia katika suala zima la kuchagua taaluma ya kusoma Chuo Kikuu,
mambo hayo yaweza kuwa yafuatayo:
2.1. UJUZI ULIO NAO AMA KIPAJI
Japokuwa kuna
baadhi ya taaluma haziihitaji ujuzi sana ni muhimu kutambua kuwa suala la ujuzi
ni la muhimu katika kipi usomee. Mathelani ujuzi katika lugha, hesabu ama kuwa
na uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu. Ujuzi ulio nao wewe utakusaidia kusoma vyema taaluma
yako na kuifurahia huku ukiunoa zaidi ujuzi huo. hili pia linawahusu wenye
vipaji, unaposoma taaluma inayokuza kipaji chako basi inekujenga zaidi kuwa na
mtazamo mpana kuhusu kipaji na ndoto yako.
2.2. MAMBO UPENDAYO
Baada ya kugundua
ujuzi ama uwezo ulio nao, suala linalofuata ni kufahamu unapenda kufanya nini
katika maisha yako baada ya kumaliza masomo. Lengo lako linatakiwa liwe kufanya
jambo ambalo unalipenda, hii itakusaidia katika kuridhika na kuyafurahia masomo
yako kwa kipindi chote utakochokuwa masomoni, utasoma kwa furaha sana na
utakuwa umeridhika. Sanjari na hapo itakusaidia kujijenga vizuri kitaaluma na
kukunoa vyema.
2.3. TAFUTA KITABU CHA CHUO KINACHOELEZEA KUHUSU CHUO (PROSPECTUS)
Prospectus ni
kitabu kinachoelezea mambo yote ya msingi unayopaswa kuyafahamu kuhusu chuo.
Kitabu hiki kinaelezea vizuri kuhusu taaluma mbalimbali zinazotolewa na chuo
husika, hii inajumuisha na kozi ndogondogo ambazo hufundishwa kwa muda wote wa
masomo kuanzia semista ya kwanza hadi ya mwisho. Kitabu hiki pia huonesha
taarifa za kifedha kama ada inayotakiwa kulipwa kwa kila taaluma na michango mingine
ya chuo. Muhimu zaidi kupitia kitabu hiki cha mwongozo ni kufahamu kuhusu taaluma
utakayopenda kuisoma. Hapo utalinganisha uwezo wako katika taaluma, yaani taaluma zipi
utazimudu na zipi zinahitaji uongeze bidii. Pia kitabu hiki huwa na sifa za
chini za kujiunga na masomo katika kila taaluma (mimimum entry qualification)
hizi zinategea sana ufaulu wako wa Kidato cha Nne, Sita ama Diploma. Huna sababu
ya kupata nakala ngumu ama kupiga simu kwenye chuo husika kwa sababu kitabu
hiki huwekwa katika tovuti ya kila chuo.
2.4. PITIA KITABU CHA MWONGOZO CHA TCU (TCU GUIDEBOOK)
Kitabu hiki
hutolewa kila mwaka wa masomo na Tume ya Vyuo Vikuu nchini. Hiki huwa na
taaluma zinazotolewa na kila chuo pamoja na vigezo husika katika kila taaluma
pamoja na ada yake. Taaluma ama chuo kisichokuwepo katika kitabu hiki huwa
hakiruhusiwi kufanya udahili kwa mwaka husika. Katika kitabu hiki utakutana na
vigezo vya chini ambavyo unatakiwa kukidhi ili kuingia katika ushindani wa
taaluma husika. Mara nyingi ushindani unategemea na ufaulu wako kidato cha nne
na kidato cha sita ama Diploma; jinsi ulivyofaulu vizuri ndivyo jinsi utakuwa
katika nafasi za juu zaidi kuchaguliwa katika taaluma na chuo ulichotuma
maombi. Vitabu vya Mwongozo hutolewa tofauti kwa Wahitimu wa Kidato cha Sita,
Diploma wale wa Kutambuliwa kwa Kujifunza hapo Awali [Recognition for
Prior Learning (RPL)]. Kila kimoja huainisha sifa kulingana
na elimu husika.
2.5. CHAGUA TAALUMA UNAZOPENDA KULINGANA NA UWEZO NA VIPAUMBELE VYAKO
Katika hatua hii
unatakiwa kuorodhesha taaluma unazotaka usoma. Kumbuka katika uchaguzi wako huo
ni taaluma moja tu utatakiwa kusoma ama kwa kupangiwa na chuo kutokana na uchaguzi
wako. Hili lisikupe shida kwa sababu wakati mwingine unaweza kubadili ukifika
chuo ili mradi tu unavyo vigezo. Kuna baadhi ya vyuo huruhusu kubadili taaluma
mwanzoni mwa semista ya kwanza. Vingine haviruhusu hivyo kama hujaipenda zaidi taaluma
hiyo, unaweza kuahirisha mwaka wa masomo ama kuhama chuo. Nasisitiza kufanya
uchaguzi sahihi zaidi ili kuepukana na kadhia hizo.
