YAFAHAMU HAYA KUTOKA BODI YA MIKOPO (HESLB)
Jana katika kipindi cha Dakika 45 ambacho hurushwa kila Jumatatu saa 3 usiku kupitia ITV/Radio One, Sam Mahela mtangazaji wa kipindi hicho alipata nafasi ya kufanya mahojiano na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo, Mh. Abdul Razaq Badru ambaye ameteuliwa na Waziri wa Elimu Prof. Ndalichako kufahamu mambo fulani kuhusu HESLB.
Mkurugenzi huyo alianza kwa kubainisha kuwa tangu kuanzishwa kwake HESLB imekopesha watu laki tatu na ishirini na nne (300,024). Aliongeza kuwa makato ya fedha kwa wale ambao walinufaika na mikopo ya elimu ya juu yanaendelea. Pia alibainisha kwamba kumekuwepo na dosari katika kuwakata watu 200 ambao hawakuwahi kunufaika na mikopo ya elimu ya juu na kusisitiza kwamba kama kuna mtu anakatwa na hakukopeshwa na bodi hiyo atoe taarifa katika Ofisi zilizojirani naye. Lakino pia alidai kuwa waliokatwa kimakosa watarudishiwa fedha zao.
Mkurugenzi aliongeza kuwa Bodi imekopesha jumla ya Tsh. Trilioni 2.4 (waliowahi kukopeshwa na wanaondelea na masomo kwa mwaka 2015/2016) na kwamba kiasi kilichorejeshwa ni Tsh Bilioni 284 na zilizokusanywa ni kiasi cha Tsh Bilioni 105. Mkurugenzi alibainisha kuwa kwa mwaka wa masomo/fedha 2015/2016 ilitakiwa mkopo jumla utolewe Tsh Bilioni 400 na kiasi kadhaa lakini Rais Magufuli alipoingia madarakani aliongeza kiasi cha Tsh Bilioni 132. Ikumbukwe kwamba fedha hizi ni zile za kujikimu, vitabu na maktaba, ada ya chuo pamoja na gharama ya mafunzo kwa vitendo.
Kuhusu kukatwa fedha kwa wafanyakazi walioajiriwa katika taasisi binafsi Mkurugenzi alidai kuwa elimu inatolewa kwa waajiri kuhusu kukata fedha hiyo kwa mujibu wa sheria. Aidha Mkurugenzi aliongeza kwamba muda wa kurejesha mkopo huo ni baada ya miaka 10 toka mnufaika amalize masomo yake bila kujali ameajiriwa au la! Aliongeza kuwa inapopita miaka 10 bila mnufaika kujeresha kiasi hicho, kunakuwa na faini ya 6% kwa mwaka kwa jumla ya miaka yote ambayo mnufaika atakuwa amechelewa kurejesha mkopo.
Kuhusu mwaka wa masomo 2016/2017, Mkurugenzi alidai kuwa wanafunzi elfu themanini na nane 88,000 ndiyo wameomba kunufaika na mikopo hiyo na kwamba zoezi la kupitia wenye sifa za kukopeshwa bado linaendelea.
Lakini pia Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa mpaka sasa Vyuo vimerejesha kiasi cha Tsh Bilioni 1 na laki 2 (1,000,200,000/=) kati ya Tsh Bilioni 2 na laki 7 (2,000,700,000/=) fedha ambazo zilitumika kwa wanafunzi hewa. Hili alilibainisha alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Sam Mahela kuhusu kiasi cha Tsh Bilioni 14 (14,000,000,000) kutumika kuwalipa wanafunzi hewa.
Aidha Mkurugenzi huyo alisema kwamba kuhusu utoaji wa mikopo unafata vigezo kama muombaji anafaa. Hili alilibainisha wakati akijibu swali kuhusu kushuka kwa udahili wa waliosoma Diploma kutoka GPA ya 3.5 hadi 3.0 kama wanaweza kunufaika na mkopo kutoka HESLB. Mkurigenzi alibainisha kuwa watu wenye mahitaji mkubwa kama vile Yatima, Walemavu na Wale wanaotoka katika hali duni pamoja na Watakaosoma kozi za uhandisi, uhandisi wa mafuta na gesi, Ualimu wa Sayansi na Hisabati pamoja na Udaktari hao watapakuwa na kipaumbele kunufaika na mkopo wa Elimu ya Juu.
Mkurugenzi alipoulizwa kuhusu wanafunzi waliokuwa wakisoma Diploma maalum ya Ualimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma na kuhamishiwa katika vyuo vingine kama wanaweza kunufaika tena mikopo, alidai kuwa utaratibu maalumu utatolewa na Serikali panapostahili.
Mkurugenzi pia alibainisha kuwa Bodi ya Mikopo (HESLB) inafanya kazi kwa ushirikiano kabisa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na kwamba ili mwanafunzi apatiwa mkopo sharti adailiwe kupitia TCU kama kigezo cha kwanza kupata mkopo wa Elimu ya Juu na kuwatoa hofu wanafunzi, wazazi na wadau wa Elimu kuhusu kuwepo awamu mbalimbali za Udahili TCU kuwa hakutokwamisha suala la ukopeshwaji kwa wenye sifa stahiki.
Pia alibainisha kuwa kiasi cha fedha Tsh Bilioni Mia tano (500,000,000,000) zimetengwa na Wizara kuhudumia mikopo ya Wanafunzi wa elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2016/2017.
Comments
Post a Comment