SHAIRI: HEKO LIBERIA

Picha kwa hisani ya Freepik


Shairi hili linakuja kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka huu nchini Liberia. Katika hali isiyo ya kawaida George Weah aliyekuwa akitetea nafasi yake alikubali kusindwa na mpinzani wake Joseph Boakai katika Uchaguzi huo pasipo mvutano na migogoro kama ilivyozoeleka katika mataifa mengi ya bara hili. Kama mshairi niliwiwa kuandika ili kupongeza kitendo hiki cha uungwana kukubali kukabidhi madaraka pasipo mvutano ambao mara nyingi hupelekea umwagaji damu. Karibu katika shairi letu kwa lugha adhimu ya Kiswahili.

Shairi: Heko Liberia
Mtunzi: Venance Gilbert Mpate
Mwaka: 19 Novemba 2023

HEKO LIBERIA

Heko Liberia naisifu yenu demokrasia,
Wenu ukomavu yote Afrika imeshuhudia,
Tupeni maarifa darasani tupate kujifunzia,
Afrika matokeo mshindani hawezi kuridhia,
Uchaguzi mtawala hakubali kupoteza felia,
Ninyi metuonesha mtawala aweza kuwa felia,
Mpinzani akashika dola imani ikaendelea,
Heko Liberia naisifu yenu demokrasia.

Mtawala akubali mwenyewe kupoteza,
Dola pembeni madarakani kumbakiza,
Tume uchaguzi naipongeza kujitakatifuza,
Afrika demokrasia miguu yajikomaza,
Kwingine tuanze maarifa kupenyeza,
Yeyote uchaguzini aweza kupoteza,
Hakika demokrasia haitakuwa ajuza,
Heko Liberia naisifu yenu demokrasia.

Afrika ikome migogoro uchaguzini,

Pumzi tulonayo watawala iheshimuni,

Vita uchaguzini visalie historiani,

Itamalaki demokrasia kote barani,

Furahani tuishi mwetu majumbani,

Yafaa nini kuwemo migogoroni?

Afrika Afrika tuishi demokrasiani,

Heko Liberia naisifu yenu demokrasia.



Kama una maoni kuhusu shairi hili usisite kuandika hapa chini ama kuniandikia katika barua pepe yangu: venancegilbert@gmail.com