2.6. USIFIKIRIE SANA KUHUSU UPATIKANAJI WA
AJIRA
Wengi wetu
tunasoma kwa kufikiria upatikanaji wa ajira, kwamba baada ya masomo tuuajiriwe
ni sahihi pia lakini jambo la muhimu kwa sasa ni kusoma na kutengeneza wasifu mzuri
katika masomo huku ukinoa kipaji na uwezo wako. Kumbuka umahiri wako ndiyo
utakaokuajiri. Ukifika chuo masomo yawe kipaumbele wakati ukifanya mengine kama
itakulazimu. Ukifikiria ajira kutokana na taaluma yako hutasoma kwa amani, soma
mambo mazuri huja mbele ya safari.
2.7. CHAGUA CHUO NA TAALUMA KULINGANA NA UFAULU WAKO
Kumekuwepo na
tabia ya watu kung'ang'ania kuchagua taaluma fulani ama vyuo fulani kutokana na
jinsi wanavyopenda wao na sifa na hadhi za vyuo watakavyo pasipokuzingatia
ufaulu wao. Wengi wamejikuta wakikosa nafasi za masomo kwa mwaka husika, hii
inatokana na kung'ang'ania chuo kutokana na hadhi yake ilihali mtu ana ufalu
mdogo kushindana na wenye ufaulu mkubwa. Hakikisha ufaulu wako unakidhi vigezo
vya ushindani wa taaluma na vyuo unavyochagua. Kama ufaulu wako ni wa chini ni
vyema kutafuta taaluma na vyuo ambazo entry qualifications zinaendana na ufaulu
wako. Usipozingatia hili utapoteza muda kurudia zoezi la udahili ama utakosa kabisa
nafasi kwa mwaka husika. Zingatia kwamba ufaulu wako ndiyo ushindani wako.
Usipochaguliwa katika chuo na taaluma fulani hakikisha una mbadala mwingine wa
chuo na si kung'ang'ania uchaguzi ambao hujachaguliwa. Na uzuri wa siku hizi ni
kwamba usipochaguliwa taaluma fulani unapewa na sababu, usipuuze sababu hizo.
2.8. FANYA UAMUZI SAHIHI NA UTUME MAOMBI KATIKA VYUO UNAVYOVIPENDA
Baada ya
kuridhika na machaguo yako ya taaluma, hakikisha umechagua machaguo sahihi bila
kukurupuka na kisha tuma maombi vyuoni. Kwa sasa maombi yanatumwa kwenye vyuo
husika ama kwa kupeleka maombi chuo moja kwa moja ama kwa kutumia njia ya
mtandao na sio kupitia TCU kama ilivyokuwa miaka iliyopita. Njia ya mtandao ni
rahisi sana ufatiliaji wake kuliko kupeleka maombi kwa njia ya barua.
3.0. MAMBO MENGINE YA KUZINGATIA
Hapo juu nimeainisha
mambo ya muhimu kwa uchaguzi wa taaluma hasa vyuo vya ndani. Hapa chini
nimeeleza kwa ufupi mambo ya jumla kuhusu uchaguzi utakaoufanya, sababu
nyingine zaweza kukinzana na maelezo hapo juu kuliangana na mtazamo wa mtu.
3.1. SOKO LA AJIRA
Kama wewe ni mtu
wa kuzingatia sana soko la ajira ni muhimu kwako kufanya utafiti kufahamu taaluma
ambazo zina wigo mpana wa ajira ama zinazoajiri sana na hata zile ambazo zina
uchache wa wataalamu. Wigo mpana wa ajira ni kuingia katika idara mbalimbali za
ajira na kuweza kuendana na idara hizo bila kufundishwa sana au tena baada ya
kumaliza masomo. Ajira zinazoajiri sana ni zile ambazo tasisi huhitaji watu
wengi mara nyingi kulingana na umuhimu wake ingawa taaluma zote ni muhimu. Ajira
zenye uchache wa wataalamu ni zile ambazo watu hawajasoma sana taaluma hizo
kutokana na upya wake.
3.2. MSHAHARA NA MUDA
Ijapokuwa jambo
unalolipenda ni muhimu zaidi, suala la mshahara ni la muhimu pia. Zingatia mshahara
na malupulupu mengine na faida utakazozipata katika taaluma unayotaka kusoma
kulingana na matarajio yako ya baadaye. Suala la muda pia ni muhimu kwa sababu
zipo taaluma zitakuhitaji kupatikana hata katika muda wa zaida hata baada ya
saa za kawaida za kazi.
3.3. UWIANO KATI YA KAZI NA MAISHA
Chunguza namna
taaluma unayochagua itaathiri muda wa kazi na maisha yako binafsi , familia na
matarajio yako mengine.
3.4. UKUAJI NA MAENDELEO
Zingatia ukuaji
wako kitaaluma na maendeleo yako binafsi. Chagua taaluma ambayo itakupa wigo
mpana wa kukua na kuendelea binafsi na kuendeleza taaluma husika yaani kuwa na
mchango chanya katika maisha yako na taaluma yenyewe.
3.5. MALENGO ENDELEVU
Fikiria kuhusu malengo
yako katika miaka ijayo. Je taaluma hiyo itakusaidia kufika huko ama utakuwa
mtu wa kujilaumu tu na kujuta kwa nini uliichagua kuisoma? Fikiria kwa makini
sana.
3.6. AFYA YAKO NA UZIMA
Hakikisha kwamba
unakuwa katika taaluma ambayo inajali afya yako na uzima. Zipo baadhi ya
taaluma huchosha mwili na akili pia, ni muhimu kuzifahamu ili ufahamu namna ya
kukabiliana na changamoto hizo.
3.7. MAZINGIRA NA UTAMADUNI WA KAZI
Baadhi ya taaluma
zitakufanya uwe mtu wa kusafiri na kuhama hama sana. Hakikisha unakuwa tayari kumudu
mambo hayo. Pia fikiria kuhusu utamaduni na miiko ya taaluma husika kama
inaendana na tabia zako.
4.0. MUHTASARI NA MAELEZO MENGINE
Mara baada ya
kufanya maombi kila Chuo hufanya utaratibu wa udahili kwa mfumo wa ushindani
walioweka wenyewe lakini utaratibu huo lazima uendane na vigezo vya Tume ya
Vyuo Vikuu nchini (TCU). Katika zama hizi za kila Chuo kufanya udahili wenyewe
kunawapa nafasi ya wao kuchagua wale wanaowataka kulingana na vigezo vyao, kwa
hiyo unashauriwa kuangalia ufaulu wako hasa idadi ya alama ulizo nazo (cutting
points) katika mchepuo/tahasusi uliyosoma Kidato cha Sita ama ufaulu wako
katika ngazi ya Stashahada (Diploma) wakati mwingine hata matokeo ya Kidato cha
Nne huangaliwa. Kwa ufupi ni kwamba wenye alama za juu huwa na uwezekano mkubwa
wa kuchaguliwa ukilinganisha na wenye alama za chini.
Vyuo vinapomaliza
uchambuzi na udahili hutangaza majina ya wale waliochaguliwa kujiunga na vyuo
hivyo moja kwa moja ama waliochaguliwa hapo na kuchaguliwa kwingineko, kwa hiyo
hapa mdahiliwa hutakiwa kuchagua chuo kimoja na taaluma moja na kisha
kuthibitisha chuo na taaluma apendayo kuisoma. Aidha vyuo pia hutoa sababu za
kwa nini wadahiliwa wengine hawakufanikiwa kuchaguliwa na mara nyingi sababu
hizo si za kupuuzia hata kidogo hasa ukiambiwa hujafikisha alama za ushindani
ama kutokidhi vigezo vya taaluma husika. Mdahiliwa hutakiwa kuzingatia sababu
hizo za kutochaguliwa na kujaribu awamu nyingine. Utaratibu huwa ni uleule
lakini katika awamu zinazofuata taaluma fulani huondolewa kwenye mfumo kutokana
na kuuwa zimesjaa wadahiliwa na hii ndiyo maana unasisitizwa kusoma taarifa kwa
kina kuhusu uchaguzi wako wa taaluma.
Utaratibu
huendelea hivyo mpaka awamu zote zitakapokwisha. Jambo la muhimu ni kwamba kuna
wakati usipozingatia baadhi ya maelezo unaweza kukosa nafasi ya chuo kwa mwaka
husika hasa kutozingatia ufaulu wako ama niseme idadi ya alama ulizo nazo
katika mchepuo ama Stashahada yako. Ni muhimu sana kuwa makini. Jambo lingine
la muhimu tena ni kuhakikisha taarifa zako binafsi zinakua sahihi kwenye mfumo
wa udahili. Zingatia yote niliyoyaeleza hapa kuepuka usumbufu.
Unaweza kumtafuta
mtu mwenye ufahamu wa mambo haya akakuelekeza vizuri zaidi ama unaweza
kuwasiliana name kwa namba nilizoweka hapa chini. Huwa natoa ushauri huu BURE
kabisa niapokuwa na muda. Mawasiliano yangu yapo hapa chini.
Makala haya yameandaliwa na kuandikwa na
Venance Gilbert
Mwalimu, Shahada ya Kwanza ya Elimu
katika Lugha na Menejimenti (BED-LM)
Chuo Kikuu Mzumbe
venancegilbert@gmail.com
0753400208.
Yalichapishwa mara ya kwanza 25/07/2017 yamefanyiwa marekebisho 05/06/2024.
Comments
Post a Comment